Surah Tahrim

Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 12

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Ewe Nabii! mbona unaharamisha alichokuhalalishia Mwenyeezi Mungu? unatafuta radhi ya wake zako, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

2. Hakika Mwenyeezi Mungu amekupeni Sharia ya kufungua viapo vyenu, na Mwenyeezi Mungu ni Mola wenu, naye ndiye Mjuzi, Mwenye hekima.

3. Na Nabii alipomwambia mmoja wa wake zake jambo la siri, basi (yule mke) alipolitangaza, na Mwenyeezi Mungu akamdhihirishia (Nabii) akajulisha sehemu yake na akaacha sehemu nyingine, basi alipompasha (mkewe) khabari hii, akasema: Nani amekupa khabari hii? (Nabii) akasema: Amenipa khabari aliye Mjuzi Mwenye khabari.

4. Kama nyinyi wawili mtatubu kwa Mwenyeezi Mungu basi nyoyo zenu zimekwisha elekea upande, na kama mtasaidiana dhidi yake (Mtume) basi Mwenyeezi Mungu ni Mlinzi wake, na Jibril, na Waumini wema, na zaidi ya hayo (pia) Malaika ni wasaidizi (wake).

5. (Mtume) akikupeni talaka, bila shaka Mola wake atampa badala yenu wake wengine walio bora kuliko nyinyi, waliosilimu, wenye kuamini, watii, wenye kutubia, wenye kufanya ibada, wafungao saumu, wajane na wasichana.

6. Enyi mlioamini! jiokoeni nafsi zenu na watu wenu katika Moto ambao kuni zake ni watu wa mawe, wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyeezi Mungu aliyowaamuru, na hutenda wanayoamrishwa.

7. Enyi mliokufuru! msitoe udhuru leo, bila shaka mtapewa malipo ya yale mliyokuwa mkitenda.

8. Enyi mlioamini! tubuni kwa Mwenyeezi Mungu toba iliyo ya kweli, huenda Mola wenu akakufutieni maovu yenu na kukuingizeni katika Pepo zipitazo mito chini yake, siku ambayo Mwenyeezi Mungu hatamfedhehesha Mtume na wale walioammi pamoja naye, nuru yao itakwenda mbele yao na pande zao za kulia (na kushoto) (na huku) wanasema: Mola wetu! Tutimizie nuru yetu na tusamehe, hakika wewe ni mwenye uwezo juu ya kila kitu.

9. Ewe Nabii! pigana na makafiri na wanafiki na uwe mgumu kwao, na makao yao ni Jahannam nayo ni marejeo mabaya.

10. Mwenyeezi Mungu amepiga mifano wa waliokufuru, kwa mke wa Nuhu na mke wa Luti hawa wawili walikuwa chini ya waja wema wawili miongoni mwa waja wetu, basi (wanawake hao) wakawafanyia khiyana, (lakini waume zao) hawakuwasaidia chochote mbele ya Mwenyeezi Mungu, na ikasemwa ingieni Motoni pamoja na waingiao.

11. Na Mwenyeezi Mungu anapiga mfano wa Walioamini kwa mkewe wa Firaun aliposema: Ee Mola wangu! nijengee nyumba Peponi karibu yako, na uniokoe na Firaun na matendo yake, na uniokoe katika watu madhalimu.

12. Na Mariam binti Imrani aliyejilinda uchi wake, na tukampulizia humo roho yetu na akayasadikisha maneno ya Mola wake, na Vitabu vyake, na alikuwa miongoni mwa wanyenyekevu.