Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 54
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwngi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, na katika Akhera sifa njema ni zake, naye ni Mwenye hekima Mwenye khabari.
2. Anajua yaingiayo ardhini na yatokayo humo na yateremkayo humo, naye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
3. Na walisema waliokufuru; Hakitatufikia Kiyama. Sema; Naam, kwa haki ya Mola wangu, bila shaka kitakufikieni, (Mola) ajuaye mambo ya siri, hakifichikani kwake (chochote) kilicho na uzito wa chembe katika mbingu wala katika ardhi, wala kidogo kuliko hiki wala kikubwa zaidi ila vimo katika Kitabu chenye kubainisha.
4. Ili awalipe wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, hao watalipwa msamaha na riziki yenye heshima.
5. Na wale waliojitahidi kuzipinga Aya zetu wakaona watashinda hao watapata adhabu mbaya yenye kuumiza.
6.Na waliopewa elimu wanafahamu ya kuwa yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako ndiyo haki, nayo huongoza kwenye njia ya Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa.
7. Na waliokufuru husema: Je, tukujulisheni mtu anayekuambieni kuwa mtakapochambuliwa vipande vipande hakika nyinyi mtakuwa katika umbo jipya?
8. Je, amezua uongo juu ya Mwenyeezi Mungu au amepata wazimu? Bali wasioamini Akhera watakuwa katika adhabu na upotovu wa mbali.
9. Je, hawaoni yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao ya mbingu na ardhi? kama tungependa tungewadidimiza ardhini, na tungeangusha juu yao kipande cha mbingu. Bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa kila mja mwenye kuelekea.
10. Na kwa hakika tulimpa Daudi fadhila kutoka kwetu, enyi milima nyenyekeeni pamoja naye, na ndege (pia) na tukamlainishia chuma.
11. (Tukamwambia) Kuwa: Tengeneza (nguo za chuma) pana, na upime katika kuunganisha, na fanyeni vitendo vizuri bila shaka ninayaona mnayoyatenda.
12. Na kwa Suleiman (tukautiisha) upepo (uliokwenda) safari yake ya asubuhi (mwendo wa) mwezi mmoja na safari yake ya jioni mwendo wa) mwezi mmoja na tukamtiririshia chemchem ya shaba. Na katika majinni (kulikuwa na) waliofanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake, na anayejitenga na amri yetu miongoni mwao tutamuonjesha adhabu ya Moto uwakao.
13. Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama ngome na masanamu na sinia kubwa kama hodhi, na masufuria makubwa sana yasiyoondolewa mahala pake. Fanyeni (vitendo vizuri) enyi watu wa Daudi kwa kushukuru, na ni wachache wanaoshukuru katika waja wangu.
14. Na tulipomfisha, hakuna aliyewajulisha kifo chake, ila mnyama wa ardhi alikula fimbo yake. Basi ilipoanguka, majinni wakatambua kama wangelijua siri wasingelikaa katika adhabu yenye kufedhehesha.
15. Bila shaka ulikuwa ni Muujiza kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika makazi yao. Bustani mbili kulia na kushoto, kuleni katika riziki ya Mola wenu, na mumshukuru, mji mzuri, na Mola Mwingi wa kusamehe.
16. Lakini wakajitenga, kwa hiyo tukawapelekea furiko kubwa na tuka wabadilishia bustani zao kwa bustani nyingine mbili zenye matunda makali na mivinje na miti kidogo ya kunazi.
17. Hayo tuliwapa kwa sababu walikufuru, nasi hatumwadhibu ila anayekufuru.
18. Na baina yao na baina ya miji tuliyo ibariki, tukaweka miji iliyo dhahiri na tukapima humo (vituo vya) safari, nendeni usiku na mchana kwa amani.
19. Lakini wakasema; Mola wetu! uweke mwendo mrefu kati ya safari zetu na wakajidhulumu nafsi zao. Ndipo tukawafanya hadithi na tukawararua vipande vipande kwa hakika katika hayo mna mazingatio kwa kila afanyaye subira sana, mwenye kushukuru.
20. Na bila shaka Iblis, alisadikisha dhana yake juu yao, nao wakamfuata isipokuwa kundi la Waumini.
21. Na yeye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila kwa sababu tudhihirishe ni nani Mwenye kuamini Akhera na nani anaye itilia shaka, na Mola wako ni Mwenye kuhifadhi kila kitu.
22. Sema: Waiteni mnaowadaia uungu kinyume cha Mwenyeezi Mungu wao hawamiliki uzito wa chembe mbinguni wala ardhini, wala hawana ushirika katika hizo, wala yeye hana msaidizi miongoni mwao.
23. Wala hautafaa uombezi mbele yake ila kwa yule aliyempa idhini, Hata inapoondolewa khofu nyoyoni mwao wanasema: Mola wenu amesema nini, wanasema: Haki, naye ndiye aliye Juu Mkubwa.
24. Sema: Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? sema: Mwenyeezi Mungu na bila shaka sisi au nyinyi tuko juu ya uongofu au katika upotovu ulio wazi.
