Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 89
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Haa mym.
2. Naapa kwa kitabu kilichobainisha.
3. Kwa hakika tumeifanya Qur’an kuwa ya uwazi ili mfahamu.
4. Na bila shaka hii imo katika Kitabu cha asili kilichoko kwetu, imetukuka, yenye hekima.
5. Je, tuache kukukumbusheni kwa sababu mmekuwa watu mliopita kiasi?
6. Na tuliwapeleka Manabii wangapi katika watu wa zamani?
7. Na hakuwafikia Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.
8. Basi tuliwaangamiza waliokuwa na nguvu zaidi kuliko hao, na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita.
9. Na ukiwauliza: Ni nani ameziumba mbingu na ardhi? Lazima watasema: Ameziumba Mwenye nguvu, Mwenye kujua.
10. Ambaye amekufanyieni ardhi kuwa tandiko, na akakufanyieni njia ndani yake ili muongoke.
11. Na ambaye ameteremsha maji mawinguni kwa kiasi, na kwa hayo tukaufufua mji uliokufa, hivyo ndivyo mtakavyotolewa.
12. Na ambaye ameumba dume na jike katika kila kitu, na akakufanyieni jahazi na wanyama mnaopanda.
13.Ili mkae mgongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Atukuzwe yeye aliyetutiisha haya tusingeliweza kutenda haya wenyewe.
14. Na bila shaka sisi tutarudia kwa Mola wetu.
15. Na wanamfanyia katika waja wake sehemu, kwa hakika mwanadamu hakufuru wazi wazi.
16. Je, amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyoviumba, na kukuchagulieni nyinyi watoto wanaume?
17. Na anapoambiwa mmoja wao yale aliyompigia mfano Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema, uso wake huwa mweusi na huhuzunika sana.
18. Je, aliyelelewa katika mapambo naye katika mabishano hawezi kusema bayana!.
19. Na wanawafanya Malaika ambao ni waja wa Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema, kuwa wanawake. Je, wameshuhudia. kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wataulizwa.
20. Na husema: Angelipenda Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema tusingewaabudu. Hawana elimu ya hayo, hawasemi ila kukisia tu.
21.Je, tumewapa Kitabu kabla ya hiki, wakawa wameshikamana nacho?
22. Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu juu ya desturi na tunafuata nyayo zao.
23. Na kadhalika hatukumpeleka muonyaji katika mji wowote ila matajiri wake walisema: Kwa hakika tuliwakuta baba zetu juu ya desturi na hakika sisi tunafuata nyao zao.
24. Akasema: Hata kama nakuleteeni (desturi) yenye muongozo bora kuliko mliyowakuta nayo baba zenu? wakasema: Kwa hakika sisi tunayakataa yale mliyotumwa nayo.
25. Ndipo tukawaangamiza, basi angalia ulikuwaje mwisho wa waliokadhibisha.
26. Na (kumbuka) Ibrahimu alipomwambia Baba yake na watu wake: Bila shaka mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyaabudu.
27. Isipokuwa yeye aliyeniumba, kwani yeye ataniongoza.
28. Na akalifanya neno hili liwe lenye kubaki katika kizazi chake ili warejee.
29. Basi niliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ukawafikia ukweli na Mtume abainishaye.
30. Na ulipowafikia ukweli wakasema: Huu ni chawi na hakika sisi tunaukataa.
31. Na wakasema: Mbona Qur’an hii haikuteremshwa juu ya mtu mkubwa katika miji miwili?
32. Je wao wanaigawa rehema ya Mola wako? Sisi tumewagawanyia maisha yao katika uhai wa dunia, na tumewainua baadhi yao daraja (kubwa) juu ya wengine, ili baadhi yao wawafanye wengine kuwa watumishi, na rehema za Mola wako ni bora kuliko wanayoyakusanya.[1]
33. Na isingekuwa watu watakuwa kundi moja, bila shaka tungelifanya dari za nyumba za watu wanaomkufuru Rahmani kwa fedha, na ngazi wanazopandia.
34. Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyoegemea juu yake.
35. Na mapambo, lakini hayo yote si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia, na Akhera mbele ya Mola wako ni ya wenye kumcha (Mwenyeezi Mungu).
36. Na anayeyafanyia upofu maneno ya Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema, tutamuwekea shetani naye anakuwa rafiki yake.
37. Na kwa hakika hao wanawazuilia njia nao hudhani kwamba wanaongoka.
38. Hata atakapotufikia, atasema: Laiti ungelikuwa umbali wa mashariki na magharibi kati yangu na wewe, ni urafiki mbaya ulioje!
39. Na haitakufaeni leo mlipodhulumu kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu.
40. Je, unaweza kumsikilizisha kiziwi, au unaweza kumuongoza kipofu na aliyomo katika upotovu ulio wazi?
41. Na kama tukikuondoa, basi hakika sisi tutajilipiza kisasi kwao.[2]
42. Au tutakuonyesha tuliyowaahidi, nasi bila shaka tuna uwezo juu yao.
43. Basi yashike yaliyofunuliwa kwako, bila shaka umo katika njia iliyonyooka.
44.Na kwa hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa watu wako, na karibu mtaulizwa.
