Sura hii imeteremshwa Makka na ina Aya 88
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Swaad. Naapa kwa Our’an yenye mawaidha.
2. Lakini wale waliokufuru wamo katika majivuno na upinzani.
3. Tumeviangamiza vizazi vingapi kabla yao, wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka umekwisha pita.
4. Na walishangaa kwa kuwafikia muonyaji anayetokana na wao, wakasema makafiri: Huyu ni mchawi muongo.
5. Je, amewafanya miungu (wote) kuwa Mungu Mmoja! kwa kweli hili hakika ni jambo la ajabu.
6. Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nendeni mkadumu na miungu wenu, hakika hili ndilo jambo linalotakiwa.
7. Sisi hatukusikia haya katika mila iliyopita, siyo haya ila ni uzushi.
8. Je, yeye ameteremshiwa mawaidha kati yetu? lakini wao wanayo shaka juu ya mawaidha yangu, bali hawajaionja adhabu yangu.
9. Je, wanazo khazina na rehema za Mola wako aliye Mwenye nguvu. Mpaji.
10. Au wanao ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake? Basi na wazipande njia zote.
11. Ni askari watakaoshindwa miongoni mwa makundi yatakayoshindwa.
12. Walikadhibisha kabla yao watu wa Nuhu na kina Adi na Firaun mwenye majeshi.
13. Na Thamudi na watu wa Luti na watu wa Porini (watu wa Shua’ybu) hayo ndiyo makundi.
14. Hao wote waliwakadhibisha Mitume, basi adhabu yangu ikathibiti.
15. Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja usio na taakhira.
16. Na husema: Mola wetu! tuhimize sehemu yetu kabla ya siku ya Hesabu.
17. Subiri juu ya hayo wanayoyasema, na umkumbuke mja wetu Daudi, mwenye nguvu, kwa hakika yeye alikuwa mwelekevu sana.
18. Hakika sisi tuliitiisha milima pamoja naye, ikitukuza jioni na asubuhi.
19. Na (pia) ndege waliokusanywa, wote walikuwa wanyenyekevu kwake.
20. Na tukautia nguvu ufalme wake na tukampa hekima na (akili ya) kukata hukumu.
21. Na je, imekufikia khabari ya wagombanao walipopindukia (ukutani kuingia) chumbani?
22. Walipomwingilia Daudi na akawaogopa, wakasema: Usiogope (sisi ni) wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenzie basi tuhukumu baina yetu kwa haki wala usipendelee, na utuongoze kwenye njia iliyo sawa.
23. Hakika huyu ni ndugu yangu, anao kondoo majike tisini na tisa, nami nina kondoo mmoja tu, lakini anasema: Nipe huyo, na amenishinda katika maneno.
24. Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kukuomba kondoo wako kuongeza katika kondoo zake, na bila shaka washirika wengi hurukiana wao kwa wao, isipokuwa wale walioamini na kutenda mema, nao hao ni wachache, Na Daudi akaona kuwa tumemjaribu, akaomba msamaha kwa Mola wake na akaanguka kunyenyekea na akaelekea.
25. Na tukamsamehe hayo, na kwa hakika alikuwa mbele yetu mwenye cheo cha kukaribiana na mahala pazuri.
26. Ewe Daudi! hakika tumekujaalia kuwa khalifa ardhini, basi uwahukumu watu kwa haki wala usifuate matamanio yakakupoteza katika njia ya Mwenyeezi Mungu wao watapata adhabu kali kwa sababu waliisahau siku ya Hesabu.
27. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake bure, hiyo ndio dhana ya wale waliokufuru, basi ni msiba wa Moto kwa wale waliokufuru.
28. Je, tuwajaalie wale walioamini na kutenda mema kuwa sawa na wafanyao uharibifu ardhini? Au tuwajaalie wacha Mungu kuwa sawa na waovu?
29. (Hiki) Kitabu tumekiteremsha kwako chenye baraka ili wapate kuzifikiri Aya zake, na wenye akili wawaidhike.
30. Na tukampa Daudi (mtoto) Suleiman, aliyekuwa mtu mwema, bila shaka alikuwa mnyenyekevu mno.
31. (Kumbukeni) alipopelekewa jioni farasi walio kimya wasimamapo, wepesi wakimbiapo.