25. Sema: Hamtaulizwa kwa makosa tuliyofanya wala hatutaulizwa kwa yale mnayoyatenda.
26. Sema: Mola wetu atatukusanya baina yetu kisha atatuhukumu baina yetu kwa haki, naye ndiye Hakimu, Mjuzi.
27. Sema: Nionyesheni wale mliowaunganisha naye kuwa washirika, hapana! Lakini yeye Mwenyeezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
28. Na hatukukutuma ila kwa watu wote uwe Mtoaji wa khabari nzuri na Muonyaji, lakini watu wengi hawajui.
29. Na wanasema; Lini (itafika) ahadi hii ikiwa mnasema kweli?
30. Sema: Mmepewa miadi ya siku ambayo hamtaakhirisha saa wala hamtaitangulia.
31. Na wakasema wale waliokufuru: Hatutaiamini Qur’an hii, wala yale yaliyokuwa kabla yake, na ungewaona madhalimu watakaposimamishwa mbele ya Mola wao, wakirudishiana maneno wao kwa wao, wale wanyonge watawaambia wale waliojiona wakubwa: Kama si nyinyi bila shaka tungelikuwa wenye kuamini.
32. Watasema wale waliojiona wakubwa kuwaambia wale wanyonge: Je, sisi tulikuzuilieni uongofu baada ya kukufikieni? (siyo!) bali nyinyi wenyewe mlikuwa waovu.
33. Na wale wanyonge watasema kuwaambia wale waliojiona wakubwa: Bali (mlikuwa mkifanya) hila usiku na mchana mlipotuamuru tumkufuru Mwenyeezi Mungu na tumfanyie washirika. Nao wataficha majuto watakapoiona adhabu, na tutaweka minyororo shingoni mwa wale waliokufuru, hawatalipwa ila yale waliyokuwa wakiyatenda.
34. Nasi hatukumtuma muonyaji katika mji wowote ila wenyeji wake wenye neema husema: Bila shaka sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo.
35. Na wakasema: Sisi tunazo mali nyingi na watoto wengi, wala sisi hatutaadhibiwa.
36. Sema; Kwa hakika Mola wangu humfungulia riziki amtakaye na humdhikisha, lakini watu wengi hawajui.
37. Na si mali zenu wala watoto wenu watakaokukaribisheni kwetu katika daraja, isipokuwa aliyeamini na kutenda mema. Basi hao watapata malipo mara mbili kwa yale waliyotenda, nao watakuwa salama katika maghorofa.
38. Na wale wanaojitahidi kuzipinga Aya zetu, wakaona watashinda hao watahudhurishwa adhabuni.
39. Sema: Kwa hakika Mola wangu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humdhikisha. Na chochote mtakachotoa, basi yeye atakilipa, naye ni mbora wa wanaoruzuku.
40. Na siku atakayowakusanya wote, kisha atawaambia Malaika: Je, hawa walikuwa wakikuabuduni?
41. Watasema: Umeepukana na kila upungufu! Wewe ndiye Mlinzi wetu, si hao, bali walikuwa wakiwaabudu majinni, wengi wao waliwaamini hao.
42. Na hii leo hawataweza baadhi yenu kuwafaidia wengine wala kuwadhuru, na tutawaambia wale waliodhulumu: Onjeni adhabu ya Moto mliokuwa mkiukadhibisha.
43. Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi, husema: Huyu siye ila ni mtu anayetaka kukuzuieni katika yale waliyokuwa wakiabudu baba zetu. Wakasema: Siyo haya ila ni uongo uliozuliwa, Na wakasema wale walioikataa haki ilipowafikia: Siyo haya ila ni uchawi ulio dhahiri.
44. Wala hatukuwapa vitabu wanavyovisoma, wala hatukuwapelekea Muonyaji kabla yako.
45. Na walikadhibisha wale waliokuwa kabla yao, na hawajapata sehemu ya kumi ya tulivyowapa hao, lakini waliwakadhibisha Mitume wangu, basi adhabu yangu ilikuwa namna gani?
46. Sema: Mimi nakunasihini tu kwa jambo kuwa: Msimame kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu, wawili wawili na mmoja mmoja, kisha mfikiri, Mwenzenu hana wazimu, yeye siye ila ni Muonyaji kwenu kabla ya kufika adhabu kali.
47. Sema: Malipo niliyokuombeni, basi hayo ni kwa ajili yenu, malipo yangu yako kwa Mwenyeezi Mungu tu, naye ni Shahidi juu ya kila kitu.
48. Sema: Bila shaka Mola wangu hutoa haki, Mjuzi wa ghaibu.
49. Sema: Ukweli umefika, na uongo hautatokea wala hautarudi.
50. Sema: Ikiwa nimepotea, basi nimepotea kwa kuidhuru nafsi yangu tu, na ikiwa nimeongoka, basi ni kwa sababu ananiletea Wahyi Mola wangu bila shaka yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu.
51. Na ungeliona watakapohangaika lakini hakuna kimbilio, na wataka matiwa mahala pa karibu.
52. Na watasema: Tumemwamini, lakini wanawezaje kushika (imani) katika mahala pa mbali?
53. Nao wamekwisha mkataa zamani na wanakisia yasiyoonekana kutoka mahala pa mbali.
54. Na watatiliwa kizuizi kati yao na kati ya yale wanayoyatamani, kama walivyofanyiwa wenzao zamani, hakika wao walikuwa katika shaka yenye kuhangaisha.