Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 85
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Haa Mym.
2. Kuteremshwa kwa Kitabu kunatokana na Mwenyeezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye ujuzi.
3. Mwenye kusamehe madhambi na Mwenye kupokea toba, Mkali wa kuadhibu, Mwenye ukarimu, hakuna aabudiwaye ila yeye tu, marejeo ni kwake.
4. Habishani katika Aya za Mwenyeezi Mungu ila wale waliokufuru, basi kusikudanganye kutembea kwao mijini.
5. Watu wa Nuhu walikadhibisha kabla yao na makundi (mengine) baada yao na kila taifa liliazimia juu ya Mtume wao ili wamkamate, na walibishana kwa ubatili ili kupoteza haki, kwa hiyo niliwakamata, basi ilikuwaje adhabu yangu!
6. Na hivyo ndivyo lilivyotumia neno la Mola wako juu ya wale waliokufuru kwamba wao ni watu wa Motoni.
7. Wale wanaokichukua kiti cha Enzi na wale wanaokizunguka, wanatukuza kwa kumsifu Mola wao, na wanamwamini na wanaowaombea samahani walioamini. Mola wetu! umekienea kila kitu kwa rehema na elimu, basi wasamehe waliotubu na wakaifuata njia yako na waepushe na adhabu ya Jahannam.
8. Mola wetu! na uwaingize katika Bustani za milele ulizo waahidi, na pia waliofanya mema miongoni mwa baba zao na wake zao na watoto wao, bila shaka wewe ndiye Mwenye nguvu Mwenye hekima.
9. Na uwaepushe na maovu, naye umuepushaye na maovu siku hiyo hakika umemrehemu, na huko ndiko kufaulu kukubwa.
10. Kwa hakika wale waliokufuru watanadiwa: Bila shaka chuki ya Mwenyeezi Mungu ni kubwa kuliko chuki mnayojichukia wenyewe. (kumbukeni) mlipoitwa kwenye imani lakini mkakataa.
11. Watasema: Mola wetu! umetufisha mara mbili na umetuhuisha mara mbili, basi tunakiri dhambi zetu, lakini je, iko njia ya kutoka?
12. Hayo ni kwa sababu ya kuwa alipoombwa Mwenyeezi Mungu peke yake mlikataa, na aliposhirikishwa mkaamini, basi hukumu ni yake Mwenyeezi Mungu Mtukufu, Mkuu.
13. Yeye ndiye anayekuonyesheni Miujiza yakc na kukuteremshieni riziki kutoka mbinguni, na hapana anayekumbuka ila anayerejea.
14. Basi muombeni Mwenyeezi Mungu mkimtakasia yeye ibada, ingawa makafiri watachukia.
15. Mwenye vyeo vya juu, Mwenyeezi Mungu, hupeleka Wahyi kwa amri yake kwa amtakaye miongoni mwa waja wake ili kuonya siku ya kukutana.
16. Siku watakayotoka haitafichika khabari yao yoyote kwa Mwenyeezi Mungu. Leo ufalme ni wa nani? ni wa Mwenyeezi Mungu Mmoja, Mwenye nguvu.
17. Leo kila mtu atapewa malipo ya yale aliyoyatenda, hakuna dhulma leo, bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.
18. Na waonye siku (ya Kiyama) iliyo karibu wakati nyoyo zitakapofika kooni, wamejaa huzuni, madhalimu hawatakuwa na rafiki wala muombezi atiiwaye.
19. (Mwenyeezi Mungu) anajua hiyana ya macho na yanayoficha vifua.
20. Na Mwenyeezi Mungu huhukumu kwa haki, na wale wanaowaomba kinyume cha Mwenyeezi Mungu hawahukumu chochote, kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
21. Je, hawakusafiri katika nchi wakaona jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Wao walikuwa wenye nguvu zaidi na athari katika ardhi kuliko hao, lakini Mwenyeezi Mungu aliwaadhibu kwa sababu ya makosa yao, wala hapakuwa na wakuwalinda na Mwenyeezi Mungu.
