Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 75
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Uteremsho wa Kitabu (hiki) umetoka kwa Mwenyeezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
2. Kwa hakika sisi tumekuteremshia Kitabu kwa haki. basi muabudu Mwenyeezi Mungu kwa kumtii halisi.
3. Sikilizeni! Utii halisi ni haki ya Mwenyeezi Mungu, lakini wale wnaowafanya wengine kuwa waungu badala yake (husema): Sisi hatuwaabudu hawa ila wapate kutufikisha karibu kabisa na Mwenyeezi Mungu. Hakika Mwenyeezi Mungu atahukumu baina yao katika yale wanayohitilafiana. Bila shaka Mwenyeezi Mungu hamuongozi aliye muongo, aliye kafiri.
4. Kama Mwenyeezi Mungu angelitaka kupata mtoto, bila shaka angelichagua amtakaye miongoni mwa aliowaumba. Lakini Yu mbali na hayo, yeye ni Mwenyeezi Mungu Mmoja, Mwenye kufanya atakalo.
5. Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, hufunika usiku juu ya mchana, na hufunika mchana juu ya usiku, na amevitiisha jua na mwezi, vyote huenda kwa muda uliowekwa jueni kuwa yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.
6. Amekuumbeni katika nafsi moja, kisha akamfanya mweziwe katika jinsi yake, na akakuumbieni wanyama, wanane madume na majike. Hukuumbeni matumboni mwa mama zenu umbo baada ya umbo katika giza tatu. Huyo ndiye Mwenyeezi Mungu Mola wenu, Ufalme ni wake hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, basi nyinyi mnageuzwa wapi?
7. Mkikufuru, basi hakika Mwenyeezi Mungu hana haja nanyi, wala haridhii kufru kwa waja wake, na kama mkishukuru, hayo atawaridhieni, wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine, kisha marudio yenu ni kwa Mola wenu, basi atakuambieni yale mliyokuwa mkifanya. Bila shaka yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
8. Na taabu inapomfikia mtu humuomba Mola wake akielekea kwake, kisha akimpa neema kutoka kwake, husahau yale aliyokuwa akimwitia zamani, na kumfanyia Mwenyeezi Mungu washirika ili apoteze (watu) katika njia yake, sema: Starehe kwa kufru yako muda kidogo, hakika wewe ni miongoni mwa watu wa Motoni.
9. Je, afanyaye ibada wakati wa usiku kwa kusujudu na kusimama na kuogopa Akhera na kutarajia rehema za Mola wake (ni sawa na asiyefanya hayo?) sema: Je, wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua? Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu.
10. Sema: Enyi waja wangu mlioamini! mcheni Mola wenu, wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema, na ardhi ya Mwenyeezi Mungu ina wasaa, bila shaka wanaofanya subira watapewa malipo yao pasipo hesabu.
11. Sema: Hakika nimeamrishwa nimuabudu Mwenyeezi Mungu kwa kumfuata Yeye tu.
12. Na nimeamrishwa kwamba niwe wa kwanza wa waliojisalimisha.
13. Sema: Mimi naogopa adhabu ya siku kubwa kama nikimuasi Mola wangu.
14. Sema: Hakika nimeamrishwa nimuabudu Mwenyeezi Mungu kwa kumtakasia utii wangu.
15. Basi nyinyi abuduni mnachopenda kinyume chake, sema: Hakika watakaopata khasara ni wale waliozitia khasarani nafsi zao na watu wao siku ya Kiyama. Angalieni! hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.
16. Yatawekwa juu yao matabaka ya Moto na chini yao matabaka, hayo Mweenyeezi Mungu huogopesha nayo waja wake: Enyi waja wangu! Nicheni.
17. Na wale wanaojiepusha na ibada potovu, na wakarejea kwa Mwenyeezi Mungu, watapata biashara njema. basi wabashirie waja wangu.
18. Ambao husikiliza kauli (nyingi zinazo semwa) kisha wakafuata zilizo nzuri zaidi. Hao ndio aliowaongoza Mwenyeezi Mungu, na hao ndio wenye akili.
19. Je, iliyemuwajibikia hukumu ya adhabu Je, unaweza kumuokoa aliyomo katika Moto?
20. Lakini waliomcha Mola wao watapata ghorofa zilizojengwa juu ya ghorofa, chini yake hupita mito, ndiyo ahadi ya Mwenyeezi Mungu, Mwenyeezi Mungu havunji ahadi.
21. Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu ameteremsha maji kutoka mawinguni, kisha akayapitisha (chini kwa chini) yakawa chemchem katika ardhi, tena akaotesha kwayo mimea ya rangi mbali mbali, kisha hunyauka, ukaiona imekuwa kimanjano, kisha huifanya kusagika sagika. Bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa wenye akili.
