Sura hii imeteremshwa Makka, Aya 128
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu
1. Amri ya Mwenyeezi Mungu itafika (tu) basi msiihimize Ametakasika na katukuka kuliko wale wanaowashirikisha.
Aya 1
“Amri ya Mwenyeezi Mungu Itafika.” Tamko la asli tulilolifasiri ni; “ATAA” na maana yake ni: “Imefika” Hii ni; Istia’ratut tasrihiyyah.
2. Huwateremsha Malaika na Wahyi kwa amri yake juu ya anayemtaka katika waja wake kwamba; Onyeni kuwa hakuna aabudiwaye isipokuwa Mimi tu, basi niogopeni.
3. Ameziumba mbingu na ardhi kwa haki ametukuka kuliko wale wanaowashirikisha.
4. Amemuumba mwanadamu kwa tole la manii lakini mara amekuwa mshindani dhahiri.
5. Na (pia) amewaumba wanyama, katika hao mnapata (vifaa vitiavyo) joto na manufaa (mengine) na wengine mnakula.
6. Na mnaona raha mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka malishoni asubuhi.
7. Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye mji msikoweza kufika isipokuwa kwa kujitia tabu. Hakika Mola wenu ni Mpole sana Mwenye kurehemu.
8. Na (amewaumba) farasi na nyumbu na punda ili muwapande na (wawe) pambo, na ataumba (vingine) msivyovijua.
9. Na ni juu ya Mwenyeezi Mungu (kuonyesha) Njia iliyo sawa, na ziko (njia) zingine zisizo sawa, na kama angelipenda bila shaka angelikuongezeni nyinyi nyote.
10. Yeye ndiye anayekuteremshieni maji kutoka mawinguni kwa hayo nyinyi mnapata ya kunywa, na miti ya kulishia.
11. (Kwa hayo) hukuotesheeni mimea na mizaituni na mitende na mizabibu na kila matunda. Bila shaka katika hayo mna dalili (kubwa) kwa watu wenye kufikiri.
12. Na amekutiishieni usiku na mchana na jua na mwezi na pia nyota zimetiishwa kwa amri yake. Hakika katika hayo zimo dalili kwa watu wenye akili.
13. Na alivyo kuumbieni katika ardhi vya rangi mbali mbali. Hakika katika hayo mna dalili (kubwa) kwa watu wanaoshika mawaidha.
14. Na yeye ndiye aliyeitiisha bahari ili humo mle nyama laini, na mtoe humo mapambo mnayoyavaa. Na utaona majahazi yakipasua humo, na ili mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru.
15. Na akaweka katika ardhi milima ili isiyumbe nanyi, na mito na barabara ili mpate kuongoka.
16. Na (ameziweka) alama, na kwa nyota wao wanafuata njia.
17. Hivi yule anayeumba atakuwa sawa na yule asiyeumba? Je, hamkumbuki?
18. Na mkihesabu neema za Mwenyeezi Mungu hamtaweza kuzihesabu. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
19. Na Mwenyeezi Mungu anayajua mnayo yaficha na munayoyadhihirisha.
20. Na Wale ambao wanawaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu hawaumbi chochote. bali wao wameumbwa.
21. Ni wafu, si wazima, na hawajui watafufuliwa lini.
22. Mungu wenu ni Mungu Mmoja, lakini wale wasioamini Akhera nyoyo zao zinakataa, nao wanatakabari.
23. Bila shaka Mwenyeezi Mungu anajua wanayoyaficha na wanayoyadhihirisha, kwani yeye hawapendi wanaotakabari.
24. Na wanapoambiwa; Mola wenu ameteremsha nini? Wanasema: Hadithi za (watu) wa zamani.
25. Ili wabebe mizigo yao kamili siku ya Kiyama, na (pia) sehemu ya mizigo ya wale wanaowapoteza bila ya elimu. Sikilizeni! ni mabaya wanayoyabeba.
26. Walifanya vitimbi wale waliokuwa kabla yao, basi Mwenyeezi Mungu akayasukua majengo kwenye misingi, ndipo dari zikawaangukia kutoka juu yao na ikawafikia adhabu kutoka wasiko kujua.