22, Hayo ni kwa sababu walikuwa wanawafikia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, lakini wakawakataa, ndipo Mwenyeezi Mungu akawaadhibu, bila shaka yeye ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu.
23. Na kwa hakika tulimtuma Musa pamoja na Miujiza yetu na hoja zilizo dhahiri.
24. Kwa Firaun na Hamana na Karuni, lakini wakasema: (Huyu ni) mchawi, muongo mkubwa.
25. Basi alipowaletea haki kutoka kwetu wakasema: Wauweni watoto wanaume na wale walioamini pamoja naye na waacheni hai wanawake wao, na hila ya makafiri haiwi ila katika upotovu.
26. Na akasema Firaun. Niacheni nimuue Musa, naye amwite Mola wake! Hakika ninachelea asije kuiharibu dini yenu au kuleta matata katika nchi.
27. Na Musa akasema: Hakika najikinga kwa Mola wangu na Mola wenu anilinde na kila mwenye kiburi, asiyeamini siku ya Hesabu.
28. Na akasema mtu Muumini aliyekuwa mmoja wa watu wa Firaun anayeficha imani yake; je, mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Mwenyeezi Mungu? Na kwa hakika yeye amekuleteeni dalili za wazi wazi zitokazo kwa Mola wenu, naye akiwa muongo, basi uongo wake ni juu yake, na kama akiwa mkweli, yatakufikieni baadhi ya hayo anayo kuahidini. Bila shaka Mwenyeezi Mungu hamuongozi yule apitaye kiasi, muongo mkubwa.
29. Enyi watu wangu! Leo ufalme ni wenu, mmeshinda katika ardhi, basi ni nani atakayetusaidia katika adhabu ya Mwenyeezi Mungu kama ikitufikia? Firaun akasema: Sikupeni shauri ila ile niliyoiona, wala sikuongozeni ila kwenye njia ya uongofu.
30. Na yule aliyeamini akasema: Enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni mfano wa siku ya makundi.
31. Mfano wa hali ya watu wa Nuhu na A’di na Thamudi na wale waliokuwa nyuma yao, na Mwenyeezi Mungu hataki dhulma kwa watu.
32. Na enyi watu wangu! kwa hakika nakukhofieni siku ya kuitana.
33. Siku mtakapogeuka kurudi nyuma, hamtakuwa na mlinzi kwa Mwenyeezi Mungu, basi huyo hana wa kumuongoza.
34. Na bila shaka zamani alikufikieni Yusufu kwa dalili zilizo wazi, lakini nyinyi mliendelea katika shaka kwa yale aliyokuleteeni, mpaka alipofariki mkasema: Mwenyeezi Mungu hataleta kabisa Mtume baada yake. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu humpoteza yule aliyepita kiasi mwenye shaka.
35. Ambao wanajadiliana katika Aya za Mwenyeezi Mungu pasipo dalili yoyote iliyowafikia, ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyeezi Mungu na mbele ya wale walioamini, hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyopiga muhuri juu ya kila moyo wa jeuri, ajitukuzaye.
36. Na Firaun akasema: Ewe Hamana! unijengee mnara ili nipate kuzifikia njia.
37. Njia za mbinguni ili nimuone Mungu wa Musa, na kwa hakika ninamjua kuwa ni muongo tu. Na hivyo ndivyo Firaun akapambiwa ubaya wa vitendo vyake na akazuiliwa njia (ya haki) Lakini hila ya Firaun haikuwa ila katika kuangamia.
38. Na yule aliyeamini alisema: Enyi watu wangu! nifuateni, nitakuongozeni njia ya uongofu.
39. Enyi watu wangu! kwa hakika maisha ya dunia hii ni starehe (ipitayo) na bila shaka Akhera ndiyo nyumba ya kukaa.
40. Afanyanye ubaya hatalipwa ila sawa na huo, na afanyae wema, akiwa mwanamume au mwanamke naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, wataruzukiwa humo bila ya hesabu.
