Surah Rum

sura hii mieteremshwa Makka, na ina  Aya 60

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Alif Lam Mym

2. Warumi wameshindwa.

3. Katika nchi iliyo karibu, nao baada ya kushindwa kwao, watashinda.

4. Katika miaka michache, amri ni ya Mwenyeezi Mungu kabla na baadaye, na siku hiyo Waumini watafurahi.

5. Kwa msaada wa Mwenyeezi Mungu humsaidia amtakaye, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

6. (Hii ni) ahadi ya Mwenyeezi Mungu, Mwenyeezi Mungu havunji ahadi yake, lakini watu wengi hawajui.

7. Wanajua hali ya dhahiri ya maisha ya dunia, nao ndio wameghafilika na Akhera.

8. Je, hawafikirii katika nafsi zao (wakaona kuwa) Mwenyeezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake ila kwa haki, na kwa muda uliowekwa? Na kwa hakika watu wengi wanakataa kukutana na Mola wao.

9. Je, hawatembei katika nchi na kuona jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko hawa, na wakiilima ardhi na kuistawisha zaidi kuliko hawa walivyoistawisha, na Mitume wao waliwafikia kwa Miujiza wazi wazi, basi hakuwa Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu.

10. Kisha ulikuwa mwisho wa wale waliofanya ubaya kwa kuzikadhibisha Aya za Mwenyeezi Mungu, na walikuwa wakizifanyia mzaha.

11. Mwenyeezi Mungu huanzisha kiumbe tena hukirudisha (mara ya pili) kisha mtarudishwa kwake.

12. Na siku kitakaposimama Kiyama waovu watakata tamaa.

13. (Wala) hawatakuwa na waombezi miongoni mwa waliokuwa wakiwashirikisha, nao watawakataa washirika wao.

14. Na siku kitakapotokea Kiyama, siku hiyo watafarikiana.

15. Lakini wale walioamini na kutenda mema, basi wao watafurahishwa katika Bustani.

16. Na wale waliokufuru na wakazikadhibisha Aya zetu na mkutano wa Akhera basi hao watahudhurishwa katika adhabu.

17. Basi mtukuzeni Mwenyeezi Mungu mnapoingia usiku na mnapoingia asubuhi.

18. Na sifa zote njema ni zake mbinguni na ardhini, na wakati wa alasiri na mnapoingia adhuhuri.

19. Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, na hukitoa kilicho kufa kutokana na kilicho hai na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake na hivyo ndivyo mtakavyotolewa.

20. Na katika dalili zake ni huku kukuumbeni kwa udongo. kisha mmekuwa watu mnaoenea.

21. Na katika dalili zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao, naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaofikiri.

22. Na katika dalili zake ni kuumba mbingu na ardhi na kutafautiana, lugha zenu na rangi zenu, kwa hakika katika hayo mna mazingatio kwa wenye elimu.

Aya 22

 UBAYA WA MAKUNDI NA KUFARAKANA

Kufarakana baina ya watu kuna aina mbili:

a) Kufarakana kunako kubalika.

b) Kufarakana kusiko kubalika.

Farka nzuri zinazokubalika ni kule kutafautiana kati ya wanadamu katika viwili wili vyao, rangi zao, lugha zao, desturi zao, akili zao na matakwa yao.

Kwani hali kama hiyo inadhihirisha neema kubwa ya Mwenyeezi Mungu (s.w) kwa viumbe wake. Anasema Mwenyeezi Mungu: “Na katika dalili zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana lugha zenu na rangi zenu, kwa hakika katika hayo mna mazingatio kwa wenye elimu.” 30:22.

Lakini, zile farka mbaya zisizokubalika ni zile za kufarakana katika dini. Anasema Mwenyeezi Mungu: “Amekupeni Sharia (njia nyoofu) ya dini, aliyomuusia Nuhu na tuliyokufunulia wewe (Muhammad) na tuliyowausia Ibrahimu na Musa na Issa, kwamba: Simamisheni dini wala msifarakane kwayo, ni ngumu kwa washirikina (dini hii) unayowaitia, Mwenyeezi Mungu humchagua kwake amtakaye na humuongoza kwake aelekeaye.” 42:13.

Na, makusudio ya kufarakana katika dini hapa ni kutofautiana katika misingi ya Itikadi, na wala si katika Furu’u ddiin.

KUFARAKANA UMMA MAKUNDI SABINI NA TATU

Anasema Mtume s.a.w kuwa: “Walifarakana Mayahudi na Wakristo makundi sabini na moja au sabini na mbili, na watafarakana umma wangu makundi sabini na tatu, yote (yatatupwa) Motoni isipokuwa (kundi) moja tu. Wakauliza:

Ni kundi gani hilo ewe Mtume wa Mwenyeezi Mungu? Akajibu: Ambao watakuwa mfano wa hivi nilivyo leo mimi na maswahaba wangu.”

