Surah Naml

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina  Aya 93

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

1. Twaa Syn. Hizo ni Aya za Qur’an na Kitabu kinacho bainisha.

2. Muongozo na khabari njema kwa wenye kuamini.

3. Ambao wanasimamisha swala na kutoa zaka nao wana yakini na Akhera

4. Kwa hakika wale wasioiamini Akhera tumewapambia vitendo vyao, lakini wana hangaika ovyo.

5. Hao ndio watakaopata adhabu mbaya na wao katika Akhera ndio wenye kupata khasara.

6. Na kwa hakika wewe unafundishwa Qur’an inayotokana kwa Mwenye hekima, Mwenye ujuzi.

7. (Kumbuka) Musa alipowaambia watu wake: Hakika nimeona moto, sasa hivi nitakuleteeni khabari au nitakuleteeni kijinga kiwakacho ili mpate kuota.

8. Basi alipoufikia, ikanadiwa kuwa: Amebarikiwa aliyomo katika moto na aliyoko pembeni mwake, na ametukuka Mwenyeezi Mungu, Mola wa walimwengu.

9. Ewe Musa! hakika mimi ndiye Mwenyeezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

10. Na itupe fimbo yako, lakini alipoiona ikiyumba kama nyoka akageuka kurudi nyuma wala hakungoja: Ewe Musa! usiogope, bila shaka Mimi mbele yangu hawaogopi Mitume.

11. Ila aliyedhulumu kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi kwa hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

12. Na ingiza mkono wako kifuani mwako utatoka mweupe pasipo ubaya, ni katika Miujiza tisa kwa Firaun na watu wake, hakika wao ni watu wenye kuvunja amri.

13. Basi ilipowafikia Miujiza yetu ionyeshayo, wakasema: Huu ni uchawi dhahiri.

14. Na wakaikataa hali nafsi zao zina yakini nayo, kwa dhulma na kujivuna, basi angalia ulikuwaje mwisho wa wenye kufanya ufisadi.

15. Na bila shaka tuliwapa Daudi na Suleiman elimu, na wakasema: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, aliyetufadhili kuliko wengi katika waja wake wenye kuamini.

 16. Na Suleiman alimrithi Daudi na akasema: Enyi watu! tumefundishwa usemi wa ndege na tumepewa kila kitu, hakika hii ndiyo fadhili (iliyo) dhahiri.

17. Na alikusanyiwa Suleiman majeshi yake kutoka katika majinni na watu na ndege, nayo yakawekwa makundi makundi.

18. Hata walipofika katika bonde la Namli (wadudu chungu) akasema mdudu chungu: Enyi wadudu chungu! ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Suleiman na majeshi yake, hali hawatambui.

19. Basi akatabasamu akiichekea kauli yake, na akasema: Ee Mola wangu! nipe nguvu nishukuru neema yako uliyonineemesha mimi na wazazi wangu na nipate kufanya vitendo vizuri uvipendavyo, na uniingize kwa rehema yako katika waja wako wema.

20. Na akawakagua ndege na akasema: Imekuwaje mbona simuoni Hud-Hudi au amekuwa miongoni mwa wasiokuwapo?

21. Lazima nitamuadhibu adhabu kali au nitamchinja, au ataniletea hoja iliyo wazi.

22. Basi hakukaa sana mara (Hud-Hud akafika) akasema: Nimegundua usilogundua, na ninakujia kutoka Sabaa na khabari zenye yakini.

23. Hakika nimekuta mwanamke anaye watawala naye amepewa kila kitu na anayo enzi kubwa.

24. Nimemkuta yeye na watu wake wakilisujudia jua badala ya Mwenyeezi Mungu, na shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia njia, kwa hiyo hawakuongoka.

 20. Mbona hawamsujudii Mwenyeezi Mungu ambaye huyatoa yaliyofichikana katika mbingu na ardhi na huyajua mnayoyaficha na mnayoyadhihirisha.

26. Mwenyeezi Mungu, hapana aabudiwaye ila yeye tu, Mola wa Enzi kubwa.

27. Akasema (Suleiman) Tutatazama kama umesema kweli au u katika waongo.

28. Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha uwaache, na utazame watarudisha nini?

29. (Malkia) akasema: Enyi wakuu (wa baraza!) Hakika nimeletewa baruatukufu.

30. Hakika imetoka kwa Suleiman, nayo ni kwa jina la Mwenyeezi Mungu, mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

31. Kwamba msinifanyie jeuri na fikeni kwangu hali yakuwa mmekwisha kusilimu.

32. (Malkia) akasema: Enyi wakuu! nipeni shauri katikajambo langu, maana sikati shauri lolote mpaka mhudhurie.

33. Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na ni wenye vita vikali, na hukumu ni juu yako, basi tazama ni nini unaamrisha.

