Surah Taghabun

Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 18

Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Vinamtukuza Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, ufalme ni wake, na sifa njema ni zake, na yeye ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.

2. Yeye ndiye aliyekuumbeni. na wengine wenu ni makafiri na wengine wenu ni Waumini, na Mwenyeezi Mungu anaona mnayoyafanya.

3. Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, na akafanya sura zenu, kisha sura zenu akazifanya vizuri, na marejeo ni kwake.

4. (Mwenyeezi Mungu) anajua vilivyomo mbinguni na ardhini, na anajua mnayoyaficha na mnayoyatangaza, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

5. Je. haikukufikieni khabari ya wale waliokufuru zamani na wakaonja ubaya wa mambo yao na wao wana adhabu yenye kuumiza.

6. Hayo ni kwa sababu Mitume wao walikuwa wakiwafikia kwa hoja wazi wazi lakini wakasema: Je, watu (wenzetu) watatuongoza? kwa hiyo wakakataa na wakageuka upande, na Mwenyeezi Mungu si mhitaji, bali Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Mwenye kusifiwa.

7. Waliokufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa sema: Naam, kwa hakika ya Mola wangu nyinyi lazima mtafufuliwa, kisha lazima mtajulishwa mliyoyatenda na hayo ni rahisi kwa Mwenyeezi Mungu.

8. Basi mwaminini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na nuru ambayo tumeiteremsha, na Mwenyeezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.

9. (Kumbukeni) siku atakayowakusanya nyinyi kwa ajili ya siku ya Mkusanyiko, hiyo ni siku ya khasara. Na anayemwamini Mwenyeezi Mungu na akafanya mema atamfutia maovu yake na atamwingiza bustanini zipitazo mito chini yake, watakaa humo milele, huko ndiko kufaulu kukubwa.

10. Na wale waliokufuru na wakakadhibisha Aya zetu, hao ndio watu wa Motoni watakaa humo milele, nayo ni marejeo mabaya.

11. Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Mwenveezi Mungu, na anayemwamini Mwenyeezi Mungu huuongoza moyo wake, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

12. Na mtiini Mwenyeezi Mungu na mtiini Mtume, lakini mkikataa, basi ni juu ya Mtume wetu kufikisha wazi wazi tu.

13. Mwenyeezi Mungu, hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, na Waumini wamtegemee Mwenyeezi Mungu tu.

14. Enyi mlioamini kwa hakika baadhi ya wake zenu na watoto wenu ni maadui zenu, basi jihadharini nao, na kama mkisamehe na kuvumilia na kuyafuta, basi hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

15. Bila shaka mali zenu na watoto wenu ni jaribio, na kwa Mwenveezi. Mungu kuna malipo makubwa.

16. Kwa hiyo mcheni Mwenyeezi Mungu muwezavyo, na sikilizeni na tiini na toeni, itakuwa kheri kwa nafsi zenu, na aepushwaye na ubakhili wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.

17. Mkimkatia Mwenyeezi Mungu sehemu nzuri atakuzidishieni na atakusameheni, na Mwenyeezi Mungu ndiye atoaye thawabu nyingi, Mpole.

18. Ajuaye siri na dhahiri, Mwenve nguvu, mwenye hekima.