Taz: Sahih Ibn Maajah     J.4  Uk. 352

 As-Sunanul Kubra          J.10 Uk. 208

 As-Sunanu Walmubtadiatu     Uk. 3

Kwa kuwa Hadithi iliyotajwa hapo juu ni Mutlaq, tunaleta sasa Hadith Muqayyad:

Anasema Mtume s.a.w kuwa: “Watafarakana umma wangu makundi sabini na tatu, makundi sabini na mbili (yatatupwa) Motoni, na (kundi) moja litaingizwa Peponi, nalo ndilo ambalo litamfuata Wasii wangu. Anasema (Ali a.s):

Kisha akapiga bega langu kwa mkono wake.”

Taz; Ithbaatul Hudaat      J.2  Uk. 186

SABABU ZA KUZUKA FARKA HIZI

Kuna sababu nyingi zilizozua farka, Lakini hapa tunazitaja tano tu:

a) Msiba mkubwa siku ya Alhamisi.

b) Kuwepo wanafiki.

c) Viongozi waovu.

d) Uasi.

e) Hadithi za Uongo.

A) MSIBA MKUBWA SIKU YA ALHAMISI

Amesema Mtume (s.a.w) kuwa:

“Nileteeni karatasi niwaandikieni maandiko hamtapotea baada yake. Umar bin Khattab, akasema: kwa hakika Mtume yamemzidi maradhi, inatutosha Qur’an. Mara wakakhitilafiana na zogo likazidi, Mtume s.a.w akasema: Niondokeeni.”

Iliposemwa: “Nileteeni karatasi’ Hii ni amri ya “Wujuub” na, kwa kufahamu hilo lazima kuzingatia mambo manne yafuatayo:

a) Mtume s.a.w aliposema: “Hamtapotea” Inakupa kufahamu kuwa: Yale maandiko ni Kinga kwa Umma usiingie katika upotovu. Na kuzuia upotovu ni jambo la lazima, kwa hiyo, kupatikana maandiko ni lazima kwao, basi kufuata amri ya Mtume (ya kuletwa karatasi) ni wajibu.

b) Mtume s.a.w kuchukia kitendo chao, na kuwaamrisha waondoke mbele yake, ni dalili kamili kuwa wao walifanya jambo baya sana.

c) Mtume s.a.w kuamrisha iletwe karatasi ili awaandikie maandiko ambayo hawatapotea baada yake, hali akiwa mgonjwa mahtuti, hii ni Ishara kubwa inayoonyesha umuhimu wa agizo alilokuwa nalo kwa umma huu.

d) Katika tukio hili, Abdullah bin Abbas (a.s) alikuwa akilia mara kwa mara akisema: Msiba mkubwa siku ya Alhamisi. Ni dalili ya wazi kuwa, kumpinga Mtume kuandika maandiko, ni kosa kubwa.

B) KUWEPO WANAFIKI

Anasema Mwenyeezi Mungu: “Na katika mabedui wanaokaa pembezoni mwenu kuna wanafiki, na katika wenyeji wa Madina (pia) wamebobea katika unafiki, huwajui, sisi tunawajua tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.”

Wanafiki wanaogopa kuteremshiwa sura itakayowatajia (unafiki wao uliomo katika nyoyo zao). Sema: Fanyeni mzaha, hakika Mwenyeezi Mungu atayatoa mnayoyaogopa. Na kama ukiwauliza: Lazima watasema; Sisi tulikuwa tukidhihaki na kucheza tu. Sema: Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Mwenyeezi Mungu Aya zake na Mtume wake? 9:64-65.

“Ewe Nabii! Pigana na makafiri na wanafiki na uwe mgumu kwao, na makazi yao ni Jahannam hayo ni marejeo mabaya.” 9:73.

C) VIONGOZI WAOVU

Anasema Mwenyeezi Mungu: “Wamewafanya makasisi wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyeezi Mungu na Masihi mwana wa Mariam, hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Mwenyeezi Mungu Mmoja, hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, ametakasika na yale wanayomshirikisha nayo.”9:31.

Hapa, siyo makusudio kuwa raia au wafuasi waliamini kuwa viongozi wao ni miungu hasa, la, lakini makusudio hapa ni kwamba: Wao waliwatii zaidi kila walisemalo na walifanyalo. Anasema Mwenyeezi Mungu: “Enyi mlioamini! Hakika wengi katika makasisi na watawa wanakula mali za watu kwa batili na kuwazuia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu.” 9:34.

Iliposemwa: “Wanakula mali za watu kwa batili” maana yake, walikuwa wakichukua rushwa ili kusamehe au kulegeza baadhi ya hukumu za Sharia.

