Sura hii imeteremshwa Makka, ina Aya 118
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Hakika wamefuzu wenye kuamini.
2. Ambao ni wanyenyekevu katika swala zao.
3. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi.
4. Na ambao wanatoa zaka.
5. Na ambao wanazilinda tupu zao.
6. Isipokuwa kwa wake zao au kwa (wanawake) wale waliomilikiwa na mikono yao basi hao si wenye kulaumiwa.
7. Lakini anayetaka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.
8. Na ambao kwa amana zao na ahadi zao ni wenye kuzitekeleza.
9. Na ambao swala zao wanazihifadhi.
10. Hao ndio warithi.
11. Ambao watairithi Pepo ya Firdaus, wao humo watakaa milele.
12. Na bila shaka tulimuumba mwanadamu kutokana na asli ya udongo.
13. Kisha tukamuumba kwa tone la manii, lililowekwa katika makao yaliyohifadhika.
14. Kisha tuliumba tone hilo kuwa pande la damu, na tukalifanya pande la damu hilo kuwa pande la nyama, kisha tulifanya pande la nyama hilo kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama, kisha tukamfanya kiumbe kingine. Basi ametukuka Mwenyeezi Mungu Mbora wa waumbaji.
15. Kisha hakika nyinyi baada ya hayo ni wenye kufa.
16. Kisha hakika nyinyi siku ya Kiyama mtafufuliwa.
17. Na bila shaka tuliziumba juu yenu njia saba, nasi katika kuumba si wenye kughafilika.
18. Na tumeteremsha kutoka mawinguni maji kwa kiasi, na tukayatuliza ardhini, na hakika sisi ni wenye uwezo wa kuyaondoa.
19. Basi kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula.
20. Na mti utokao katika mlima wa sinai, unaotoa mafuta na kitoweo kwa walao.
21. Na hakika mnayo mazingatio (makubwa) katika wanyama, tunakunywesheni katika vile vilivyomo matumboni mwao, na mnapata katika hao manufaa mengi, na baadhi yao mnawala.
22. Najuu yao na juu ya majahazi mnabebwa.
23. Na bila shaka tulimtuma Nuhu kwa watu wake, na akasema: Enyi watu wangu! mwabuduni Mwenyeezi Mungu hamna mungu isipokuwaYeye, basi je, hamuogopi?
24. (Lakini) wakasema wakuu wa wale waliokufuru katika watu wake: Siye huyu ila ni mtu kama nyinyi, anataka kujipatia ubora juu yenu, na kama Mwenyeezi Mungu angependa lazima angeteremsha Malaika hatukusikia haya kwa baba zetu wa kwanza.
25. Huyu siye ila ni mtu mwenye wazimu, basi mngojeeni kwa muda.
26. (Nuhu) akasema: Mola wangu! nisaidie kwa sababu wamenikadhibisha.
27. Basi tulimletea Wahyi kwamba: Unda jahazi mbele ya macho yetu na sawa na Wahyi wetu. Basi itakapofika amri yetu na chemchem ya maji ikabubujika hapo uwaingize ndani yake wa kila namna, dume na jike na watu wako, ila ambaye kauli imepita wala usinitajie hao waliodhulumu bila shaka wao watagharikishwa.
28. Na utakapotulia wewe na walio pamoja nawe jahazini, basi useme: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu ambaye ametuokoa katika watu madhalimu.
29. Na Useme: Mola wangu! uniteremshe mteremsho wenye baraka, maana wewe ni mbora wa wateremshaji.
30. Bila shaka katika hayo mna mazingatio na kwa hakika, Sisi ni wenye kukufanyieni mtihani.
31. Kisha tuliumba baada yao kizazi kingine.
32. Na tukawapelekea Mtume kutoka miongoni mwao, (akawaambia):
Muabuduni Mwenyeezi Mungu, hamna mungu isipokuwa Yeye, je hamuogopi?
33. Na wakasema wakubwa katika watu wake waliokufuru na kukadhibisha mkutano wa Akhera, na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, huyu siye ila ni mtu kama nyinyi, anakula katika vile mnavyokula na anakunywa katika vile mnavyokunywa.
