Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 50
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Naapa kwa (pepo) zinazopelekwa kwa upole.
2. Na kwa (pepo) zinazovuma kwa kasi.
3. Tena kwa (pepo) zinazopeperusha (mawingu) mpeperusho.
4. Na zinafarikisha mbali mbali.
5. Tena kwa (Malaika) wanaopeleka mawaidha.
6. Kuondoa udhuru au kuhadharisha.
7. Kwa hakika mnayoahidiwa bila shaka yatatokea.
8. Basi nyota zitakapofutwa (nuru zake).
9. Na mbingu zitakapopasuliwa.
10. Na milima itakaposagwasagwa.
11. Na Mitume watakapokusanywa.
12. Kwa siku gani wamewekewa muda?
13. Siku ya hukumu.
14. Na nini kitakachojulisha siku ya hukumu ni nini?
15. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
16. Je, hatukuwaangamiza (watu) wa zamani?
17. Kisha tukawafuatishia (watu) wengine.
18. Hivyo ndivyo tutakavyowafanya waovu.
19. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
20. Je, hatukukuumbeni kwa maji yaliyo dhalili?
21. Kisha tukayaweka mahala pa utulivu.
22. Mpaka muda maalum.
23. Na tukakadiria, nasi ni wazuri kabisa wa kukadiria.
24. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
25. Je, sisi hatukuifanya ardhi yenye kukusanya.
26. Wazima na Wafu?
27. Na ndani yake tukaweka milima mirefu na tumekunywesheni maji matamu.
28. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
29. Nendeni kwenye yale mliyokuwa mkikadhibisha.
30. Nendeni kwenye kivuli chenye matawi matatu.
31. Hayatoi kivuli chenye matawi matatu.
32. Hakika huo Moto hutoa macheche yaliyo kama majumba.
33. Kama kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano.
34. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
35. Hii ni siku ambayo hawatazungumza.
36. Wala hawatapewa ruhusa kutoa udhuru.
37. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
38. Hii ni siku ya hukumu tumekukusanyeni nyinyi na waliotangulia.
39. Basi ikiwa mnayo hila ifanyeni juu yangu.
40. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
41. Bila shaka wamchao (Mwenyeezi Mungu) watakuwa katika vivuli na chem chem.
42. Na matunda wanayoyapenda.
43. Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa sababu ya yale mliyokuwa mkitenda.
44. Hakika sisi ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
45. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
46. Kuleni na mjifurahishe kidogo, hakika nyinyi ni waovu.
47. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
48. Na ikisemwa kwao: Inameni (abuduni) hawainami.
49. Ole wao siku hiyo wanaokadhibisha.
50. Bali hadithi gani baada ya hii wataiamini?