Iliposemwa: “Na wanazuia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu’ Maana yake, wao pamoja na kula kwao haramu, waliwazuia watu kufuata haki. Makasisi na watawa huzitumia serikali zinazotawalakuwatesa na kuwauwa wale v.anaopingana nao katika itikadi.

D) UASI

Uasi ni moja kati ya sababu ambazo ziliwaingiza watu katika farka, kama anavyosema Mwenyeezi Mungu: “Watu walikuwa kundi rnoja, basi Mwenyeezi Mungu akawapelekea Manabii watoao khabari njema na waonyao, na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa haki, ili ahukumu baina ya watu katika yale waliyokhitilafiana. Wala hawakukhitilafiana katika hicho (Kitabu) ila wale waliopewa (Kitabu) baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi, kwa sababu ya Uasi kati yao. Hapo Mwenyeezi Mungu akawaongoza walioamini kwa yale waliyokhitilafiana katika haki kwa idhini yake na Mwenyeezi Mungu humuongoza amtakaye kwenye njia iliyonyooka.” 2:213.

“Na kwa hakika tuliwapa wana wa Israeli Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawapa vitu vizuri na tukawafadhili kuliko walimwengu. Na tukawapa maelezo ya amri, lakini hawakukhitilafiana ila baada ya kuwafikia elimu, kwa Uasi baina yao (tu) hakika Mola wako atahukumu kati yao siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana.” 45:16-17.

Na, kati ya sababu zilizowaingiza watu katika farka ni tukio zima la Saqifa Bani Saaidah. Ukitaka kufahamu tena, lisome tukio hilo katika tafsiri yetu.

E) HADITHI ZA UONGO

Kuzuia hadithi za uongo, ni jambo lililosababisha watu kuingia katika farka.

Anasema Abu Huraira kuwa: “Miji minne ni katika miji ya Peponi: Makka, Madina, Baytul Muqaddas na Dimashq. Ama, miji ya Motoni ni: kostontiniya, Tabariyya, Antokiya na Swan’aa.”

Abu Huraira anasema tena: “Bila shaka utakombolewa mji wa Kostontiniyya na Amiri bora zaidi, ni Amiri wa Kostontiniyya, na jeshi bora zaidi ni jeshi hilo.”

Kumbuka, Amiri wa jeshi lililoukomboa mji wa Kostontiniyya alikuwa Yazid bin Muawiya.

Taz: Adh’waau alaa Sunnatil Muhamadiyya Uk. 121 na 129

Anasema Abdul Karim bin Abil A’wjaa: “Wallahi ingawa mtaniuwa, kwa kweli nimekwisha weka hadithi (za uongo) elfu nne, nikiharamisha humo halali na nikihalalisha haramu.

Taz: Tarekhut Tabari J.6  Uk. 299

23. Na katika dalili zake ni kulala kwenu kwa usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhili yake. Hakika katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaosikia.

24. Na katika dalili zake ni kukuonyesheni umeme kwa khofu na tumaini na kuteremsha maji kutoka mawinguni, kwa hayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaofahamu.

25. Na katika dalili zake ni kuwa mbingu na ardhi husimama kwa amri yake, kisha atakapokuiteni wito mmoja, nanyi ndipo mtatoka ardhini.

26. Vilivyomo mbinguni na ardhini ni vyake, vyote humtii.

27. Na yeye ndiye anayeanzisha kiumbe tena atakayekirudisha, na jambo hili ni rahisi kwake, na sifa zilizotukuka katika mbingu na ardhi ni zake, naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

28. Amekupigieni mfano kwa hali ya nafsi zenu: Je, katika hao waliomilikiwa na mikono yenu kuna washirika wenu katika yale tuliyo kupeni hata mkashiriki sawa sawa, mkawaogopa kama mnavyoogopana wenyewe? Hivyo ndivyo tunavyozieleza Aya kwa watu wanaofahamu.

29. Lakini waliodhulumu walifuata matamanio yao pasipo kujua, basi ni nani awezaye kumuongoza ambaye Mwenyeezi Mungu amempoteza? Nao hawatakuwa na wasaidizi.

30. Basi uelekeze uso wako kwa dini iliyo sawa sawa ndilo umbile Mwenyeezi Mungu alilowaumba watu. Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe wa Mwenyeezi Mungu, hiyo ndiyo dini iliyo haki lakini watu wengi hawajui.

31. Nyenyekeeni kwake na mcheni, na simamisheni swala, wala msiwe katika washirikina.

32. Katika wale walioitenga dini yao na wakawa makundi makundi, kila kundi hufurahia waliyo nayo.

33. Yakiwapata watu madhara humuomba Mola wao kwa kumnyenyekea kisha anapowaonjesha rehema yake, hapo baadhi yao mara humshirikisha Mola wao.