27. Kisha siku ya Kiyama atawahizi na atasema: Wako wapi washirika wangu ambao kwa ajili yao mlikuwa mkigombana (na Manabii?) watasema wale waliopewa elimu; Hakika hizaya na msiba leo vitawafikia makafiri.
28. Ambao Malaika huwafisha hali wamejidhulumu nafsi zao, basi watasalimu amri (kwa Mwenyeezi Mungu) waseme: Hatukuwa tukifanya uovu wowote. Naam, Hakika Mwenyeezi Mungu anajua sana mliyokuwa mkitenda,
29. Kwa hiyo ingieni milango ya Jahannam humo mkae milele. Basi ni maovu mno makazi ya wenye kufanya kiburi.
30. Na wataambiwa wale wenye kumcha (Mwenyeezi Mungu) ni nini aliyoteremsha Mola wenu? wanasema: Kheri. Wale waliofanya wema katika dunia hii (pia) watapata wema na hakika nyumba ya Akhera ni nzuri, na ni bora kabisa nyumba ya wacha (Mungu).
31. Bustani za milele wataziingia (ambazo) inapita humo chini yake mito, humo watapata watakacho. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu awalipavyo wenye kumcha (Mwenyeezi Mungu).
32. Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema, wakasema: Amani iwejuu yenu, ingieni Peponi kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyatenda.
33. Hawangoji ila Malaika wawafikie au iwafikie amri ya Mola wako. Kama hivyo walifanya wale waliokuwa kabla yao. Na Mwenyeezi Mungu hakuwadhulumu, lakini walikuwa wamejidhulumu wenyewe.
34. Nasi ukawafikia uovu wa yale waliyoyafanya na ikawazunguka adhabu waliyokuwa wakiifanyia mzaha.
35. Na washirikisha wanasema: Mwenyeezi Mungu angelitaka tusingeliabudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeliharamisha chochote bila ya yeye. Kama hivyo walifanya waliokuwa kabla yao. Basi (si kazi ya) Mitume isipokuwa kufikisha (ujumbe) wazi wazi.
36. Na bila shaka tulimpeleka Mtume katika kila umma, ya kwamba:
Muabuduni Mwenyeezi Mungu na muepukeni shetani. Basi yuko miongoni mwao ambaye Mwenyeezi Mungu amemuongoza, na yuko miongoni mwao ambaye aliyethibitikiwa na upotovu. Basi tembeeni katika ardhi na muangalie ulikuwaje mwisho wa wenye kukadhibisha.
37. Ukiwa na hima ya kutaka kuwaongoza, basi hakika Mwenyeezi Mungu hamuongozi yule anayepoteza (wengine) na hawana wasaidizi.
38. Nao wakamuapa Mwenyeezi Mungu kwa kiapo chao cha nguvu (kwamba) Mwenyeezi Mungu hatamfufua afaye. Naam, ni ahadi iliyolazimika kwake, lakini watu wengi hawajui.
39. Ili kuwababainishia yale waliyokhitilafiana kwayo na wajue waliokufuru kuwa wao walikua waongo.
40. Hakika kauli yetu kwa kitu tunachokitaka ni kukiambia: Kuwa, basi kinakuwa.
41. Na wale waliohama kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu baada ya kudhulumiwa, bila shaka tutawakalisha katika dunia kwa wema, na malipo ya Akhera ni makubwa zaidi, laiti wangelijua!
42. (Hao ni) wale wanaosubiri na wakamtegemea Mola wao.
43. Nasi hatukuwapeleka (Mitume) kabla yako isipokuwa wanaume ambao tuliwapa Wahyi, basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.
Aya 43
Wenye kumbukumbu watakaoulizwa ni: Ahlul Bait (a.s)
Taz: Almizan fyi tafsiril Our’an J.12 Uk. 303
Albur’han fyi tafsiril Qur’an J.2 Uk. 369
Majmaul bayan fyi tafsiri Qur’an J.3 Uk. 362
Tafsirus Saafi j.3 Uk.137
44. Kwa hoja zilizo wazi na kwa maandiko na tumekuteremshia Qur’an ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, na ili wapate kufikiri.
