Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 45
Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Qaaf. Naapa kwa Our’an tukufu.
2. Bali wanastaajabu kuwa amewafikia Muonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu.
3. Je, tutakapokufa na tukawa udongo! marejeo hayo ni ya mbali.
4. Kwa hakika tunajua yale ardhi inayowapunguzia, na kwetu kiko Kitabu kinacho hifadhi.
5. Lakini waliikadhibisha haki ilipowafikia, na wamo katika jambo linalohangaisha.
6. Je, hawaioni mbingu iliyo juu yao, tumeijengaje na tumeipambaje wala haina ufa?
7. Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima na tukaimeesha mimea mizuri ya kila namna.
8. Ndiyo busara na ukumbusho kwa kila mtu mwelekevu.
9. Na tumeyateremsha kutoka mawinguni maji yaliyobarikiwa, na kwa hayo tukameesha mabustani na nafaka zivunwazo.
10. Na mitende mirefu yenye makole yaliyozaa kwa wingi.
11. Chakula kwa ajili ya waja (wangu) na tukaufufua kwa (maji) hayo mji uliokufa, hivyo ndivyo ulivyo ufufuo.
12. Walikadhibisha kabla yao watu wa Nuhu na wakazi wa Rass na Thamudi.
13. Na Adi na Firaun na watu wa Luti.
14. Na wakazi wa machakani na watu wa Tubbaa, wote waliwakadhibisha Mitume, kwa hiyo onyo (langu) likathibitika.
15. Je, tulichoka kwa umbo la kwanza? bali wao wamo katika shaka juu ya umbo jipya.
16. Na bila shaka tumemuumba mtu nasi tunayajua yanayompitikia katika nafsi yake nasi tuko karibu naye zaidi kuliko mshipa wa shingo (yake).
17. Wanapopokea wapokeaji wawili anayekaa kuliani na (anayekaa) kushotoni.
18. Hatoi kauli yoyote isipokuwa karibu naye yuko mngojeaji tayari (kuandika).
19. Na kutoka roho kutakapomfia kwa haki, hayo ndiyo uliyokuwa ukiyakimbia.
20. Na itapulizwa parapanda, hiyo ndiyo siku ya miadi.
21. Na itakuja kila nafsi pamoja na muendeshaji na shahidi.
22. Kwa hakika ulikuwa huna khabari ya jambo hili, lakini tumekuondolea pazia lako na kuona kwako leo kuwa kukali.
23. Na mwenzake atamwambia: Haya ndiyo yaliyowekwa tayari kwangu.
24. Mtupeni katika Jahannam kila kafiri asi.
25. Akatazae kheri, arukae mipaka, mwenye shaka.
26. Aliyeweka rnungu mwingine pamoja na Mwenyeezi Mungu, basi mtupeni katika adhabu kali.
27. Mwenzake atasema: Ee Mola wetu! sikumpoteza bali yeye alikuwa katika upotovu wa mbali.
28. Mwenyeezi Mungu atasema: Msigombane mbele yangu, nilikwisha watangulizieni onyo.
29. Kwangu kauli haibadilishwi, wala mimi siwadhulumu waja (wangu).
30. Siku tutakayoiambia Jahannam: je, umejaa? Nayo itasema: Je, kuna zaidi?
31. Na Pepo italetwa karibu kwa wamchao (Mwenyeezi Mungu) haiko mbali.
32. Hii ndiyo mnayoahidiwa, kwa kila aelekeaye, ajilindaye (na maasi).
33. Anayemuogopa Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema faraghani na akafa kwa moyo uelekeao.
34. Ingieni (Peponi) kwa salama, hiyo ni siku ya kukaa milele.
35. Humo watapata chochote wakitakacho, na kwetu kuna zaidi.
36. Na vizazi vingapi tumeviangamiza kabla yao waliokuwa na nguvu zaidi kuliko wao, nao walitembea katika miji mingi je, yako makimbilio.
37. Kwa hakika katika hili mna ukumbusho kwa mwenye moyo au kwa ategaye sikio naye mwenyewe ni shahidi.
38. Na bila shaka tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika nyakati sita, wala uchovu haukutugusa.
39. Basi vumilia hayo wasemayo na mtukuze Mola wako kwa kumsifu kabla ya kutoka juu na kabla ya kuchwa.
40. Na katika usiku mtukuze na (pia) baada ya kusujudu.
41. Na sikia siku atakayonadi mwenye kunadi toka mahala pa karibu.
42. Siku watakayosikia ukelele kwa haki, hiyo ndiyo siku ya kutoka.
43. Bila shaka sisi tunahuisha na tunafisha, na marudio ni kwetu.
44. Siku itakapowapasukia ardhi, (watoke humo) upesi, huo ni mkusanyo rahisi kwetu.
45. Sisi tunajua sana wanayoyasema, wala wewe si jabari juu yao, kwa hiyo mkumbushe kwa Qur’an anayeogopa onyo langu.