Surah Nur

Sura hii imeteremshwa Madina, ina Aya 64

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Ni sura tumeiteremsha, na tumeilazimisha, na tumeteremsha ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke.

2. Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, basi mpigeni kila mmoja wao mijeledi mia. Wala isiwashikeni kwa ajili yao huruma katika hukumu ya Mwenyeezi Mungu ikiwa nyinyi mnamwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho na lishuhudie adhabu yao kundi la waumini.

3. Mwanamume mzinifu haoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina, na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina, na hayo yameharamishwa kwa waumini.

4. Na wale wanaowasingizia wanawake waaminifu kisha hawaleti mashahidi wanne, basi wapigeni mijeledi themanini na msiwakubalie ushahidi wao kabisa na hao ndio mafasiki.

5. Isipokuwa wale wenye kutubu baada ya hayo na wakasahihisha, basi bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu.

6. Na wale wanaowasingizia wake zao (kuwa wamezini) na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudulia mara nne kwa kiapo cha Mwenyeezi Mungu, kwamba: Bila shaka yeye ni katika wasema kweli.

7. Na mara ya tano (aape) kwamba: Laana ya Mwenyeezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.

8. Na (mkewe) itamuondokea adhabu kwa kutoa ushahidi mara nne kwa kiapo cha Mwenyeezi Mungu, kwamba: Huyu (mume) ni miongoni mwa waongo.

9. Na mara ya tano (aape) kwamba: Ghadhabu ya Mwenyeezi Mungu iwe juu yake kama (mumewe) ni miongoni mwa wakweli.

10. Na lau isingelikuwa fadhili ya Mwenyeezi Mungu juu yenu na rehema yake (mngetaabika) na kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mpokeaji wa toba, Mwenye hekima.

11. Hakika wale walioleta uongo ni kundi miongoni mwenu. Msiufikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu, kila mtu katika wao atapata aliyoyachuma katika madhambi, na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kubwa.[1]

12. Mbona mlipousikia, wanaume waumini na wanawake waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhahiri?

13. Mbona hawakuleta mashahidi wanne? Na ilivyokuwa hawakuleta mashahidi, basi hao mbele ya Mwenyeezi Mungu ndio waongo.

14. Na kama isingelikuwa juu yenu fadhili ya Mwenyeezi Mungu na rehema yake katika dunia na Akhera, bila shaka ingelikupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyojiingiza.

15. Mlipoupokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyoyajua, na mliufikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Mwenyeezi Mungu ni kubwa.

16. Na mbona mlipousikia hamkusema: Haitupasi kuzungumza haya, utakatifu ni wako, huu ni uongo mkubwa.

17. Mwenyeezi Mungu anakunasihini, msirudie kabisa mfano wa haya, ikiwa nyinyi ni wenye kuamini.

18. Na Mwenyeezi Mungu anakubainishieni Aya (zake) na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.

19. Kwa hakika wale wanaopenda uenee uchafu kwa walioamini, watapata adhabu yenye kuumiza katika dunia na Akhera, na Mwenyeezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.

20. Na isingelikuwa fadhili ya Mwenyeezi Mungu juu yenu na rehema yake na kwamba Mwenyeezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu (yangetokea machafuko makubwa).

21. Enyi mlioamini! msifuate nyayo za shetani, na atakayefuata nyayo za shetani, basi hakika yeye huamrisha mambo ya aibu na maovu, na lau kuwa si fadhili za Mwenyeezi Mungu na rehema zake asingelitakasika miongoni mwenu hata mmoja, lakini Mwenyeezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

22. Na wasiape wale wenye utajiri na wenye wasaa (kujizuia) kuwapa walio jamaa na masikini na waliohama katika njia ya Mwenyeezi Mungu, na wasamehe na waachilie, Je, nyinyi hampendi Mwenyeezi Mungu awasamehe? Na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

23. Bila shaka wale wanaowasingizia wanawake wanaojiheshimu, wasiojua (maovu) waumini, wamelaniwa katika dunia na Akhera, nao watapata adhabu kubwa.

24. Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao, kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.

25. Siku hiyo Mwenyeezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki, na watajua kuwa Mwenyeezi Mungu ndiye Haki iliyo wazi.

26. Wanawake wabaya ni kwa wanaume wabaya, na wanaume wabaya ni kwa wanawake wabaya, na wanawake wema ni kwa wanaume wema na wanaume wema ni kwa wanawake wema, hao wameepushwa na hayo wanayoyasema, wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.

27. Enyi mlioamini! Msiingie nyumba ambazo si nyumba zenu mpaka muombe ruhusa, na muwatolee salamu waliomo humo, hayo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka.