45. Je, wameaminisha wale waliofanya vitimbi vibaya kwamba, Mwenyeezi Mungu hatawadidimiza katika ardhi au haitawafika adhabu kutoka wasikokujua?
46. Au hatawakamata katika kwenda kwao huko na huko, kisha hawataweza kuponyoka?
47. Au hatawakamata kwa kuwaadhibu kidogo kidogo? Hakika Mola wenu ni Mpole sana, Mwenye kurehemu.
48. Je, hawaoni kila kitu alichoumba Mwenyeezi Mungu, vivuli vyake vinazunguka kutoka kulia na kushoto vikimsujudia Mwenyeezi Mungu, hali ni vyenye kudhalilika.
49. Na vinamsujudia Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini katika wanyama na Malaika, nao hawatakabari.
50. Wanamuogopa Mola wao aliye juu yao, na wanatenda wanayoamrishwa.
51. Na Mwenyeezi Mungu amesema: Msifanye waungu wawili, hakika Yeye ni Mwenyeezi Mungu Mmoja tu, basi niogopeni Mimi tu.
52. Na ni vyake vilivyomo katika mbingu na ardhi, na ibada anastahiki yeye tu daima. Je, mtamuogopa (mwingine) asiyekuwa Mwenyeezi Mungu?
53. Na neema yoyote mliyo nayo, basi imetoka kwa Mwenyeezi Mungu kisha inapowaguseni dhara, basi mnamlilia yeye.
54. Kisha anapowaondoleeni dhara, mara kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao.
55. Ili wavikatae tulivyowapa, basi stareheni kidogo, nanyi hivi karibuni mtajua.
56. Na sehemu ya vile tulivyowapa wanawawekea (waungu wao) wasiofahamu. Wallahi, bila shaka nyinyi mtaulizwa juu ya yale mliyokuwa mkiyazua.
57. Na wanamuwekea Mwenyeezi Mungu mabinti, Subhana! hali wao hupata wanavyovitaka.
58. Na mmoja wao anapopewa habari ya (kuzaliwa mtoto) wa kike, uso wake huwa mweusi, naye kajaa chuki.
59 (Akawa) anajificha asionekane na watu kwa sababu ya habari mbaya aliyoambiwa. Je, akaenaye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? Tazama uovu wa wanavyohukumu.
60. Hali ya wale wasioamini Akhera ni mbaya, na Mwenyeezi Mungu ndiye Mwenye sifa tukufu, naye ni Mwenye nguvu Mwenye hekima.
61. Na lau Mwenyeezi Mungu anawatesa watu kwa sababu ya maasi yao, asingeliacha hata mnyama mmoja juu ya ardhi, lakini anawaakhirisha, mpaka muda uliowekwa. Na unapofika muda wao hawawezi kuikawiza saa moja wala hawawezi kuitanguliza.
62. Na wanampa Mwenyeezi Mungu wanavyovichukia, na ndimi zao zinasema uwongo kwamba wao watapata mema bila shaka wamewekewa Moto, nao wataachwa (humo).
63. Wallahi, Sisi tulipeleka (Mitume) kwa watu wa kabla yako, lakini shetani akawapambia vitendo vyao, kwa hiyo leo yeye ni kiongozi wao,
nao watapata adhabu yenye kuumiza.
64. Na hatukukuteremshia Kitabu isipokuwa uwabainishie yale ambayo wanakhitilafiana, na (pia kiwe) muongozo na rehema kwawatu wanaoamini.
65. Na Mwenyeezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, kwa hakika katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaosikia.
66. Na bila shaka katika nyama hoa liko fundisho kwa ajili yenu, Tunakunywesheni katika vile vilivyomo matumboni mwao, baina ya mavi na damu, maziwa safi mazuri kwa wanywao.
67. Na katika matunda ya mitende na mizabibu (ambayo) mnatengeneza ulevi na riziki nzuri. Hakika katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaotumia akili.