32. Basi akasema: Navipenda vitu vizuri kwa kumkumbuka Mola wangu, kisha wakafichikana nyuma ya pazia.
33. Warudisheni kwangu, na akaanza kuwapangusa miguu (yao) na shingo (zao).
34. Na hakika tulimjaribu Suleiman na tukauweka mwili juu ya kiti chake, kisha akarejea.
35. Akasema: Molawangu! nisamehe na unipe ufalme, asiupate yeyote baada yangu, bila shaka wewe ndiye Mpaji.
36. Basi tukamtiishia upepo ukaenda pole pole kwa amri yake anakotaka kufika.
37. Na mashetani (pia tukamtiishia) kila ajengaye na azamiaye.
38. Na wengine wafungwao minyororoni.
39. Hiki ndicho kipawa chetu bila ya hesabu, basi fanya ihsani au zuia.
40. Na kwa hakika alikuwa mbele yetu mwenye cheo cha kukaribiana na mahala pazuri.
41. Na mkumbuke mja wetu Ayubu, alipo mwita Mola wake: Kwa hakika shetani amenifikishia udhia na taabu.
42. Kaza mwendo, hapa mahala baridi pakuogea na kinywaji.
43. Na tukampa watu wake na wengine kama wao pamoja nao, kwa rehema itokayo kwetu na mawaidha kwa watu wenye akili.
44. Na shika kicha cha vijiti mkononi mwako, kisha mpige nacho (mkeo) wala usivunje kiapo bila shaka tulimkuta ni mwenye subira, mja mwema, kwa hakika alikuwa mnyenyekevu sana.
45. Na wakumbuke waja wetu, Ibrahimu na Isihaka na Yaakub waliokuwa wenye nguvu na busara.
46. Hakika sisi tuliwachagua kwa lile jambo zuri la kuikumbuka Akhera.
47. Nao bila shaka walikuwa mbele yetu miongoni mwa watu bora waliochaguliwa.
48. Na mkumbuke Ismaili na Ilyasa na Dhulkifli, na hao wote walikuwa miongoni mwa watu bora.
49. Huu ni ukumbusho! na kwa hakika wamchao Mwenyeezi Mungu mahala pao pa kurudia patakuwa pazuri.
50. Bustani za kukaa milele zilizofunguliwa milango kwa ajili yao.
51. Humo wataomba matunda mengi na kinywaji.
52. Na pamoja nao (watakuwapo) Huurul a’yn (wanawake wa Peponi) watulizao macho.
53. Haya ndiyo mliyoahidiwa kwa siku ya Hesabu.
54. Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyomalizika.
55. Hivi ndivyo na kwa hakika wale warukao mipaka, pa kurudia pao patakuwa pabaya.
56. Jahannam, wataiingia, nacho ni kitanda kibaya.
57. Hivi ndivyo, basi waonje maji ya moto na usaha.
58. Na (adhabu) nyingine za namna hii nyingi.
59. Hili ndilo jeshi litakaloingia pamoja nanyi, hawatapata makaribisho, hakika wao wataingia Motoni.
60. Watasema: Lakini nynyi nanyi hamna makaribisho! Nyinyi ndio mliotutangulizia hii, tena kao baya.
61. Watasema: Mola wetu! aliyetutangulizia haya basi mzidishie adhabu mara mbili Motoni.
62. Nawaseme: Imekuwaje, hatuwaoni watu tuliokuwa tukiwahesabu katika waovu.
63. Je, tuliwafanyia mzaha au macho yamewakosa?
64. Bila shaka hayo, kukhasimiana watu wa Motoni ni kweli.
65. Sema: Hakika mimi ni Muonyaji tu, na hakuna aabudiwaye isipokuwa Mwenyeezi Mungu tu, Mmoja Mwenye nguvu.
66. Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake, Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.
67. Sema: Hii ni khabari kubwa.
68. Mnajiepusha nayo.
69. Sikuwa na elimu ya mkutano wa wakuu waliotukuka walipokuwa wakishindana.
70. Haifunuliwi kwangu isipokuwa kwamba mimi ni muonyaji tu aliye dhahiri.
71. (Kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika mimi nitaumba mtu katika udongo.
72. Na nitakapomkamilisha na kumpulizia roho yangu, basi mwangukieni kwa kutii.[1]
73. Basi Malaika wakatii wote pamoja.
74. Isipokuwa Iblis alijivuna na akawa katika makafiri.
75. Akasema: Ewe Iblis, ni nini kimekuzuia kumtii yule niliyemuumba kwa mikono yangu? Je, umetakabari au umekuwa miongoni mwa wakubwa?
76. Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.
77. Akasema: Basi toka humo, hakika wewe ndiye mwenye kufukuzwa.
78. Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka siku ya Malipo.
79. Akasema: Mola wangu! nipe nafasi mpaka siku watakayofufuliwa.
80. Akasema: Haya, hakika umekuwa miongoni mwa waliopewa nafasi.
81. Mpaka wakati wa siku maalumu.
82. Akasema: kwa haki ya utukufu wako, bila shaka nitawapoteza wote.
83. Isipokuwa waja wako miongoni mwao waliosafishwa.
84. Akasema: Ni haki, na ndiyo haki nisemayo.
85.Lazima nitaijaza Jahannam wewe na kwa wale wote wenye kukufuata miongoni mwao.
86. Sema: Sikuombeni malipo juu ya hayo wala mimi si katika wale wanaojilazimisha.
87. Huu siyo ila ni ukumbusho kwa walimwengu.
88. Na lazima mtajua khabari zake baadaye kidogo.