34. Kwa kuyakataa tuliyowapa, basi stareheni, karibuni mtajua.

35. Je, tumewateremshia dalili inayowaambia juu ya yale wamshirikishayo nayo?

36. Na tunapowaonjesha watu rehema, huifurahia, na kama ukiwafikia ubaya kwa sababu ya yale iliyoyatanguliza mikono yao, mara wanakata tamaa.

37. Je, hawaoni ya kwamba Mwenyeezi Mungu hutoa riziki nyingi kwa amtakaye na hudhikisha? Bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaoamini.

38. Basi mpe jamaa haki yake na masikini na msafiri, hayo ni hora kwa wale wanaotaka radhi ya Mwenyeezi Mungu na hao ndio wenye kufaulu.

39. Na riba ile mtoayo ili izidi katika mali ya watu, basi mbele ya Mwenyeezi Mungu haizidi, lakini (mali) mnayoitoa zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyeezi Mungu, basi hao ndio wazidishao (mali zao).

40. Mwenyeezi Mungu ndiye aliyekuumbeni kisha akakupeni riziki kisha atakufisheni, kisha atakufufueni. Je, miongoni mwa washirika wenu yuko awezae kufanya lolote katika hayo? Yeye ameepukana na upungufu na yu juu kabisa kuliko yale wanayomshirikisha nayo.

41. Uharibifu umedhihiri barani na baharini kwa sababu ya yale iliyoyafanya mikono ya watu, ili awaonjeshe (adhabu ya) sehemu ya waliyoyafanya huenda wakarudi.

42. Sema: Nendeni katika ardhi na tazameni jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waliotangulia, wengi wao walikuwa washirikina.

43. Basi uelekeze uso wako katika dini iliyo na haki kabla ya kufika siku isiyozuilika kutoka kwa Mwenyeezi Mungu siku hiyo watatengana.

44. Anayekufuru, basi (madhara ya ) kufru yake ni juu yake, na afanyae mema, basi (hao) wanazitengenezea nafsi zao.

45. Ili awalipe wale walioamini na kufanya vitendo vizuri katika fadhili yake. Bila shaka yeye hawapendi makafiri.

46. Na katika dalili zake ni kuzituma pepo ziletazo khabari nzuri, na ili kuwaonjesheni rehema yake, na ili yatembee majahazi kwa amri yake, na mzitafute fadhili zake, na ili mshukuru.

47. Na kwa hakika tuliwatuma Mitume kwa watu wao, na wakawafikia kwa Miujiza wazi wazi, kisha tukawaadhibu wale waliokosa, na ilikuwa haki juu yetu kuwasaidia waumini.

48. Mwenyeezi Mungu ndiye anayezituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapowafikishia awatakao katika waja wake, mara wao huwa na furaha.

49. Na ingawa kabla ya kuwateremshia walikuwa wenye kukata tamaa.

50. Basi ziangalie alama za rehema ya Mwenyeezi Mungu jinsi anavyoihuisha ardhi baada va kufa kwake, bila shaka yeye ndiye Mwenye kuhuisha wafu, naye ndiye Mwenye uwezo juu ya kila kitu.

51. Na kama tukiutuma upepo na wakauona umekuwa rangi ya manjano, juu ya haya kwa hakika wataendelea kukufuru.

52. Na wewe, bila shaka huwezi kuwasikilizisha wafu, wala huwezi kuwasikilizisha viziwi wito, watakapogeuka kurudi nyuma.

53. Wala huwezi kuwaongoza vipofu katika upotovu wao huwasikilizishi ila wanaoziamini Aya zetu, hao ndio wenye kunyenyekea.

54. Mwenyeezi Mungu ndiye aliyekuumbeni katika udhaifu, na baada ya udhaifu akafanya nguvu, kisha baada ya nguvu akaufanya udhaifu na uzee, huumba apendavyo, naye ni Mjuzi Mwenye uwezo.

55. Na siku kitakaposimama Kiyama waovu wataapa ya kwamba Hawakukaa (ulimwenguni) isipokuwa saa moja tu, hivyo ndivyo walivyokuwa wakigeuzwa.

56. Na waliopewa elimu na imani watasema: Hakika nyinyi mmekaa kwa hukumu ya Mwenyeezi Mungu mpaka siku ya ufufuo, basi hii ni siku ya ufufuo, lakini mlikuwa hamjui.

57. Na siku hiyo hautawafaa waliodhulumu udhuru wao, wala hawatapokelewa toba yao.

58. Na kwa hakika tumepiga mfano wa kila namna kwa ajili ya watu katika Our’an hii, na kama ukiwajia na hoja yoyote, bila shaka wale waliokufuru watasema; Nyinyi si chochote ila ni wabatilishaji (haki).

59. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyopiga muhuri katika nyoyo za wale wasiofahamu.

60. Basi subiri, bila shaka ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni haki, wala wasikuhafifishe wale wasiokuwa na yakini.