68. Na Mola wako akamfahamisha nyuki kwamba tengeneza majumba katika milima na katika miti na katika yale wanayojenga (watu).
69. Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako zilizofanywa nyepesi, Kinatoka katika matumbo yao kinywaji chenye rangi mbali mbali ndani yake kina matibabu kwa watu. Hakika katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaofikiri.
70. Na Mwenyeezi Mungu amekuumbeni kisha anakufisheni na miongoni mwenu yuko anayerudishwa katika umri wa unyonge kabisa akawa hajui chochote baada ya ujuzi (aliokuwa nao) kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Muweza.
71. Na Mwenyeezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki. Lakini wale waliofadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale waliomilikiwa na mikono yao ili wawe sawa katika (riziki) hiyo. Basi je, wanazikataa neema za Mwenyeezi Mungu?
72. Na Mwenyeezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu watoto na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri. Basi je, wanaamini batili na kuzikataa neema za Mwenyeezi Mungu?
73. Na wanawaabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu wasiowamilikishia riziki (hata kidogo) kutoka mbinguni na ardhini, wala hawana uwezo (wowote).
74. Basi msimpigie Mwenyeezi Mungu mifano, hakika Mwenyeezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
75. Mwenyeezi Mungu anapiga mfano wa mtumwa anayemilikiwa, asiyeweza chochote, na (mwingine) tuliyemruzuku kutoka kwetu riziki nzuri, naye anatoa katika hiyo kwa siri na dhahiri. Je, wako sawa? Alhamdulillah! lakini wengi wao hawajui.
76. Na Mwenyeezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili; Mmoja wao ni bubu hawezi chochote, naye ni mzigo juu ya bwana wake, popote amwelekezapo haleti kheri. Je, yeye anaweza kuwa sawa na yule anayeamuru kwa uadilifu naye yuko juu ya njia iliyonyooka?
77.Na iko kwa Mwenyeezi Mungu tu siri ya mbinguni na ardhini, wala halikuwa jambo la Kiyama ila ni kama kupepesa jicho au ni karibu zaidi. hakika Mwenyeezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
78. Na Mwenyeezi Mungu amekutoeni matumboni mwa mama zenu, hali yakuwa, hamjui chochote na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo ili mpate kushukuru.
79. Je, hawawaoni ndege waliotiishwa katika anga la mbingu? hakuna awazuiaye (angani wasianguke) isipokuwa Mwenyeezi Mungu. Hakika katika hayo mna mazingatio kwa watu wanaoamini.
80. Na Mwenyeezi Mungu amekujaalieni majumba yenu yawe makazi na (pia) amekujaalieni majumba katika ngozi za wanyama, mnazoziona nyepesi wakati wa safari yenu, na wakati wa kutua kwenu, na katika sufu zao, na manyoya yao, na nywele zao, (mnatengeneza) vyombo na vifaa (vya kutumia) kwa muda.
81. Na Mwenyeezi Mungu katika vitu alivyo viumba amekufanyieni vitu vitiavyo vivuli, na amekufanyieni makazi katika milima, na amekufanyieni kanzu zinakukingeni na joto, na nguo za chuma ndivyo hivyo anavyokutimizieni neema zake ili mpate kutii.
82. Lakini wakikataa, basi hakika juu yako ni kufikisha tu (ujumbe) ulio wazi.
83. Wanazijua neemaza Mwenyeezi Mungu, kisha wanazikanusha, na wengi wao ni makafiri.
84. Na siku tutakapowapeleka mashahidi katika kila umma, kisha haitaruhusiwa kwa waliokufuru (kutoa udhuru) wala hawataachiliwa kutaka radhi.
85. Na wale waliodhulumu watakapoiona adhabu, basi hawatapunguziwa wala hawatapewa muhula.
86. Na walioshirikisha watakapowaona washirika wao, watasema Mola wetu! hawa ndio washirika wetu ambao tulikuwa tukiwaabudu badala yako. Ndipo watakapowatupia neno: Hakika nyinyi ni waongo.
