Surah Talaq

Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 12

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Ewe Nabii! Mnapowaacha wanawake, basi waacheni katika wakati wa eda zao, na fanyeni hesabu ya (siku) za eda, na mcheni Mwenyeezi Mungu, Mola wenu. Msiwatoe katika nyumba zao wala wasitoke wenyewe, mpaka wafanye jambo la ufasiki ulio wazi. Na hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyeezi Mungu na anayeruka mipaka ya Mwenyeezi Mungu, basi hakika amejidhulumu nafsi yake. Hujui pengine Mwenyeezi Mungu atatokeza jambo jingine baada ya haya.[1]

2. Basi wanapofikia muda wao, ndipo muwaweke kwa wema, au achaneni nao kwa wema, na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu, na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu. Hivyo ndivyo anavyoagizwa yule anayemwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, na anayemuogopa Mwenyeezi Mungu, (Mwenyeezi Mungu) humtengenezea njia ya kuokoka.

3. Na humpa riziki kwa mahala asipopatazamia, na anayemtegemea Mwenyeezi Mungu basi yeye humtoshea, kwa hakika Mwenyeezi Mungu anatimiza kusudi lake, hakika Mwenyeezi Mungu amekwisha kiwekea kila kitu kipimo.

4. Na wale waliokoma hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayo shaka, basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, na (pia ndiyo eda kwa wale) ambao hawajapata hedhi. Na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa, na anayemuogopa Mwenyeezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi.

5. Hiyo ni amri ya Mwenyeezi Mungu aliyoiteremsha kwenu, na anayemuogopa Mwenyeezi Mungu humfutia maovu yake na humpa malipo makubwa.

6. Wawekeni humo humo mnamokaa nyinyi kama mpatavyo, wala msiwadhuru kwa kuwatia katika dhiki, na kama wakiwa na mimba, basi wagharamieni mpaka wajifungue. 

Na kama wakikunyonyesheeni, basi toeni Malipo yao  na shaurianeni kwa wema, na kama mkiona udhia baina yenu, basi amnyonyeshee (mwanamke) mwingine.

7. Mwenye wasaa agharimu kadri ya wasaa wake, na yule ambaye amepungukiwa riziki yake, basi atoe katika kile alichompa Mwenyeezi Mungu, Mwenyeezi Mungu hamkalif’ishi mtu yeyote ila kwa kadri alivyompa, karibuni Mwenyeezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraja.

8. Na miji mingapi iliyovunja amri ya Mola wake na Mitume yake, basi tuliihesabu hesabu ngumu na tukaiadhibu kwa adhabu kali.

9. Basi ikauonja ubaya wa mambo yao, na mwisho wa mambo yao ilikuwa khasara.

10. Mwenyeezi Mungu amewaandalia adhabu kali, basi mcheni Mwenyeezi Mungu enyi wenye akili mlioamini, hakika Mwenyeezi Mungu amekuteremshieni Ukumbusho.

11. Mtume anayekusomeeni Aya za Mwenyeezi Mungu zinazobainisha, ili kuwatoa wale walioamini na wakatenda mema. katika giza kuwapeleka kwenye nuru, na anayemwamini Mwenyeezi Mungu na kutenda mema) atamwingiza katika Pepo zipitazo mito chini yake. watakaa humo milele. Bila shaka Mwenyeezi Mungu amekwishampa riziki nzuri.

12. Mwenyeezi Mungu ni yule ambaye ameziumba mbingu saba na ardhi mfano wa hizo. amri zinashuka baina yao, ili mjue kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu, na kwamba Mwenyeezi Mungu amekizunguka kila kitu kwa elimu.