Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 49
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Naapa kwa Mlima.
2. Na kwa Kitahu kilichoandikwa.
3. Katika karatasi ya ngozi iliyokunjuliwa.
4. Na kwa nyumba inayozuriwa.
5. Na kwa paa lililonyanyuliwa.
6. Na kwa bahari iliyojazwa.
7. Kwa hakika adhabu ya Mola wako itatokea.
8. Hakuna atakayeizuia.
9. Siku itakapotikisika mbingu kwa mtikisiko.
10. Na majabali yatatoweka kabisa.
11. Basi adhabu siku hiyo kwa wakadhibishao.
12. Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
13. Siku watakayosukumwa kwenye Moto wa Jahannam kwa msukumo wa nguvu.
14. Huu ndio Moto ambao mlikuwa mkiukadhibisha.
15. Basi je, huu ni uchawi au hamuoni?
16. Uingieni, mkingoja au msingoje ni mamoja kwenu, mtalipwa mliyokuwa mkiyatenda.
17. Kwa hakika wamchao (Mwenyeezi Mungu) watakuwa katika Mabustani na neema.
18. Wakifurahia yale aliyowapa Mola wao, na Mola wao amewalinda na adhabu ya Moto uwakao.
19. (Wataambiwa watu wema) kuleni na kunyweni kwa raha kwa sababu ya hayo mliyokuwa mkiyatenda.
20. Wakiegemea juu ya viti vya fahari vilivyopangwa safu, na tutawaoza wanawake weupe wenye macho mazuri.
21. Na wale walioammi na wakafuatwa na vizazi vyao katika imani tukawakutanisha nao watoto wao, wala hatutawapunja kitu katika vitendo vyao, kila mtu atalipwa kwa kile alichokichuma.
22. Na tutawapa matunda na nyama katika vile watakavyopenda.
23. Watapeana humo gilasi (za vinywaji) kisicholeta upuuzi wala dhambi.
24. Na wavulana wao watawazunguka zunguka kama kwamba ni lulu zilizofichwa.
25. Wataelekeana wao kwa wao wakiulizana.
26. Watasema: Hakika zamani tulikuwa pamoja na watu wetu tukiogopa.
27. Lakini Mwenyeezi Mungu ametufanyia ihsani na ametuokoa na adhabu ya upepo wa Moto.
28. Hakika sisi zamani tulikuwa tukimuabudu yeye, hakika yeye ndiye Mwema, Mwenye kurehemu.
29. Basi ukumbushe, na wewe kwa neema za Mola wako si mchawi wala si mwenda wazimu.
30. Au wanasema: Huyu ni mshairi tunamtazamia kupatwa na mauti.
31. Sema: Ngojeni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika wangojeao.
32, Je, akili zao zinawaamuru haya au wao ni watu waovu?
33. Au wanasema: (Qur’an) ameitunga yeye bali wao hawaamini.
34. Basi walete hadithi kama hii ikiwa wanasema kweli.
35. Je, wameumbwa pasipo kitu, au wao ndio waumbaji?
36. Au wameumba mbingu na ardhi? bali hawana yakini.
37. Au wanazo khazina za Mola wako au wao ndio walinzi?
38. Au wanayo ngazi ya kusikilizia? Basi msikiaji wao alete dalili iliyo wazi.
39. Au yeye anao wasichana nanyi mnao wavulana.
40. Au unawaomba malipo, kwa hiyo wanaelemewa na gharama?
41. Au iko kwao (elimu ya) siri nao wanaandika?
42. Au wanaitaka hila? na wale waliokufuru ndio watakaotegwa.
43. Au yuko kwao anayeabudiwa asiye kuwa Mwenyeezi Mungu? Mwenyeezi Mungu ametakasika na hao wanaomshirikisha naye.
44. Na kama wakiona kipande cha mbingu kikianguka husema: Ni mawingu yanayobebana.
45. Basi waache mpaka wakutane na siku yao ambayo wataangamizwa.
46. Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo wala hawatasaidiwa.
47. Na kwa hakika wale waliodhulumu watakuwa na adhabu zaidi ya hiyo, lakini wengi wao hawajui.
48. Na ingoje hukumu ya Mola wako, hakika wewe uko mbele ya macho yetu, na mtukuze kwa kumsifu Mola wako unaposimama.
49. Na katika usiku pia mtukuze, na nyota zinapokuchwa.