Sura hii imeteremshwa Makka, Aya 30
Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Ametukuka yule ambaye mkononi mwake umo ufalme, naye ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
2. Ambaye ameumba kifo na uzima ili kukujaribuni, ni nani miongoni mwenu aliye na vitendo vizuri zaidi, naye ni Mwenye nguvu, Mwingi wa kusamehe.
3. Ambaye ameumba mbingu saba zilizo tabaka tabaka, huoni tofauti yoyote katika uumbaji wa Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema, basi rudisha macho, je unaona kosa?
4. Tena rudisha macho mara kwa mara, mtazamo wako utarudia hali ya mahangaiko na mchoko.
5. Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa na tumeyafanya ili kupiga mashetani, na tumewawekea tayari adhabu ya Moto uwakao.
6. Na kwa waliomkufuru Mola wao iko adhabu ya Jahannam na ni marejeo mabaya mno!
7. Watakapotupwa humo watasikia mngurumo wake nao unafoka.
8. Unakaribia kupasuka kwa hasira kila mara kundi litakapotupwa humo walinzi wake watawauliza; Je, hakuwafikieni Muonyaji?
9. Watasema: Kwa nini, alitufikia muonyaii lakini tulikadhibisha na tulisema: Mwenyeezi Mungu hakuteremsha chochote nyinyi hammo ila katika upotovu mkubwa.
10. Na watasema: Kama tungelisikia au tungelikuwa na akili hatungekuwa katika watu wa Motoni.
11. Na watakiri dhambi zao, basi kuangamia kumewastahiki watu wa Motoni.
12. Hakika wale wanaomuogopa Mola wao kwa siri wao watapata msamaha na malipo makubwa.
13. Na ficheni kauli yenu au idhihirisheni hakika yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
14. Je, asijue aliyeumba? naye ndiye aonaye visivyoonekana Mwenye khabari.
15. Yeye ndiye aliyefanya ardhi laini kwa ajili yenu, basi nendeni katika pande zake na kuleni katika nziki zake, na kwake ndio marejeo.
16. Je, mnadhani mko salama kwa alioko mbinguni ya kuwa yeye hatakudidimizeni ardhini, na huku inataharaki.
17. Au je, mnadhani mko salama kwa alioko mbinguni kuwa yeye hatakuleteeni kimbunga chenye changarawe? basi karibuni mtajua lilivyo onyo langu.
18. Na bila shaka wamekwisha kadhibisha wale wa kabla yao, basi lilikuwaje kasiriko langu?
19. Je, hawaoni ndege walioko juu yao wakizinyoosha (mbawa zao) na kuzikunja? Hakuna awashikiliaye ila Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema, hakika yeye anaona kila kitu.
20. Au ni lipi hilo jeshi lenu liwezalo kukunusuruni pasipo Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema? Hawako makafiri ila katika udanganyifu.
21. Au ni nani ambaye atakupeni riziki kama akizuia riziki zake? bali wanaendelea katika uasi na chuki.
22. Je anayekwenda kifudifudi kwa uso wake ni mwongofu zaidi au anayekwenda sawasawa katika njia iliyonyooka.
23. Sema: Yeye ndiye aliyekuumbeni na akakupeni masikio na macho na nyoyo, kidogo tu mnayoshukuru.
24. Sema: Yeye ndiye aliyekutawanyeni katika ardhi, na kwake mtakusanywa.
25. Nao husema: Lini (itatimizwa) ahadi hii ikiwa mnasema kweli?
26. Sema: Kwa hakika elimu iko kwa Mwenyeezi Mungu na hakika Mimi ni Muonyaji tu abainishaye.
27. Lakini watakapoiona karibu, nyuso za waliokufuru zitahuzunika, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyokuwa mkiyaomba.
28. Sema: Niambieni kama Mwenyeezi Mungu akiniangamiza mimi na walio pamoja nami, au akiturehemu, basi ni nani atakayewalinda makafiri katika adhabu yenye kuumiza?
29. Sema: Yeye ndiye Mwenye huruma tunamwamini yeye, na kwake tunaiegemea na karibuni mtajua ni nani aliye katika upotovu dhahiri.
30. Sema: Mnaonaje, kama maji yenu yakiwa yamezama, basi nani atakuleteeni maji safi yenye kutiririka?