87. Na siku hiyo watasalimu amri mbele ya Mwenyeezi Mungu na yatawapotea waliyokuwa wakiyazua.
88. (Ama) wale waliokufuru na kuwazuia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu, tutawazidishia adhabu juu ya adhabu, kwa sababu walikuwa wakifisidi.
89. Na siku tutakapompeleka shahidi katika kila umma juu yao kutoka miongoni mwao, na wewe tutakuleta uwe shahidi juu ya hawa. Na tumekuteremshia Kitabu kielezacho kila kitu, na ni muongozo na rehema na khabari za furaha kwa wanaojisalimisha.
90. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu anaamrisha uadilifu na hisani na kuwapa jamaa, na anakataza uchafu na uovu na uasi, anakuwaidhini, ili mpate kukumbuka.
91. Na timizeni ahadi ya Mwenyeezi Mungu mnapoahidi wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha, hali mmekwisha mfanya Mwenyeezi Mungu kuwa mdhamini wenu. Hakika Mwenyeezi Mungu anayajua mnayoyafanya.
92. Wala msiwe kama yule mwanamke aliyekata uzi wake vipande vipande, baada ya kuusokota kuwa mgumu, mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana kati yenu ili lisije kundi moja la watu kuwa na nguvu zaidi kuliko kundi la watu wengine. Hakika Mwenyeezi Mungu anakujaribuni kwa (njia) hiyo, na bila shaka atakubainishieni siku ya Kiyama mliyokuwa nikikhitilafiana.
93. Na Mwenyeezi Mungu angelitaka bila shaka angelikufanyeni kundi moja, lakini anampoteza anayetaka, na anamuongoza anayetaka, na lazima mtaulizwa juu ya yale mliyokuwa mkiyafanya. ‘
94. Wala msivifanye vipao vyenu njia ya kudanganyana baina yenu, usije mguu ukateleza baada ya kuuimarisha na mkayaonja maovu kwa sababu ya wale mliowazuilia njia ya Mwenyeezi Mungu, na mkapata adhabu kubwa.
95. Wala msiuze ahadi ya Mwenyeezi Mungu kwa thamani ndogo kilichoko kwa Mwenyeezi Mungu ndicho bora kwenu ikiwa mnajua.
96. Mlivyonavyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyeezi Mungu ndivyo vitakavyo bakia, na bila shaka sisi tutawalipa walio subiri malipo yao sawa na matendo mazuri waliyokuwa wakiyatenda.
97. Afanyaye mema mwanamume au mwanamke hali yakuwa ni Muumini basi tutamhuisha maisha mema, na bila shaka tutawapa malipo yao kwa sababu ya matendo bora waliyokuwa wakitenda.
98. Na ukitaka kusoma Our’an basi jikinge kwa Mwenyeezi Mungu (akulinde) na shetani afukuzwaye.
99. Hakika yeye hana nguvu juu ya wale walioamini na wanaomtegemea Mola wao.
100. Nguvu yake ni juu ya wale tu wanao mfanya kiongozi na wale wanaomshirikisha (Mwenyeezi Mungu).
101. Na tunapoibadili Aya mahala pa Aya (nyingine) hali Mwenyeezi Mungu ndiye ajuaye sana anayoyateremsha, wanasema: Wewe ni mzushi tu! Bali wengi wao hawajui.
102. Sema roho takatifu ameiteremsha kutoka kwa Mola wako kwa haki, ili kuwaimarisha wale walioamini, na kuwa muongozo na khabari njema kwa wenye kunyenyekea.
103. Na bila shaka tunajua kwamba wanasema: Yuko mtu anayemfundisha Lugha ya yule wanayemuelekea ni ya kigeni na hii ni lugha ya Kiarabu chenye bayana.
104. Hakika wale wasioziamini Aya za Mwenyeezi Mungu, Mwenyeezi Mungu hawaongozi, hao watapata adhabu yenye kuumiza.
105. Wanaozua uongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyeezi Mungu, na hao ndio waongo.
106. Anayemkataa Mwenyeezi Mungu baada ya imani yake (ataadhibiwa) isipokuwa yule aliye lazimishwa hali moyo wake unatulia kwa imani, lakini anayefungua kifua kwa kufru, basi ghadhabu ya Mwenyeezi Mungu iko juu yao, na watapata adhabu kubwa.