34. Na kama mkimtii mtu kama nyinyi kwa hakika hapo mtakuwa wenye kupata khasara.
35. Je, anakuahidini kuwa mtakapokufa na mkawa mchanga na mifupa, hakika mtatolewa.
36. Hayawi, hayawi hayo mnayoahidiwa.
37. Hakuna ila maisha yetu ya dunia tunakufa na tunaishi, wala sisi si wenye kufufuliwa.
38. Huyu siye ila ni mtu anayemzulia Mwenyeezi Mungu uongo, wala sisi si wenye kuamini.
39. Akasema: Mola wangu nisaidie kwa sababu wamenikadhibisha.
40. Akasema: Baada ya muda kidogo, lazima watakuwa wenye kujuta.
41. Basi ukawanyakua ukelele kwa haki, na tukawafanya kuwa takataka basi maangamio yaliwathibitikia watu madhalimu.
42. Kisha tukaviumba baada yao vizazi. Vingine.
43. Hapana taifa liwezalo kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.
44. Kisha tukawatumia Mitume wetu mmoja baada ya mmoja. Kila mara alipowafikia watu Mtume wao walimkadhibisha, hivyo tukawaandamanisha baadhi yao wengine, na tukawafanya kuwa visa, basi maangamio kwa watu wasioamini.
45. Kisha tulimtuma Musa na nduguye Harun pamoja na Miujiza yetu na dalili zilizo dhahiri.
46. Kwa Firaun na wakuu wake, lakini wakajivuna, nao walikuwa watu jeuri.
47. Na wakasema: Je, tuwaamini watu wawili walio mfano wetu na watu wao ni watumwa wetu?
48. Basi wakawakadhibisha na wakawa miongoni mwa walioangamizwa.
49. Na bila shaka tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.
50. Na tulimfanya mwana wa Mariam na mama yake kuwa Muujiza, na tukawapa makimbilio mahala palipoinuka penye utulivu na chem chem.
51. Enyi Mitume! kuleni katika vitu vizuri na fanyeni mema, hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayoyatenda.
52. Na kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu, basi niogopeni.
53. Lakini walikatiana jambo lao baina yao sehemu mbali mbali kila kundi likifurahia waliyo nayo.
54, Basi waache katika ujinga wao kwa muda.
55. Je, wanadhani kuwa tunawasaidia kwa mali na watoto.
56. Tunawaharakishia katika mambo ya kheri? Lakini hawatambui.
57. Kwa hakika hao ambao kwa kumuogopa Mola wao wananyenyekea.
58. Na hao ambao Aya za Mola wao wanaziamini.
59. Na hao arnbao Mola wao hawamshirikishi.
60. Na ambao wanatoa walichopewa na hali nyoyo zao zinaogopa kwamba watarejea kwa Mola wao.
61. Hao ndio wafanyao haraka katika mambo ya kheri, na ndio waendao mbele katika hayo.
62. Nasi hatuikalifishi nafsi ila uwezo wake, na tunalo daftari lisemalo kweli, nao hawatadhulumiwa.
63. Lakini nyoyo zao zimeghafilika na hayo, na wanavyo vitendo wanavyovitenda visivyo kuwa hivyo.
64. Hata tutakapowatia katika adhabu wale waliodekezwa kwa starehe kati yao, hapo ndipo watakapo lalama.
65. Msilalame leo, bila shaka nyinyi hamtanusurika nasi.
66. Hakika zilikuwa Aya zangu zikisomwa kwenu, lakini mlikuwa mkirudi nyuma kwa visigino vyenu.
67. Mkitakabari, mkiizungumza usiku (Qur-an) kwa dharau.
68. Je, hawakuifikiri kauli au yamewafikia yasiyowafikia baba zao wa kwanza?
69. Au hawakumjua Mtume wao kwa hiyo wanamkataa?
70. Au wanasema (Muhammad) ni mwenye wazimu? Bali amewafikia kwa haki, na wengi wanaichukia haki.
7l. Na kama haki ingelifuata matamanio yao, zingeliharibika mbingu na ardhi na vilivyomo. Lakini tumewaletea ukumbusho wao, nao walijitenga mbali na ukumbusho wao.