41. Na enyi watu wangu! mimi nina nini nakuiteni kwenye uokofu, nanyi mnaniita kwenye Moto!
42. Mnaniita nimkufuru Mwenyeezi Mungu na kumshirikisha na yule ambaye simjui, nami nakuiteni kwa Mwenye nguvu, Mwingi wa kusamehe.
43. Bila shaka nyinyi mnaniita kwa yule ambaye hana wito duniani wala katika Akhera, na marudio yetu ni kwa Mwenyeezi Mungu na wapitao kiasi hao ndio watu wa Motoni.
44. Basi mtayakumbuka ninayokuambieni nami ninamkabidhi Mwenyeezi Mungu jambo langu, hakika Mwenyeezi Mungu ndiye awaonaye waja (wake).
45. Na Mwenyeezi Mungu akamlinda katika ubaya wa hila walizofanya, na adhabu kali zaidi.
46. Ni Moto! wanawekewa asubuhi na jioni. Na siku kitakapotokea Kiyama (kutasemwa) waingizeni watu wa Firaun katika adhabu kali zaidi.
47. Na watakapobishana katika Moto huo kisha wadhaifu watawaambia wale waliojikuza: Kwa hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi je, mnaweza kutuondolea (hata) sehemu ya Moto?
48. Watasema waliojikuza: Sisi sote tumo humo, hakika Mwenyeezi Mungu amekwisha hukumu baina ya watu.
49. Na wale waliomo Motoni watawaambia walinzi wa Jahannam: Muombeni Mola wenu atupunguzie siku moja ya adhabu.
50. Watasema; Je hawakuwa wakikufikieni Mitume wenu kwa hoja zilizo wazi? watasema: Kwa nini! watasema: Basi ombeni (wenyewe) lakini maombi ya makafiri hayawi ila kupotea bure.
51. Bila shaka sisi tunawasaidia Mitume wetu na wale walioamini katika maisha ya dunia na siku watakaposimama mashahidi.
52. Siku ambayo hautawafaa madhalimu udhuru wao na watapata laana mahala pao patakuwa pabaya.
53. Na kwa hakika tulimpa Musa muongozo na tukawarithisha wana wa Israeli Kitabu.
54. (Kilichokuwa) muongozo na ukumbusho wa wenye akili.
55. Basi subiri, bila shaka ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni kweli, na uombe msamaha kwa dhambi zako, na umtukuze Mola wako kwa kumsifu jioni na asubuhi.
56. Kwa hakika wale wanaobishana katika Aya za Mwenyeezi Mungu pasipo dalili yoyote iliyowafikia, hamna nyoyoni mwao ila kiburi, lakini hawataufikia, basi jikinge kwa Mwenyeezi Mungu, kwa hakika yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
57. Kwa hakika umbo la mbingu na ardhi ni kubwa kuliko umbo la wanadamu, lakini watu wengi hawajui,
58. Na kipofu na mwenye macho hawawi sawa, na wale walioamini na kufanya wema hawawi sawa na afanyaye maovu, mnayoyakumbuka ni kidogo.
59. Kwa hakika Kiyama kitafika, nacho hakina shaka, lakini watu wengi hawaamini.
60. Na Mola wenu husema: Niombeni nitakujibuni. Kwa hakika wale wajivunao kufanya ibada yangu, wataingia Jahannam wakifedheheka.
61. Mwenyeezi Mungu ndiye alikufanyieni usiku ili mtulie humo, na mchana wenye nuru, hakika Mwenyeezi Mungu ndiye huwafadhili watu, lakini watu wengi hawashukuru.
62. Mungu huyo ndiye Mola wenu, Muumba wa kila kitu hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, basi mnageuzwa wapi?