22. Je, mtu ambaye Mwenyeezi Mungu amemfungulia kifua chake kuukubali Uislaamu, naye yuko katika nuru itokayo kwa Mola wake (ni sawa na mwenye moyo mgumu?) Basi adhabu kali kwa wale wenye nyoyo ngumu, kumkumbuka Mwenyeezi Mungu, hao wamo katika upotovu dhahiri.
23.Mwenyeezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa. Kitabu chenye maneno yanayopatana (na) yanayokaririwa, husisimka kwayo ngozi za wale wanaomuogopa Mola wao, kisha ngozi zao na nyoyo zao huwa laini kwa kumkumbuka Mola wao. Huo ndio muongozo wa Mwenyeezi Mungu, kwa huo humuongoza amtakaye, na anayepotezwa na Mwenyeezi Mungu, basi hakuna wa kumuongoza.
24. Je, yule ajilindaye uso wake na adhabu mbaya siku ya Kiyama (ni sawa na asiyejilinda?) Na waliodhulumu wataambiwa: Onjeni mliyokuwa mkiyachuma.
25. Waliokuwa kabla yao walikadhibisha, na adhabu ikawafikia kutoka mahala wasipopatambua.
26. Basi Mwenyeezi Mungu akawaonjesha fedheha katika maisha ya dunia, na adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi, laiti wangelijua!
27. Na bila shaka tumewapigia watu mifano ya kila namna katika hii Qur’an ili wapate kukumbuka.
28. Qur’an yenye kufafanua, isiyo na upotovu ili wajilinde.
29. Mwenyeezi Mungu amekupigieni mfano wa mtu mwenye washirika wanaogombana, na wa mtu mwingine aliye husika na mtu mmoja, je, wako sawa katika hali? Alhamdu lillahi! lakini wengine wao hawajui.
30. Kwa hakika wewe utakufa, na hakika wao (pia) watakufa.
31. Kisha bila shaka mtagombana siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu.
32. Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia uongo juu ya Mwenyeezi Mungu na kukadhibisha kweli imfikiapo? Je, siyo katika Jahannam makazi ya makafiri?
33.Na aliyeleta ukweli na aliyeusadikisha, hao ndio wamchao (Mwenyeezi Mungu).
34. Watapata watakachopata kwa Mola wao, hayo ndiyo malipo ya watendao mema.
35. Ili Mwenyeezi Mungu awafutie ubaya walioufanya na kuwalipa malipo yao kwa wema waliokuwa wakifanya.
36. Je Mwenyeezi Mungu hamtoshei mja wake? Na wanaokukhofisha kwa wale walio kinyume chake, na aliyepotezwa na Mwenyeezi Mungu, basi hana kiongozi.
37. Na ambaye Mwenyeezi Mungu anamuongoza hakuna awezaye Kumpoteza. Je, Mwenyeezi Mungu si Mwenye nguvu, Mwenye kisasi?
38. Na ukiwauliza: Ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi? Bila shaka watasema: Mwenyeezi Mungu. Sema: Je, mnawaonaje wale mnaowaomba kinyume cha Mwenyeezi Mungu, kama Mwenyeezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema yake? Sema: Mwenyeezi Mungu ananitosha, kwake wategemee wanaotegemea.
39. Sema: Enyi watu wangu! fanyeni mahala penu (mtakavyo) mimi pia nafanya, basi hivi karibuni mtajua.
40. Na nani itakayemfikia adhabu ya kumfedhehesha na itakayemshukia adhabu yenye kuendelea.
41. Kwa hakika tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu kwa haki, basi anayeongoka ni kwa nafsi yake, na anayepotea bila shaka anapotea kwa hasara (ya nafsi) yake, na wewe siye mlinzi wao.
42. Mwenyeezi Mungu hupokea roho wakati wa mauti yao, na zile zisizokufa, katika usingizi wao. Basi huzizuia zile alizozihukumia kufa, na huzirudisha nyingine mpaka wakati uliowekwa bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaotafakari.
43. Au wamejifanyia waombezi kinyume cha Mwenyeezi Mungu? Sema: Ingawa hawana mamlaka juu ya kitu chochote wala hawatambui?
44. Sema: Uombezi wote ni kwa Mwenyeezi Mungu, ufalme wa mbingu na ardhi ni wake, kisha mtarejeshwa kwake.
45. Na anapotajwa Mwenyeezi Mungu peke yake nyoyo za wale wasioamini Akhera huchukia, na wanapotajwa wale walio kinyume naye, mara wanafurahi.
46. Sema: Ewe Mola! Muumba wa mbingu na ardhi, Mjuzi wa yasiyoonekana na yanayoonekana, wewe utahukumu baina ya waja wako katika yale waliyo kuwa wakikhitilafiana.
