Surah Saff

Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 14

Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Vinamtukuza Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

2. Enyi mlioamini! mbona mnasema msiyoyatenda?

3. Ni kosa kubwa mbele ya Mwenyeezi Mungu kusema msiyoyatenda.

4. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu anawapenda wale wanaopigana katika njia yake kwa safu kama kwamba wao ni jengo lililokamatana.

5. Na Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! mbona mnaniudhi hali mnajua kuwa mimi ni Mtume wa Mwenyeezi Mungu kwenu? Lakini walipokataa (kumtii) Mwenyeezi Mungu akazidisha nyoyo zao (kukataa kama watakavyo) na Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu waovu.

6. Na (wakumbushe) aliposema Issa bin Mariam: Enyi wana wa Israeli! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyeezi Mungu kwenu, ninaethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kutoa khabari njema ya Mtume atakaekuja baada yangu, jina lake ni Ahmad, lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhahiri.

7. Na ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule anayemzulia Mwenyeezi Mungu uongo na hali anaitwa kwenye Uislaamu? Na Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

8. Wanataka kuzima nuru ya Mwenyeezi Mungu kwa vinywa vyao, na Mwenyeezi Mungu atakamilisha nuru yake ingawa makafiri watachukia.

9. Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa muongozo na kwa dini ya haki ili ishinde dini zote ingawa washirikina watachukia.

10. Enyi mlioamini! Je, niwajulisheni biashara itakayo waokoweni katika adhabu iumizayo.

11. Mwaminini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na piganieni dini ya Mwenyeezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu hayo ni bora kwenu ikiwa mnajua.

12. Atakusameheni dhambi zenu na atakuingizeni katika Mabustani yapitayo mito chini yake na makao mazuri katika Bustani za milele. huko ndiko kufaulu kukubwa.

13. Na kingine mnachokipenda, (nayo) ni nusura, itokayo kwa Mwenveezi Mungu na ushindi ulio karibu, na wapashe khabari njema wenye kuamini.

14. Envi mlioamini! kuweni wasaidizi wa Mwenyeezi Mungu kama alivyosema Issa bin Mariam kuwaambia wafuasi (wake): Ni nani wasaidizi wangu kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu? wafuasi wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyeezi Mungu, basi taifa moja la wana wa Israeli walioamini, na taifa jingine wakakufuru, ndipo tukawasaidia wale walioamini juu ya maadui zao na wakawa wenye kushinda.