Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 34
Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Alif Lam Mym.
2. Hizo ni Aya za Kitabu kilichotengenezwa vizuri kabisa.
3. Muongozo na rehema kwa wafanyao mema.
4. Wale wanaosimamisha swala na kutoa zaka, nao wana yakini na Akhera.
5. Hao ndio wako juu ya muongozo utokao kwa Mola wao na hao ndio wenye kufaulu.
6. Na katika watu yupo anayenunua maneno ya upuuzi ili kupoteza katika njia ya Mwenyeezi Mungu pasipo elimu, na kuifanyia mzaha, hao watapata adhabu ifedheheshayo.
7. Na wanaposomewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna kama hawakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi, basi mpe khabari za adhabu yenye kuumiza.
8. Hakika wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, zitakuwa kwao Bustani za neema.
9. Watakaa humo milele ni ahadi ya Mwenyeezi Mungu iliyo haki, na yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
10. Ameziumba mbingu pasipo nguzo mzionazo na ameiweka milima ardhini ili (ardhi) isikuyumbisheni, na ametawanya humo wanyama wa kila namna na tumeyateremsha maji kutoka mawinguni na humo tumeotesha (mimea) mizuri ya kila aina.
11. Haya ndiyo maumbile ya Mwenyeezi Mungu, basi nionyesheni ni nini walichoumba wale walio kinyume naye, lakini madhalimu wamo katika upotovu dhahiri.
12. Na kwa hakika tulimpa Luqmani hekima ya kwamba, mshukuru Mwenyeezi Mungu, na atakayekushukuru, basi kwa hakika atashukuru kwa ajili ya nafsi yake, na atakaekufuru, basi Mwenyeezi Mungu ni Mkwasi, Mwenye kusifiwa.
13. Na (kumbukeni) Luqmani alipomwarnbia mwanawe huku akimsihi: Ewe mwanangu! usimshirikishe Mwenyeezi Mungu na chochote, hakika shirki ndiyo dhulma kubwa.
14. Na tumemuusia mwanadamu kwa ajili ya wazazi wake, mama yake amembeba kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha kunyonya katika miaka rniwili, kwamba: Unishukuru mimi na wazazi wako, marudio (ya mwisho) ni kwangu.
15. Na kama (wazazi wako) wakikushurutisha kunishirikisha na yule ambaye huna khabari naye, basi usiwatii, na kaa nao kwa wema hapa duniani, na shika njia ya yule anayeelekea kwangu kisha mtarejea kwangu, basi nitakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.
16. Ewe mwanangu! kwa hakika jambo lolote lijapokuwa na uzito wa chembe ya khardali, likawa ndani ya mwamba au mbinguni au ardhini, Mwenyeezi Mungu atalileta, bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye khabari.
17. Ewe Mwanangu! simamisha swala na uamrishe mema, na kukataza mabaya na usubiri juu ya yale yanayokupata, hakika hayo ni katika mambo yanayoazimiwa.
18. Wala usiwafanyie watu jeuri, wala usitembee katika nchi kwa maringo hakika Mwenyeezi Mungu hampendi kila ajivunaye, ajifakharishaye.
19. Na ushike mwendo wa katikati, na uteremshe sauti yako, bila shaka sauti ya punda ni mbaya kuliko sauti zote.
20. Je, hamuoni ya kwamba Mwenyeezi Mungu amekutiishieni, vilivyomo mbinguni na ardhini, na akakukamilishieni neema zake zilizo dhahir na za siri? na wako watu wanaobishana katika (mambo ya) Mwenyeezi Mungu pasipo elimu wala muongozo wala Kitabu chenye nuru.
21. Na wanapoambiwa, fuateni aliyoyateremsha Mwenyeezi Mungu, husema:
Bali tunafuata tuliyowakuta nayo baba zetu. Je, ijapokuwa shetani, anawaita kwenye adhabu ya Moto?
22. Na ajisalimishaye uso wake kwa Mwenyeezi Mungu naye nimtenda mema, basi bila shaka amekwisha kamata kishikio kilicho madhubuti, na mwisho wa mambo yote ni kwa Mwenyeezi Mungu.
23. Na anayekufuru, basi isikuhuzunishe kufru yake, marudio yao ni kwetu, ndipo tutawaambia yale waliyoyafanya, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
24. Tutawastarehesha kidogo, kisha tutawasuknma katika adhabu ngumu.
25. Na kama ukiwauliza: Ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi? Bila shaka watasema: Mwenyeezi Mungu. Sema kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu lakini wengi wao hawajui.
26. Kila kilichomo mbinguni na ardhini ni cha Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa.
27. Na lau kama miti yote iliyomo ardhini ingelikuwa kalamu, na bahari akaifanya wino, baada yake bahari nyingine saba, maneno ya Mwenyeezi Mungu yasingelikwisha. Bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye hekima.
28. Hakukuwa kuumbwa kwenu wala kufufuliwa kwenu ila kama nafsi moja hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
29. Je, huoni ya kwamba Mwenyeezi Mungu huingiza usiku katika mchana, na huingiza mchana katika usiku na amevitiisha jua na mwezi, vyote hupita mpaka wakati uliowekwa, na Mwenyeezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.
30. Hivyo ni kwa sababu Mwenyeezi Mungu ndiye Haki, na wanachokiomba badala yake ni uongo, na bila shaka Mwenyeezi Mungu ndiye Mtukufu, Mkuu.
31. Je, huoni kwamba jahazi hupita baharini kwa neema za Mwenyeezi Mungu ili awaonyeshe dalili zake: Hakika katika hayo mna mazingatio kwa kila mwenye subira nyingi, mwenye shukrani.
32. Na wimbi linapowafunika kama vivuli, humuomba Mwenyeezi Mungu kwa kumtii kweli kweli, lakini anapowaokoa kuwaleta barani, baadhi yao hushika mwendo wa kati kati, wala hapana anayezikanusha neema zetu ila kila mdanganyifu mkuu, kafiri mkubwa.
33. Enyi watu! Mcheni Mola wenu na iogopeni siku ambayo haitamfaa baba kwa watoto wake, wala mtoto hatamfaa baba yake hata kidogo, bila shaka ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni haki, basi yasikudanganyeni maisha ya dunia hii, wala asikudanganyeni mdanganyifu katika (mambo ya) Mwenyeezi Mungu.
34. Kwa hakika ujuzi wa Kiyama uko kwa Mwenyeezi Mungu, naye huteremsha mvua, kuyajua yaliyomo matumboni, na nafsi yoyote haijui ni nini itakayochuma kesho, wala haijui nafsi itafia ardhi gani, bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi Mwenye khabari.