Surah Najm

Sura hii imeteremshwa Makka, Aya 62.

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Naapa kwa nyota inapoanguka.

2. Kwamba mtu wenu hakupotea wala hakukosa.

3. Wala hasemi kwa tamaa (ya nafsi yake).

4. Hayakuwa haya ila ni Wahyi uliofunuliwa.

5. Amemfundisha Mwenye nguvu sana.

6. Mwenye uwezo, naye akastawi.

7. Naye yu katika upeo wa juu kabisa.

8. Kisha akakaribia, na akateremka.

9. Ndipo akawa umbali wa pinde mbili au karibu zaidi.

10. Na akamfunulia mja wake aliyoyafunua.

11. Moyo haukusema uongo uliyoyaona.

12. Je, mnabishana naye juu ya yale aliyoyaona?

13. Na bila shaka yeye amemuona (Jibril) kwa mara nyingine (katika sura ya kimalaika).

14. Penye mkunazi wa mwisho.

15. Karibu yake pana Bustani inayokaliwa.

16. Kilipoufunika mkunazi kilichofunika.

17. Jicho (lake) halikuhangaika wala halikuruka mpaka.

18, Kwa hakika aliona katika dalili za Mola wake zilizo kuu.

19. Je, mmewaona Lata na Uzza?

20. Na Manata, mwingine wa tatu?[1]

21. Je, nyinyi mna watoto wa kiume na yeye ana watoto wa kike?

22. Huo tena ni mgawanyo mbaya.

23. Hayakuwa haya ila ni majina mliyowapa nyinyi na baba zenu, Mwenyeezi Mungu hakuteremsha dalili juu yao. Hawafuati ila dhana na zinayoyapenda nafsi (zao) na kwa hakika muongozo umewafikia kutoka kwa Mola wao.

24. Je, mwanadamu anaweza kupata kila anachotamani?

25. Lakini mwanzo na mwisho ni wa Mwenyeezi Mungu.

26. Na wako Malaika wangapi mbinguni ambao uombezi wao hautafaa chochote isipokuwa baada ya Mwenyeezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia.

27. Hakika wale wasioamini Akhera wanawaita Malaika kwa majina ya kike.

28. Nao hawana elimu ya haya, hawafuati ila dhana, na kwa hakika dhana haisaidii chochote mbele ya haki.

29. Basi jiepushe na yule aupaye kisogo ukumbusho wetu na wala hataki ila maisha ya dunia.

30. Huo ni mwisho wao katika elimu, hakika Mola wako ndiye amjuaye sana anayepotea njia yake, na ndiye amjuaye sana anayeongoka.

31. Na ni vyake Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, ili awalipe wale waliofanya ubaya kwa yale waliyoyatenda, na kuwalipa mema wale waliofanya mema.

32. Ambao wanajiepusha na madhambi makuu na vitendo vibaya isipokuwa makosa hafifu, bila shaka Mola wako ndiye Mwenye msamaha mkubwa. Yeye ndiye anayekujueni sana tangu alipokuumbeni katika ardhi na mlipokuwa mimba matumboni mwa mama zenu, basi msijitakase nafsi zenu, yeye anamjua sana anayetakasika.

33. Je, umemuona yule aliyegeuka?

34. Na akatoa kidogo kisha akajiziwia.

35. Je, anayo elimu ya yasioonekana na akayona?

36. Au hakuambiwa yaliyomo katika Vitabu vya Musa?

37. Na vya Ibrahimu aliyetimiza ahadi.

38. Kwamba habebi mbebaji mzigo wa mwingine.

39. Na kwamba mtu hatapata ila yale aliyoyafanya.

40. Na kwamba amali yake itaonekana.

41. Kisha atalipwa malipo yaliyo kamili.

42. Na kwamba mwisho ni kwa Mola wako.

43. Na kwamba yeye ndiye anayechekesha na kuliza.

44. Na kwamba yeye ndiye afishaye na kuhuisha.

45. Na kwamba yeye ndiye aliyeumba dume na jike.

46. Katika mbegu ya uzazi inapotiwa.

47. Na kwamba juu yake ufufuo mwingine.

48. Na kwamba yeye ndiye atajirishaye na atiaye umasikini.

49. Na kwamba yeye ndiye Mola wa (nyota) ya Shi-iraa.

50. Na kwamba yeye ndiye aliyewaangamiza Adi wa kwanza.

51. Na Thamudi, hakuwabakisha.

52. Na kabla (yao) watu wa Nuhu, hakika wao walikuwa madhalimu na waasi sana.

53. Na miji iliyopinduliwa ndiye aliyeiangusha.

54. Vikaifunika vilivyoifunika.

55. Basi neema gani ya Mola wako unayoifanyia shaka?

56. Huyu ni Muonyaji miongoni mwa Waonyaji wa zamani.

57. Tukio lililo karibu linasogea.

58. Hakuna awezaye kuliondoa ila Mwenyeezi Mungu.

59. Je, mnaistaajabia hadithi hii?

60. Na mnacheka wala hamlii?

61. Na hali nyinyi mmeghafilika?

62. Basi msujudieni Mwenyeezi Mungu na Mumuabudu.