Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 56
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Ewe uliyevaa.
2. Simama na uonye.
3. Na Mola wako umtukuze.
4. Na nguo zako uzisafishe.
5. Na uchafu uondoe.
6. Wala usiwafanyie ihsani ili upate zaidi.
7. Na kwa ajili ya Mola wako fanya subira.
8. Basi itakapopigwa parapanda.
9. Basi siku hiyo itakuwa siku ngumu.
10. Kwa makafiri haitakuwa nyepesi.
11. Niache mimi na niliyemuumba peke yangu.
12. Na nikampa mali nyingi.
13. Na watoto waonekanao.
14. Na nikampangia mpango.
15. Kisha anatumaini nizidishe.
16. Siyo, hakika yeye alikuwa adui ya Aya zetu.
17. Karibuni nitamtesa kwa mateso makuu.
18. Hakika yeye alifikiri na alipimia.
19. Basi ameangamia alipimaje!
20. Tena ameangamia alipimaje!
21. Kisha akatazama.
22. Kisha akakunja kipaji na akafinya uso.
23. Kisha aligeuka na akajivuna.
24. Na akasema: Hii si kitu ila ni uchawi ulionukuliwa.
25. Hii siyo ila ni kauli ya binadamu.
26. Karibuni nitamtia Motoni.
27. Na nini kitakujulisha Moto ni nini?
28. Hautabakisha wala hautaacha.
29. Unababua ngozi.
30. Juu yake wako (walinzi) kumi na tisa.
31. Na hatukuweka walinzi wa Moto ila Malaika, wala hatukuifanya hesabu yao ila kuwa jaribio kwa wale waliokufuru, ili wawe na yakini waliopewa Kitabu, na walioamini wazidi katika imani, wala wasiwe na shaka wale waliopewa Kitabu na Waumini, na ili walio na ugonjwa katika nyoyo zao na waliokufuru waseme: Anataka nini Mwenyeezi Mungu kwa mfano huu? Hivyo ndivyo anavyompoteza Mwenyeezi Mungu anayetaka, na anamuongoza anayetaka, wala hapana yeyote ajuaye majeshi ya Mola wako ila yeye tu, na hayo si kitu ila ni ukumbusho kwa mwanadamu.
32. Sivyo, naapa kwa mwezi.
33. Na kwa usiku unapokucha.
34. Na kwa asubuhi inapopambazuka.
35. Hakika huo ni mmoja wapo katika (misiba) mikubwa.
36. Ni onyo kwa binadamu.
37. Kwa anayetaka miongoni mwenu kwenda mbele au kurudi nyuma.
38. Kila nafsi itafungika (Motoni) kwa (amali mbaya) ilizozichuma.
39. Isipokuwa watu wa kheri.
40. Katika Mabustani, wataulizana.
41. Juu ya waovu.
42. Ni kipi kilichokupelekeni Motoni.
43. Watasema: Hatukuwa miongoni mwa waliosali.
44. Wala hatukuwa tukilisha masikini.
45. Na tulikuwa tukipiga porojo pamoja na wapigao porojo.
46. Na tulikuwa tukikadhibisha siku ya hukumu.
47. Mpaka mauti yakatufikia.
48. Basi hautawafaa uombezi wa waombezi.
49. Basi wamekuwaje kukengeuka onyo hili?
50. Kama kwamba ni punda wanaokwenda mbio.
51. Wanaokimbia simba.
52. Bali kila mmoja wao anataka apewe nyaraka zilizofunuliwa.
53. Sivyo, bali wao hawaiogopi Akhera.
54. Sivyo kwa hakika huo ni ukumbusho.
55. Basi anayetaka aukumbuke.
56. Na hawatakumbuka isipokuwa apende Mwenyeezi Mungu, yeye ndiye Mwenye kuogopwa na Mwenye kusamehe.
55. Basi anayetaka aukumbuke.
56. Na hawatakumbuka isipokuwa apende Mwenyeezi Mungu, yeye ndiye Mwenye kuogopwa na Mwenye kusamehe.