47. Na kama madhalimu wangelikuwa na vyote vinavyopatikana ardhini, na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila shaka wangelivitoa kujikombolea katika adhabu mbaya siku ya Kiyama, na yatawadhihirikia kutoka kwa Mwenyeezi Mungu ambayo hawakuwa wakiyatazamia.[1]
48. Na utawadhihirikia ubaya wa yale waliyoyachuma, na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
49. Na dhara inapomgusa mwanadamu hutuomba, kisha tunapompa neema zitokazo kwetu husema: Nimepewa kwa sababu ya ujuzi (wangu) Siyo! huo ni mtihani, lakini wengi wao hawajui.
50. Wamekwisha sema haya wale wa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.
51. Basi ukawapata ubaya wa yale waliyochuma, na wale waliodhulumu miongoni mwa hawa utawapata ubaya wa yale waliyoyachuma nao si wenye kumshinda (Mwenyeezi Mungu).
52. Je, wao hawajui kwamba Mwenyeezi Mungu hutoa riziki nyingi kwa yule amtakaye na hudhikisha? kwa hakika katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaoamini.
53. Sema: Enyi waja wangu mliojidhulumu wenyewe! msikate tamaa katika rehema za Mwenyeezi Mungu, bila shaka Mwenyeezi Mungu husamehe dhambi zote, hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu.
54. Na rejeeni kwa Mola wenu na mnyenyekee kwake kabla ya kukufikieni adhabu, kisha hamtasaidiwa.
55. Na fuateni yaliyo bora katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu kabla ya kukufikieni adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui.
56. Isije ikasema nafsi yoyote: Ole wangu kwa yale niliyopunguza upande wa Mwenyeezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wafanyao mzaha.
57. Au ikasema: Kama Mwenyeezi Mungu angeniongoza, bila shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye kumcha (Mwenyeezi Mungu).
58. Au ikasema ionapo adhabu: Kama ningepata marejeo ningekuwa miongoni mwa wafanyao mema.
59. Naam! lakini ukazikadhibisha na ukajivuna na ukawa miongoni mwa makafiri.
60. Na siku ya Kiyama utawaona wale waliomsingizia uongo Mwenyeezi Mungu nyuso zao zimekuwa nyeusi. Je, si katika Jahannam makazi ya wale wanaotakabari?
61. Na Mwenyeezi Mungu atawaokoa wale wamchao kwa ajili ya kufaulu kwao, hautawagusa ubaya wala hawatahuzunika.
62. Mwenyeezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu na yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu.
63. Funguo za mbingu na ardhi ziko kwake, na wale waliozikataa Aya za Mwenyeezi Mungu hao ndio wenye khasara.
64. Sema: Je, mnaniamuru niabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu, enyi wajinga!
65. Na kwa hakika yamefunuliwa kwako na kwa wale waliokuwa kabla yako: Kama ukishirikisha, bila shaka vitendo vyako vitaharibika na lazima utakuwa miongoni mwa wenye khasara.
66. Bali muabudu Mwenyeezi Mungu na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.
67. Na hawakumheshimu Mwenyeezi Mungu heshima impasayo, na siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kulia, ameepukana na upungufu na yu juu kabisa kuliko yale wanayo mshirikisha.
68. Na litapigwa baragumu ndipo watazimia waliomo mbinguni na waliomo ardhini ila yule amtakaye Mwenyeezi Mungu. Tena litapigwa mara nyingine, ndipo watasimama wakiangalia.
69. Na ardhi itang’aa kwa nuru ya Mola wake, na daftari (ya vitendo) itawekwa na wataletwa Manabii na Mashahidi na itahukumiwa kati yao kwa haki wala hawatadhulumiwa.
70. Na kila nafsi itapewa sawa sawa yale iliyoyafanya naye anajua sana wanayoyatenda.
71. Na waliokufuru watapelekwa kwenye Jahannam makundi kwa makundi, mpaka watakapoifikia itafunguliwa milango yake na walinzi wake watawaambia: Je, hawakukufikieni Mitume kutoka miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu na kukuonyeni mkutano wa siku yenu hii? Watasema: Ndiyo, lakini limetimia neno la adhabu juu ya makafiri.
72. Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannam mkakae humo milele basi ni ubaya ulioje wa makazi ya wanaotakabari.
73. Na waliomcha Mola wao watapelekwa Peponi vikundi vikundi mpaka watakapoifikia na milango yake itafunguliwa, na walinzi wake watawaambia: Amani juu yenu, furahini, basi ingieni humo mkakae milele.
74. Nao watasema: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, ambaye ametutimizia ahadi yake na ameturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote tupendapo, basi ni malipo mazuri yaliyoje kwa watendao (mema).
75. Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa kiti cha enzi wakimtukuza kwa kumsifu Mola wao. Na itahukumiwa kati yao kwa haki na itasemwa: Alhamdu lillahi rabbil a’lamin” (Yaani) kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, Mola wa walimwengu.