34. (Malkia) akasema: Hakika wafalme wanapouingia mji, wanauharibu na wanawafanya watukufu wake kuwa dhalili hivyo ndivyo wanavyofanya.[1]

35. Na mimi ninawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayorudi nayo wajumbe.

36. Basi alipofika (mjumbe) kwa Suleiman akasema (Suleiman): Je, nyinyi mnanisaidia kwa mali? lakini aliyonipa Mwenyeezi Mungu ni bora kuliko aliyokupeni lakini nyinyi mnaifurahia zawadi yenu.

37. Rudi (nayo) kwao, lazima tutawaendea na majeshi wasiyoweza kuyakabili na bila shaka tutawafukuza humo wakidhalilika hali wamekuwa wanyonge.

38. (Suleiman) akasema: Enyi wakuu wa baraza! Ni nani atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajafika kwangu, hali ya kuwa wamekwisha kusilimu?

39. Akasema Afriti katika majinni: Mimi nitakuletea hicho kabla hujasimama kutoka mahala pako, na mimi bila shaka ninazo nguvu za hayo, (na) mwaminifu.

40. Akasema yule aliyekuwa na elimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea hicho kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni kwa fadhili za Mola wangu, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru? Na anayeshukuru, basi anashukuru kwa ajili ya nafsi yake na anayekufuru, kwa hakika Mola wangu ni Mkwasi, Mkarimu.

41. (Suleiman) Akasema: Kibadilini kiti chake cha enzi, tutaona kama ataongoka au atakuwa miongoni mwa wale wasioongoka.

42. Basi (Malkia) alipofika, akawaambia: Je, kiti chako cha enzi ni kama hiki? Akasema: kama ndicho hasa, nasi tulipewa elimu (ya Utume wako) kabla ya kuona Muujiza huu na tulikuwa wenye kunyenyekea.

43. Na (Suleiman) akamkataza yale aliyokuwa akiabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu, bila shaka (malkia) alikuwa katika watu makafiri.

44. Akaambiwa liingie jumba. Lakini alipoliona, akalidhani kuwa eneo la maji na akapandisha nguo mpaka katika miundi yake. (Suleirnan) akasema:

Hakika hilo ni jumba lililosakafiwa kwa vioo! Akasema (malkia): “Mola wangu! hakika nimedhulumu nafsi yangu na (sasa) najisalimisha pamoja na Suleiman kwa Mola wa walimwengu.”

45. Na bila shaka tuliwapelekea kina Thamudi ndugu yao Saleh, akawaambia:

Muabuduni Mwenyeezi Mungu. Basi mara wakawa makundi mawili wakigombana.

46. Akasema: Enyi watu wangu! kwanini mnauhimiza ubaya kabla ya wema? mbona hamuombi msamaha kwa Mwenyeezi Mungu ili mrehemewe?

47. Wakasema: Tumepata bahati mbaya kwa sababu yako na kwa sababu ya wale walio pamoja nawe. Akasema: Bahati yenu mbaya iko kwa Mwenyeezi Mungu lakini nyinyi ni watu mnaojaribiwa.

48. Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya matata katika ardhi wala hawakusuluhisha.

49. Wakasema: Apianeni kwa Mwenyeezi Mungu (kuwa) Tutamshambulia usiku yeye na watu wake, kisha kwa hakika tutamwambia mrithi wake, sisi hatukuona maangamio ya watu wake, na bila shaka sisi ni wa kweli.

50. Na wakafanya hila, nasi pia tukafanya hila hali hawatambui.

51. Basi angalia ulivyokuwa mwisho wa hila zao, hakika tuliwaangamiza pamoja na watu wao wote.

52. Basi hizo ni nyumba zao zilizoanguka kwa sababu walidhulumu, bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaojua.

53. Na tukawaokoa wale walioamini na waliokuwa wakimcha (Mwenyeezi Mungu).

54. Na Luti alipowaambia watu wake: Je, mnaufanya ubaya na hali mnaona.

55. Je, nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio mabaya badala ya wanawake? Bali nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.

56. Basi halikuwa jawabu la watu wake ila kusema: Wafukuzeni wafuasi wa Luti katika mji wenu, bila shaka wao ni watu wanaojitakasa.

57. Kwa hiyo tukamuokoa yeye na wafuasi wake ila mkewe, tukamkadiria katika wakaao nyuma.

58. Na tukawanyeshea mvua, ni mbaya mno mvua hiyo ya wale walioonywa.

59. Sema: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, na amani iwashukie waja wake ambao aliwachagua. Je, Mwenyeezi Mungu ni bora au wanaowashirikisha?

60. Au ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza? Nyinyi hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je, yupo mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Bali hao ni watu waliopotoka.