107. Hayo ni kwa sababu wameyapenda zaidi maisha ya dunia kuliko Akhera, na kwamba Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu makafiri.
108. Hao ndio Mwenyeezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na masikio yao na macho yao, na hao ndio wenye kughafilika.
109. Hakuna shaka kwamba wao ndio wenye khasara katika Akhera.
110. Kisha hakika Mola wako kwa wale walio hama baada ya kuteswa kisha wakapigania dini na wakasubiri, bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehernu.
111. (Wakumbushe) siku ambayo kila nafsi itakuja kujitetea na kila nafsi itapewa sawa na iliyoyafanya, nao hawatadhulumiwa.
112. Na Mwenyeezi Mungu amepiga mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikaufikia kwa wingi kutoka kila mahala, lakini ukazikufuru neema za Mwenyeezi Mungu kwa hiyo Mwenyeezi Mungu akauonjesha vazi la njaa na khofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya.
113. Na aliwafikia Mtume kutoka miongoni mwao, lakini wakamkadhibisha, ndipo adhabu ikawashika hali (wamekuwa) madhalimu.
114. Basi kuleni katika vile alivyokupeni Mwenyeezi Mungu, vilivyomo halali na vizuri, na shukuruni neema ya Mwenyeezi Mungu ikiwa nyinyi mnamwabudu yeye tu.
115. Amekuharamishieni tu nyamafu na damu na nyama ya nguruwe na achinjwaye kwa jina lisilokuwa la Mwenyeezi Mungu lakini anayelazimishwa bila kuasi wala kuruka mipaka, basi hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
116. Wala msiseme, kwa sababu ya uongo usemao ndimi zenu, hii ni halali na hii ni haramu, msije mkamzulia uongo Mwenyeezi Mungu. hakika wale wamzuliao uongo Mwenyeezi Mungu hawatafaulu.
117. Ni starehe ndogo, nao watapata adhabu yenye kuumiza.
1 18. Na ambao ni Mayahudi zamani tuliwaharamishia tuliyokuhadithia, na Sisi hatukuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
119. Kisha hakika Mola wako, kwa wale waliofanya uovu kwa ujinga, kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mema, bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
120. Hakika Ibrahimu alikuwa mfano (mwema) mnyenyekevu kwa Mwenyeezi Mungu, mtu kamili, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
122. Na tukampa wema katika dunia, na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
123. Kisha tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya Ibrahimu (aliyekuwa) mtii kamili wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
124. Hakika (adhabu ya) Jumamosi iliwekwa juu ya wale waliokhitilafiana kwa ajili ya hiyo (Jumamosi) na kwa hakika Mola wako atahukumu baina yao siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana.
125. Uite (watu) kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako ndiye anamjua sana aliyepotea katika njia yake, naye ndiye awajuaye sana walio ongoka.
Aya 125
Iliposemwa: “Na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.”
TARATIBU ZITAKAZO ONGOZA MJADALA
1. Upande wowote (wasiokuwa Shia au Shia) utakaotaka mjadala, basi gharama ya maandalizi yote itakuwa ni juu yao.
2. Lazima kila upande katika pande mbili zinazojadiliana ziweke wazi itikadi zao ni zipi. Kwa mfano, Shia ajitambulishe ni Shia gani, na Sunni ni Sunni gani, Na kama si Sunni basi aweke wazi yeye ni nani?
3. Mipango ifanywe na Serikali, ya kuhifadhi amani wakati mjadala unaendelea.
4. Miadala utarekodiwa, katika kanda za Audio na Vidio na kutawanywa kote.
5. Kwa kuwa la msingi kabisa ni Uislaamu, na kwa kuwa wasiokuwa Shia wanawatuhumu Shia kwa ukafiri, ni vyema mada.hii ikawa ya kwanza kujadiliwa. Yaani; “Je, Shia ithna a’shari ni kafiri?” Ushahidi au hoja za kuthibitisha madai ya pande mbili zitoke katika Our’an au Hadithi za Mtume s.a.w au tukio la kitarekh lililothibiti.