28. Na kama hamtamkuta humo yeyote, basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini, basi rudini, ni takaso kwenu, na Mwenyeezi Mungu anajua mnayoyatenda.

29. Si vibaya kwenu kuingia majumba yasiyokaliwa mlimo na manufaa yenu na Mwenyeezi Mungu anajua mnayoyadhihirisha na mnayoyaficha.

30. Waambie waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao, bila shaka Mwenyeezi Mungu anazo khabari za yale wanayoyafanya.

31. Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, na wasionyeshe uzuri wao ila kwa’ waume zao, au baba zao, au baba za waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao, au wanawake wenzao, au wale waliomilikiwa na mikono yao au wafuasi  wanaume wasio na matamanio (kwa wanawake) au watoto ambao hawajajua siri za wanawake. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubieni nyote kwa Mwenyeezi Mungu enyi wenye kuamini ili mpate kufaulu.[2]

32. Na waozeni wajane miongoni mwenu na wawezao kuowa na kusimamia haki zake katika watumwa wenu na wajakazi wenu, wakiwa mafakiri Mwenyeezi Mungu atawatajirisha katika fadhili zake, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.[3]

33. Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea mpaka Mwenyeezi Mungu awatajirishe kwa fadhili zake. Na wale wanaotaka kuandikiwa katika wale waliomilikiwa na mikono yenu, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyeezi Mungu aliyokupeni wala msiwashurutishe vijana wenu wa kike kufanya ukahaba kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ili hali wao wanataka kujiheshimu. Na takayewalazimisha, basi hakika Mwenycezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu

34. Na bila shaka tumekuteremshieni Aya zinazoeleza wazi wazi na mifano kutokana na waliotangulia kabla yenu, na mawaidha kwa wacha Mungu.

35. Mwenyeezi Mungu ni nuru ya mbingu na ardhi, mfano wa nuru yake ni kama shubaka ndani yake mna taa. Taa ile imo katika tungi, tungi lile ni kama nyota ing’aayo inayowashwa katika mti uliobarikiwa wa mzaituni, si wa mashariki wala magharibi yanakaribia mafuta yake kung’aa ingawa moto haujayagusa, nuru juu ya nuru, Mwenyeezi Mungu humuongoza kwenye nuru yake amtakaye, na Mwenyeezi Mungu hupiga mifano kwa watu, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

36. Katika Nyumba ambazo Mwenyeezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, humtukuza humo asubuhi najioni.[4]

37. Watu ambao haiwashughulishi biashara wala kuuza kunikumbuka Mwenyeezi Mungu, na kusimamisha swala, na kutoa zaka, wakiogopa siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.

38. Ili Mwenyeezi Mungu awalipe mazuri ya yale waliyoyafanya, na kuwazidishia katika fadhili zake, na Mwenyeezi Mungu humruzuku amtakaye pasipo hesabu.

39. Na wale waliokufuru vitendo vyao ni kama mazigazi jangwani mwenye kiu huyadhani ni maji hata ayafikiapo hapati chochote, na humkuta Mwenyeezi Mungu hapo, naye humpa hesabu yake sawa sawa, na Mwenyeezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.

40. Au ni kama giza katika bahari yenye maji mengi, inayofunikwa na mawimbi, juu ya mawimbi najuu yake kuna mawingu, giza juu ya giza, anapoutoa mkono wake anakaribia asiuone, na ambaye Mwenyeezi Mungu hakumjaalia nuru, basi huyo hana nuru.

41. Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu vinamtukuza vilivyomo mbinguni na ardhini, na ndege kwa kukunjua mbawa zao? kila mmoja amekwisha jua swala yake na namna ya kumtakasa, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa yale wanayoyafanya.

42. Na ni wa Mwenyeezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa Mwenyeezi Mungu tu ndiko marejeo.

43 Je, huoni kwamba Mwenyeezi Mungu anayaendesha mawingu, kisha huyagandisha pamoja, kisha huyarundika, na unaona mvua ikitoka katikati yake, naye huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamfikishia amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye, hukaribia mwanga wa umeme wake kupofua macho.

44. Mwenyeezi Mungu hubadilisha usiku na mchana, bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa wenye busara.

45. Na Mwenyeezi Mungu amemuumba kila mnyama kwa maji, wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine wao huenda kwa miguu miwili na wengine wao huenda kwa (miguu) minne, Mwenyeezi Mungu huumba atakayo hakika Mwenyeezi Mungu anao uwezo juu ya kila kitu.