45. Na kawaulize Mitume wetu tuliowapeleka kabla yako; Je, tulifanya miungu mingine badala ya Mwenyeezi Mungu mwingi wa rehema iabudiwayo?
46. Na bila shaka tulimtuma Musa na Aya zetu kwa Firaun na wakuu wake, akasema: Kwa hakika mimi ni Mjumbe wa Mola wa walimwengu.
47. Lakini alipowafikia na hoja zetu, mara wao wakazicheka.
48. Na hatukuwaonyesha hoja yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko yenziye, na tukawakamata kwa adhabu ili warudi (kwetu).
49. Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako aliyokuahidi, kwa hakika tutakuwa wenye kuongoka.
50. Basi tulipowaondolea adhabu. mara wakavunja (mapatano)
51. Na Firaun alitangaza katika watu wake akisema; Enyi watu wangu! je, utawala wa Misri si wangu, na pia mito hii ipitayo chini yangu? je, hamuoni?
52. Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge wala hawezi kusema wazi wazi?
53. Basi mbona hakuvishwa bangili za dhahabu, au kuja Malaika pamoja naye wakimuandama?
54. Na akawapumbaza watu wake, nao wakanitii, kwa hakika wao walikuwa watu waasi.
55. Basi walipotukasirisha tuliwaangamiza na tukawagharikisha wote.
56. Kisha tukawafanya kuwa mfano na hadithi kwa watu wa baadaye.
57. Na alipopigiwa mfano mwana wa Mariam, mara watu wako wakaupigia kelele.
58. Na husema: Je, miungu yetu ni bora au yeye? Hawakuelezi hayo ila kwa kujadiliana tu, bali hao ni watu wagomvi.
59. Yeye siye ila ni mja tuliyemneemesha na tukamfanya mfano kwa wana wa Israeli.
60. Na kama tungelipenda tungeliwafanya Malaika (kuwa makhalifa) katika ardhi badala yetu.
61. Na kwa hakika yeye ni elimu ya Kiyama msikifanyie shaka na nifuateni: Hii ndiyo njia iliyonyooka.
62. Wala asikuzuieni shetani, bila shaka yeye kwenu ni adui dhahiri.
63. Na alipofika Isa kwa dalili zilizo wazi, akasema: Nimekujieni na elimu na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyokhitilafiana basi mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.
64. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu ndiye Mola wangu na Mola wenu, basi Mwabuduni, hii ndiyo njia iliyonyooka.
65. Lakini makundi yakakhitilafiana wao kwa wao, basi ole wao waliodhulumu kwa adhabu ya siku yenye kuumiza.
66. Hawangojei ila Kiyama tu kuwafikia kwa ghafla, hali hawatambui. 67. Marafiki siku hiyo watakuwa maadui wao kwa wao, ila wenye kumcha (Mwenyeezi Mungu).
68. Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika.
69. Ambao waliziamini Aya zetu na walikuwa Waislamu.
70. Ingieni katika Bustani nyinyi na wake zenu mtafurahishwa.
71. Watatembezewa sahani za dhahabu na vikombe, na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele.
72. Na hiyo ni Bustani mliyorithishwa kwa hayo mliyokuwa mkiyafanya.
73. Yamo matunda mengi kwa ajili yenu mtakayokula.
74. Kwa hakika waovu watakaa milele katika adhabu ya Jahannam.
75. Hawatapunguziwa nao humo watakata tamaa.
76. Wala sisi hatukuwadhulumu, bali wao wenyewe walikuwa madhalimu.
77. Nao watamwita: Ewe Malik! na atufishe Mola wako! (Malik) atasema: Bila shaka mtakaa mumo humo.
78. Kwa hakika tumekuleteeni haki, lakini wengi wenu haki mnaichukia.
79. Au wamekata shauri? Bali kwa hakika sisi ndio tunao pitisha.
80. Au wanadhani kuwa hatusikii siri zao na minong’ono yao? Naam, na Wajumbe wetu wako karibu nao wanayaandika.
81. Sema: Kama Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema angelikuwa na mtoto, ningelikuwa wa kwanza wa kumuabudu.
82. Ameepukana Mola wa mbingu na ardhi, Mola wa Arshi na hayo wanayomsifia.
83. Basi waache wapige porojo na wacheze mpaka wakutwe na siku yao wanayo ahidiwa.
84. Na yeye ndiye anayeabudiwa mbinguni na anayeabudiwa ardhini, naye ni Mwenye hekima, Mwenye elimu.
85. Na Mwenye baraka ni yule ambaye ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake ni wake, na uko kwake ujuzi wa (kujua) Kiyama, na kwake mtarudishwa.
86. Wala hawana uwezo wa uombezi wale wanaowaabudu badala yake. ila anayeishuhudia haki, nao wanajua.
87. Na ukiwauliza: Ni nani aliyewaumba? Lazima watasema: Ni Mwenyeezi Mungu, basi ni wapi wanakogeuziwa?
88. Na usemi wake (wa kila mara) ni: Ee Mola wangu! kwa hakika hawa ni watu wasioamini.
89. Basi wasamehe na uwaambie (maneno ya) Amani: Hivi karibuni watajua.