61. Au ni nani aliyeifanya ardhi kuwa mahala pa kustarehe na akaweka ndani yake mito na akaiwekea milima, na akaweka kizuizi kati ya bahari mbili? Je yuko mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Bali wengi wao hawajui.

62. Au ni nani anayemjibu aliyedhikika amuombapo na kuondoa dhiki, na kukufanyeni wenye kuendesha dunia? Je yuko, mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Ni kidogo mnayoyakumbuka.

63. Au ni nani anayekuongozeni katika giza la bara na bahari, na ni nani azipelekaye pepo kutoa khabari njema kabla ya rehema zake? Je, yuko mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Mwenyeezi Mungu ametukuka juu ya wale wanaowashirikisha.

64. Au ni nani anayeanzisha kiumbe kisha anakirudisha, na ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Je, yuko mungu pamoja na Mwenyeezi Mungu? Sema: Leteni dalili zenu ikiwa mnasema kweli.

65. Sema; Hakuna aliyoko katika mbingu na ardhi ajuaye yasiyoonekana ila Mwenyeezi Mungu tu, nao hawajui ni lini watafufuliwa.

66. Lakini imekwisha elimu yao juu ya Akhera, bali wao wamo katika shaka nayo, bali wao ni vipofu nayo.

67. Na wale waliokufuru wakasema: Je, tutakapokuwa udongo sisi na baba zetu, je, tutatolewa?

68. Bila shaka haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani, haya siyo ila ni visa vya watu wa kale.

69. Sema: Nendeni katika ardhi na muone jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waovu.

70. Wala usiwahuzunikie, wala usiwe katika dhiki kwa sababu ya hila wazifanyazo.

71. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini ikiwa mnasema kweli?

72. Sema: Bila shaka iko karibu kukufikieni sehemu ya yale mnayoyahimiza.

73. Na kwa hakika Mola wako ni Mwenye fadhili kwa watu, lakini wengi wao hawashukuru.

74. Na kwa hakika Mola wako anayajua yanayoficha vifua vyao na wanayoyadhihirisha.

75. Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika Kitabu kibainishacho.

76. Bila shaka Qur’an hii inawaeleza wana wa Israeli mengi ambayo kwa hayo wanakhitilafiana.

77. Na kwa hakika hiyo ni muongozo na rehema kwa wenye kuamini.

78. Hakika Mola wako atawakatia baina yao hukumu yake, naye ni Mwenye nguvu, Mjuzi.

79. Basi tegemea kwa Mwenyeezi Mungu hakika wewe uko juu ya haki iliyo wazi.

80. Kwa hakika huwezi kuwasikilizisha wafu, wala kuwasikilizisha viziwi mwito, wanapogeuka kurudi nyuma.

81. Wala huwezi kuwaongoza vipofu katika upotovu wao. Huwezi kumsikilizisha isipokuwa yule anayeziamini Aya zetu, basi hao ndio watii.

82. Na kauli itakapowathibitikia tutawatolea mnyama katika ardhi atakaye wasemeza kwa sababu watu walikuwa hawaziamini dalili zetu. 

83. Na siku tutakapokusanya katika kila umma kundi miongoni mwa wale wanaokadhibisha dalili zetu, nao watawekwa mafungu mafungu. 

84. Hata watakapofika, atasema: Je, nyinyi mlizikadhibisha Aya zangu pasipo kuzijua vyema? Au mlikuwa mkifanya nini?

85. Na itawathibitikia kauli kwa sababu walidhulumu, nao hawatasema.

86. Je, hawaoni kwamba tumeuumba usiku ili watulie humo, na mchana uangazao? kwa hakika katika hayo mna mazingatio kwa watu wenye kuamini.

87. Na siku litakapopulizwa parapanda, ndipo watahangaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini ila yule Mwenyeezi Mungu amtakaye, na wote watamfikia hali ya kuwa madhalili.

88. Na utaona milima utaidhania imeganda, nayo itapita mpito wa mawingu ndio sanaa ya Mwenyeezi Mungu aliyekitengeneza kila kitu, bila shaka yeye anazo khabari za mnayoyatenda.

89. Atakayeleta mema, basi atapata mema kuliko hayo, nao katika mahangaiko ya siku hiyo watasalimika.

90. Na watakaoleta ubaya, basi zitaangushwa nyuso zao Motoni, hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda.

91. Bila shaka nimeamrishwa nimwabudu Mola wa mji huu tu ambaye ameutukuza, na ni vyake vitu vyote, na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wanaonyenyekea.

92. Na kwamba nisome Qur’an. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa (faida ya) nafsi yake tu, na aliyepotea basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa Waonyaji tu.

93. Na sema: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu (ambaye) karibuni atakuonyesheni dalili zake na mtazifahamu, wala Mola wako haghafiliki na hayo mnayoyafanya.