46. Kwa hakika tumeteremsha Aya zinazo bainisha, na Mwenyeezi Mungu humuongoza anayetaka kwenye njia iliyo nyooka.

47. Na wanasema: Tumemuamini Mwenyeezi Mungu na Mtume, na tumetii, kisha hugeuka kundi moja kati yao baada ya hayo, wala hao si wenye kuamini.

48. Na wanapoitwa kwa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake ili awahukumu baina yao, ndipo kundi moja miongoni mwao linajitenga.

49. Na kama ikiwa haki ni yao, wanamfikia kwa kutii.

50. Je, wana maradhi katika nyoyo zao, au wanashaka, au wanaogopa kuwa atawadhulumu Mwenyeezi Mungu na Mtume wake? Bali hao ndio madhalimu.

51. Hakika kauli yaWaumini wanapoitwa kwa Mwenyeezi Mungu na Mtume wake ili awahukumu baina yao, husema: Tunasikia na tunakubali, na hao ndio wenye kufaulu.

52. Na anayemtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na kumnyenyekea Mwenyeezi Mungu na kumuogopa basi hao ndio watakaofuzu.

53. Na wanaapa kwa Mwenyeezi Mungu ukomo wa kiapo chao, kwamba:

ukiwaamrisha bila shaka wataondoka, sema: Msiape, utiifu unajulikana, hakika Mwenyeezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.

54. Sema: Mtiini Mwenyeezi Mungu na mtiini Mtume, na kama mkikataa, basi aliyolazimishwa yeye ni juu yake, na ni juu yenu mliyolazimishwa nyinyi na kama mkimtii mtaongoka, si vingine juu ya Mtume ila kufikisha (ujumbe wake) wazi wazi.

55. Mwenyeezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri, bila shaka atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale wa kabla yao, na lazima atawaimarishia dini yao aliyowapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wataniabudu, hawatanishirikisha na chochote, na afakayekufuru baada ya hayo, basi hao ndio wenye kuvunja amri.

56. Na simamisheni swala na toeni zaka na mtiini Mtume ili mrehemewe.

57. Msiwadhanie wale waliokufuru kuwa watamshinda (Mwenyeezi Mungu) katika ardhi, na makazi yao ni Moto na marudio (yao) bila shaka ni mabaya.

59. Enyi mlioamini! Wakuombeni ruhusa wale iliyowamiliki mikono yenu, na wale wasiofikia baleghe miongoni mwenu mara tatu: Kabla ya swala ya alfajirii na mnapovua nguo zenu adhuhuri na baada ya swala ya isha, hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya juu yenu wala juu yao baada ya nyakati hizo, mnazungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyo kuelezeni Aya (zake) na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

59. Na watoto watakapo baleghe miongoni mwenu, basi waombe ruhusa kama walivyoomba ruhusa wale wa kabla yao. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyokubainishieni Aya zake, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

60. Na wanawake wakongwe ambao hawatumaini kuolewa basi si vibaya kwao kufunua nguo zao, bila kuonyesha mapambo. Na kama wakijizuilia (kufunua hizo nguo) ni bora kwao, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mjuzi.

61. Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kilema, wala si vibaya kwa mgonjwa, wala kwenu, kama mkila katika nyumba zenu au nyumba za baba zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za ndugu zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za a’mi zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za dada wa mama zenu, au za wale mlio washikia funguo zao, au rafiki yenu. Si vibaya juu yenu kama mkila pamoja au mbali mbali. Na mnapoingia katika majumba basi mtoleane salamu, ni maamkio yanayotoka kwa Mwenyeezi Mungu yenye baraka njema. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyokubainishieni Aya ili mpate kufahamu.

62.  Waumini ni wale tu waliomwamini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, pia wanapokuwa pamoja naye kwa jambo linalohusiana na wote, hawaondoki mpaka wamuombe ruhusa, kwa hakika wale wanaokuomba ruhusa hao ndio wanaomuamini Mwenyeezi  Mungu na Mtume wake. Na watakapokuomba ruhusa kwa ajili ya baadhi ya kazi zao, basi mruhusu umtakaye miongoni mwao, na uwaombee msamaha kwa Mwenyeezi Mungu. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

63. Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Mwenyeezi Mungu anawajua miongoni mwenu wale waondokao kwa utoro wakijificha. Basi wajihadhari wale wanaokaidi amri yake, isije ikawapata balaa au ikawafikia adhabu yenye kuumiza.

64. Sikilizeni! kwa hakika ni vya Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Bila shaka anajua mliyo nayo, na siku watakaporudishwa kwake, basi atawaambia waliyoyafanya na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.