Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 17
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Naapa kwa mbingu na chenye kuja usiku.
2. Na nini kitakujulisha ni nini chenye kuja usiku?
3. Ni nyota inayong’aa.
4. Hakuna nafsi yoyote isiyokuwa na mchungaji juu yake.
5. Basi mtu ajitazame ameumbwa kwa kitu gani.
6. Ameumbwa kwa maji yanayotoka kwa nguvu.
7. Yatokayo kati kati ya mifupa ya mgongo na kifua.
8. Kwa hakika yeye ana uwezo wa kumrudisha.
9. Siku zitakapodhihirishwa siri.
10. Basi hatakuwa na nguvu wala msaidizi.
11. Naapa kwa mbingu yenye mvua.
12. Na kwa ardhi yenye mipasuko.
13. Hakika hii (Qur’an)ni kauli ya haki.
14. Wala si upuuzi.
15. Hakika wao wanafanya hila.
16. Nami pia nafanya hila.
17. Basi wape muda makafiri, wape muda kidogo.