72. Au unawaomba malipo? Lakini malipo ya Mola wako ni bora, nayeni Mbora wa wanaoruzuku.
73. Na kwa hakika wewe unawaita kwenye njia iliyonyooka.
74. Na hakika wale wasioiamini Akhera wanajitenga na njia hiyo.
75. Na Lau tukiwarehemu na kuwaondolea shida waliyonayo bila shaka wataendelea katika upotovu wao wakihangaika.
76. Na hakika tuliwatia adhabu kali, lakini hawakuelekea kwa Mola wao wala hawakunyenyekea.
77. Mpaka tulipowafungulia mlango wa adhabu kali, ndipo wakawa wenye kukata tamaa.
78. Na yeye ndiye aliyekuumbieni kusikia na kuona na nyoyo, ni machache mnayoyashukuru.
79. Naye ndiye aliyekuenezeni katika ardhi, na kwake mtakusanywa.
80. Na yeye ndiye anayehuisha na kufisha, na ni yake mabadiliko ya usiku na mchana, basi je hamfahamu?
81. Bali walisema kama walivyosema (watu) wa kwanza.
82. Walisema: Je, tukifa na tukawa udongo na mifupa, je, tutafufuliwa?
83. Bila shaka tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani, hayakuwa haya ila ni visa vya (watu) wa zamani.
84. Sema: Ni ya nani ardhi na vilivyomo kama nyinyi mnajua.
85. Watasema; Ni ya Mwenyeezi Mungu! Sema basi je, hamkumbuki?
86. Sema: Ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa Arshi kuu?
87. Watasema: Ni vya Mwenyeezi Mungu! Sema: Basi je, hamuogopi?
88. Sema: Ni nani mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu naye ndiye alindaye, na hakilindwi (chochote) kinyume naye kama mnajua?
89. Watasema: Ni wa Mwenyeezi Mungu, sema: Basi vipi mnadanganywa?
90. Bali tumewaletea haki, na kwa hakika wao ndio waongo.
91. Mwenyeezi Mungu hakujipatishia mtoto wala hakuwa pamoja naye mungu (mwingine) hapo kila mungu angeliwachukua aliowaumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengine, Mwenyeezi Mungu ameepukana na sifa wanazomsifu.
92. Mjuzi wa siri na dhahiri na aliye juu kuliko wanayomshirikisha nayo.
93. Sema: Mola wangu! ukinionyesha waliyoahidiwa.
94. Mola wangu! usinijaalie katika watu madhalimu.
95. Na hakika sisi kwa kukuonyesha tuliyowaahidi ni waweza.
96. Ondosha mabaya kwa mema, sisi tunajua wanayoyasema.
97. Na sema: Mola wangu! najikinga kwako na wasiwasi wa mashetani.
98. Na najikinga kwako Mola wangu! wasinikaribie.
99. Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti husema: Mola wangu! nirudishe.
100. Ili nifanye mema katika yale niliyoyaacha. Hapana, hakika hili ni neno tu analolisema, na mbele yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa.
101. Basi litakapopulizwa parapanda, hapo hautakuwapo ujamaa baina yao siku hiyo, wala hawataulizana.
102. Ama yule mizani yake itakayokuwa nzito, basi hao ndio wenye kufaulu.
103. Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, basi hao ndio waliozitia hasarani nafsi zao, katika Jahannam watakaa milele.
104. Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa humo wenye kukunjana.
105. Je, Aya zangu hazikuwa mkisomewa, na nyinyi mkizikadhibisha?
106. Watasema? Mola wetu! tulizidiwa na ubaya wetu na tukawa watu wenye kupotea.
107. Mola wetu! tutoe humo, na tufanyapo tena bila shaka tutakuwa madhalimu.
108. Atasema: Nyamazeni humo wala msinisemeshe.
109. Bila shaka kulikuwa na kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu! tumeamini basi tusamehe na turehemu nawe ndiye mbora wa wanaorehemu.
110. Lakini nyinyi mliwafanyia kejeli hata wakakusahaulisheni kunikumbuka, na mlikuwa mkiwacheka.
111. Hakika leo nimewalipa kwa sababu walisubiri, bila shaka hao ndio wenye kufuzu.
112. Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hesabu ya miaka?
113. Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku basi waulize wafanyao hesabu.
114. Atasema: Nyinyi hamkukaa ila kidogo, laiti mngelikuwa mmejua.
115. Je, mlidhani kwamba tumekuumbeni bure na kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?
116. Basi ametukuka Mwenyeezi Mungu, Mfalme wa haki, hakuna aabudiwaye ila yeye tu, Mola wa Arshi yenye heshima.
117. Na anayemwabudu pamoja na Mwenyeezi Mungu mwingine, hana ushahidi wa hili basi bila shaka hesabu yake iko kwa Mola wake, kwa hakika makafiri hawafanikiwi.
118. Na sema: Mola wangu! samehe na rehemu, nawe ndiye Mbora wa wanaorehemu.