6. Kila kikao, kitashughulika na mada maja tu.
7. Vikao vyote vitakuwa chini ya Mwenyekiti Mwislaamu, mwenye uzoefu, asiyekuwa na upendeleo wa upande wowote, na ambaye pande zote mbili zitamkubali.
8. Mwenyekiti atasaidiwa na watu wawili ambao kila mmoja atateuliwa na upande wake katika pande mbili zinazojadiliana, na ambao pande zote mbili zitawakubali.
9. Mjadala ufanywe ndani ya ukumbi utakaokubaliwa na pande zote mbili, hii ni kudhibiti nidhamu na kuepuka vurugu.
10. Ni lazima kwa kila upande kuleta vitabu vyao ambavyo ndani yake mna hizo hoja/dalili wazitegemeazo wao wenyewe. Ili upande wa pili ukitaka kuthibitisha hoja hizo, watapewa vitabu hivyo, na kuhoji.
11. Kila upande uruhusiwe kualika idadi ya watakao hudhuria sawa na ile ya upande wa pili, kulingana na jumla ya watu wanaoweza kuingia katika ukumbi huo.
12. Kwa wale ambao hawataruhusiwa kuingia ukumbini, mipango itaandaliwa ya kuwawezesha kufuatilia yanayoendelea ndani ya ukumbi, kwa kutumia vipaza sauti.
13. Kila upande utawakilishwa na msemaji mmoja tu, atakayeteuliwa na upande wake. Hata hivyo, kila msemaji atakuwa na haki ya kuteua wasaidizi/ washauri ambao hawatazungumza chochote. Na idadi yao ni sawa kwa kila upande, ambao watakubaliwa na pande zote mbili.
14. Mtoa hoja apewe saa moja kamili kuisemea hoja yake. Baada ya hapo, mpinga hoja naye apewe saa moja kamili kujibu. Kisha mtoa hoja apewe nusu saa kujibu. Halafu, kwa muda wa dakika (45) waliohudhuria waachiwe nafasi kupitia kwa Mwenyekiti ya kuwauliza maswali wasemaji kwa maandishi.
15. Mjadala uendeshwe kwa Kiswahili, na kwa lugha ya kielimu, isiyo na kejeli, ufidhuli wala matusi.
16. Waliohudhuria, wasiruhusiwe kushangilia upande wao, wala kuzomea upande wa pili.
17. Kama wasemaji wa pande zote mbili watakuwa ni watu wa kutoka nchi moja, basi mjadala ufanywe katika nchi yao. Kama watakuwa ni watu wa nchi mbili, basi mjadala ufanywe katika moja wapo ya nchi mbili hizo.
18. Taratibu hizi lazima zifuatwe kama zilivyoelekeza, na yeyote atakayekiuka taratibu hizi basi, Mwenyekiti atatumia madaraka yake ya kumnyamazisha muhusika asiseme tena katika kikao hicho. Kwa siku hiyo mjadala utafungwa, mpaka tarehe itakayotajwa kwa kukubaliana na pande zote mbili.
19. Kwa kutumia taratibu zote zilizotajwa katika waraka huu, na ili ithibiti kwamba pande zote mbili zimekubali kutimiza masharti yote yaliyotajwa ndani ya waraka huu, lazima kila upande usaini hapa:-
Jina kamili na sahihi ya msemaji wa upande wa Shia.
Jina kamili na sahihi ya msemaji wa upande wa anayepinga Shia.
Jina kamili na sahihi ya Mwenyekiti.
126. Na mkilipiza, basi lipizeni sawa na vile mlivyoonewa, na kama mkisubiri, hakika huo ni ubora kwa wanaosubiri.
127. Na subiri, na kusubiri kwako kusiwe ila kwa sababu ya Mwenyeezi Mungu tu, wala usihuzunike kwa ajili yao, wala usiwe katika dhiki kwa sababu ya vitimbi wanavyovifanya.
128. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu yu pamoja na wale wanaomcha, na wale wenye kufanya wema.