63. Hivyo ndivyo walivyogeuzwa wale waliokuwa wakizikataa Aya za Mwenyeezi Mungu.
64. Mwenyeezi Mungu ndiye aliyekufanyieni ardhi mahala pa kukaaa, na mbingu kuwa dari, na akakutieni sura na akazifanya nzuri sura zenu na akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndiye Mungu, Mola wenu, basi Mwenye baraka ni Mwenyeezi Mungu, Mola wa walimwengu.
65. Yeye ndiye aliye Hai, hakuna aabudiwaye ila Yeye tu kwa hiyo muombeni mkimtakasia utii, kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu. Mola wa walimwengu.
66. Sema: Hakika nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu ziliponifikia dalili zilizo wazi kutoka kwa Molawangu, na nimeamrishwa nimnyenyekee Mola wa walimwengu.
67. Yeye ndiye aliyekuumbeni kwa udongo, kisha kwa manii, kisha kwa pande la damu, halafu akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga, kisha (akakuacheni) ili mpate nguvu zenu kamili, kisha muwe wazee, na wengine wenu hufishwa kabla (ya uzee) na ili mfikie muda uliowekwa, na ili mpate kufahamu.
68. Yeye ndiye anayehuisha na kufisha na anapolihukumia jambo lolote, basi huliambia: Kuwa, nalo likawa.
69. Je, huwaoni wale wanaobishana katika Aya za Mwenyeezi Mungu, wanageuziwa wapi?
70. Ambao wamekadhibisha Kitabu na yale tuliyowatuma nayo Mitume wetu, lakini karibuni watajua.
71. Zitakapokuwa pingu shingoni mwao na minyororo watabururwa.
72. Katika maji ya moto, kisha wataunguzwa Motoni.
73. Tena wataambiwa: Wako wapi mliokuwa mkiwashirikisha.
74. Badala ya Mwenyeezi Mungu? Watasema wametupotea, bali toka zamani hatukuwa tunaabudu chochote. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu huwapoteza makafiri
75. Hayo ni kwa sababu mlikuwa mkifurahi katika ardhi pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa. mkijivuna.
76. Ingieni milangoni mwa Jahannam mkakae humo milele, basi ni mabaya yalioje makazi ya wanaotakabari.
77. Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni kweli, na kama tukikuonyesha baadhi ya wale tuliyowaahidi au tukikufisha. basi watarudishwa kwetu.
78. Na kwa hakika tuliwatuma Mitume kabla yako, wengine wao tumekusimulia na wengine wao hatukukusimulia, na haikuwa kwa Mtume yeyote kuleta Muujiza, wowote ila kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu. Na itakapofika hukumu ya Mwenyeezi Mungu itahukumiwa kwa haki na wafanyao mambo ya batili hapo watapata khasara.
79. Mwenyeezi Mungu ndiye aliyekufanyieni wanyama ili muwapande baadhi yao na wengine wao mpate kuwala.
80. Na katika hao mnayo manufaa, na mnapata kwao haja zilizomo vifuani mwenu, na mnachukuliwa juu yao, na juu ya jahazi.
81. Naye anakuonyesheni dalili zake, basi mtakataa ipi katika dalili za Mwenyeezi Mungu?
82. Je, hawajasafiri katika ardhi wakaona umekuwaje mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? wao walikuwa wengi kuliko hao na zaidi katika nguvu na katika majengo ardhini, lakini hayakuwafaa yale waliyoyachuma.
83. Basi walipowafikia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi wakafurahia elimu waliyokuwa nayo, na yakawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia maskhara.
84. Lakini walipoiona adhabu yetu wakasema: Tunamwamini Mwenveezi Mungu pekee na tunawakataa (waungu)tuliokuwa tukiwashirikisha naye.
85. Lakini imani yao haikuwa yenye kuwafaa walipoiona adhabu yetu, hii ni kawaida ya Mwenyeezi Mungu iliyopita katika waja wake na hapo waliokufuru watapata khasara.