Surah Takwir

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 29

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu,

1. Jua litakapo kunjwa.

2. Na nyota zitapoanguka.

3. Na milima itakapoendeshwa.

4. Na ngamia wenye mimba watakapoachwa.

5. Na Wanyama wa mwitu watakapokusanywa.

6. Na bahari zitakapowashwa Moto.

7. Na nafsi zitakapounganishwa.

8. Na mtoto mwanamke aliyezikwa hai atakapoulizwa.

9. Kwa kosa gani aliuawa.

10. Na madaftari yatakapoenezwa.

11. Na mbingu zitakapoondolewa.

12. Na Moto utakapo kokwa.

13. Na Pepo itakaposogezwa.

14. (Wakati huo) Nafsi itajua ilicho kihudhurisha.

15. Basi naapa kwa nyota zinazorejea nyuma.

16. Zinazokwenda (na) kujificha.

17. Na kwa usiku unapoingia.

18. Na kwa asubuhi inapopambazuka.

19. Kwa hakika hii ni kauli ya Mtume Mtukufu.

20. Mwenye nguvu, mwenye cheo cha heshima kwa Mwenyeezi Mungu.

21. Anayetiiwa kisha mwaminifu.

22. Na Mwenzenu hana wazimu.

23. Na hakika yeye alimuona (Jibril) katika upeo wa macho ulio safi.

24. Wala yeye si bakhili kueleza mambo ya siri.

25. Wala hii si kauli ya shetani aliyefukuzwa.

26. Basi mnakwenda wapi?

27. Hiyo siyo ila ni ukumbusho kwa walimwengu.

28. Kwa yule miongoni mwenu anayetaka kushika njia.

29. Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Mwenyeezi Mungu Mola wa walimwengu.