Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 55
Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Saa (ya kulika Kiyama) imekaribia, na mwezi umepasuka.
2. Na wakiona Muujiza hugeuka upande na kusema: Uchawi unaoendelea.
3. Na walikadhibisha na wakafuata tamaa zao, na kila jambo limewekwa kwa wakati wake.
4. Na kwa hakika zimewafikia baadhi ya khabari zenye kukataza.
5. (Zenye) hekima kamili, lakini maonyo hayafai.
6. Hivyo jiepushe nao, siku atakapoita mwitaji kwenye jambo zito.
7. Macho yao yatainama watatoka katika makaburi kama kwamba ni nzige waliotawanyika.
8. Wakimkimbilia mwitaji, watasema makafiri; Siku hii ni siku ngumu.
9. Kabla yao watu wa Nuhu walikadhibisha walimkadhibisha mja wetu na wakasema ni mwendawazimu, na akakemewa.
10. Ndipo akamuomba Mola wake: Kwa hakika nimeshindwa, kwa hiyo nisaidie.
11. Mara tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika.
12. Na tukazibubujisha chemchem katika ardhi na maji yakakutana juu ya jambo lililokadiriwa.
13. Na tukamchukua juu ya ile (jahazi) iliyotengenezwa kwa mbao na misumari.
14. Ikaenda mbele ya macho yetu, ni tunzo kwa yule aliyekuwa amekataliwa.
15. Na kwa hakika tuliiacha iwe dalili lakini je, yuko anayekumbuka?
16. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
17. Na kwa hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kufahamika, lakini je, yuko anayekumbuka?
18. Walikadhibisha kina Adi, basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
19. Hakika tuliwapelekea upepo mkali katika siku ya nuksi iendeleayo.
20. Ukiwang’oa watu kama kwamba ni magogo ya mitende yaliyong’olewa.
21. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu.
22. Na kwa hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kufahamika, lakini je, yuko anayeikumbuka?
23. Thamudi waliwakadhibisha waonyaji.
24. Na wakasema: Je, tumfuate mtu mmoja miongoni mwetu! kwa hakika ndipo tutakuwa katika upotovu na kichaa.
25. Je, ameteremshiwa ukumbusho kati yetu? bali yeye ni muongo ajivunaye.
26. Watajua kesho ni nani muongo ajivunaye.
27. Kwa hakika tutampeleka ngamia jike ili kuwajaribu, basi uwaangalie na usubiri.
28. Na uwaambie kuwa maji yamegawanywa baina yao, kila (sehemu ya) maji itahudhuriwa.
29. Basi wakamwita rafiki yao naye akashika (upanga) akamkata (ngamia) miguu.
30. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!
31. Kwa hakika tuliwapelekea mngurumo mmoja tu, basi wakawa kama majani makavu yaliyosagika.
32. Na bila shaka tumeifanya Our’an iwe nyepesi kufahamika, lakini je, yuko anayeikumbuka?
33. Watu wa Luti waliwakadhibisha waonyaji.
34. Hakika sisi tuliwapelekea tufani ya mawe isipokuwa wafuasi wa Luti, tukawaokoa karibu na alfaiiri.
35. Kwa neema iliyotoka kwetu, hivyo ndivyo tunavyomlipa anayeshukuru.
36. Na kwa hakika yeye aliwaonya adhabu yetu, lakini (wao) waliyatilia shaka maonyo.
37. Na wakamtaka asiwaangalie wageni wake, ndipo tukayapofusha macho, basi onjeni adhabu yangu na maonyo yangu.
38. Na kwa hakika adhabu iendeleayo ikawafikia asubuhi.
39. Basi onjeni adhabu yangu na maonyo yangu.
40. Na bila shaka tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kufahamika, lakini je, yuko anayeikumbuka?
41. Na kwa hakika Waonyaji waliwafikia watu wa Firaun.
42. Wakakadhibisha Aya zetu zote, kwa hiyo tukawaadhibu kwa adhabu ya Mwenye nguvu, Mwenye uwezo.
43. Je, makafiri wenu ni bora kuliko hao, au je, yameandikwa Vitabuni kwamba nyinyi mtaachwa?
44. Au wanasema: Sisi ni wengi na tunaweza kujinusuru.
45. (Waambie); Wingi (wao huo) karibu watashindwa na watageuza migongo.
46. Lakini Kiyama ndio wakati wao, na saa hiyo ni nzito sana na chungu sana.
47. Bila shaka waovu wamo katika upotovu na kichaa.
48. Siku watakayokokotwa Motoni kifudi fudi; Onjeni mguso wa Jahannam.
49. Kwa hakika sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.
50. Na haiwi amri yetu ila moja tu, kama kukapua macho.
51. Na bila shaka tumekwisha waangamiza wenzenu, lakini je, yuko anayekumbuka?
52. Na kila jambo walilofanya limo madaftarini.
53. Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.
54. Bila shaka wamchao (Mwenyeezi Mungu) watakuwa katika Mabustani na mito.
55. Katika makao mazuri karibu na mfalme Mwenye uwezo.