Surah Jinn

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 28

Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Sema: Imefunuliwa kwangu kuwa, kundi moja la majinni lilisikia (Qur’an) likasema: Hakika tumesikia Qur’an ya ajabu.

2. Inaongoza kwenye uongofu, kwa hiyo tumeamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu.

3. Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu umetukuka, hakujifanyia mke wala mwana.

4. Na kwa hakika mpumbavu miongoni mwetu alikuwa akisema maneno ya upuuzi juu ya Mwenyeezi Mungu.

5. Nasi tulikuwa tukidhani kuwa watu na majinni hawatasema uongo juu ya Mwenyeezi Mungu.

6. Na hakika kulikuwa na watu miongoni mwa wanadamu wakijikinga kwa watu miongoni mwa majinni, hivyo wakawazidishia kiburi.

7. Na kwa hakika wao walidhani kama mlivyodhani nyinyi kuwa, Mwenyeezi Mungu hatamtuma yeyote.

8. Nasi tuliigusa mbingu tukaiona imejaa walinzi wenye nguvu na nyota zing’aazo.

9. Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza, lakini anayetaka kusikiliza sasa atakuta kimondo kikimvizia.

10. Nasi hatujui kama shari inatakiwa kwa wale wanaokaa ardhini au Mola wao anawatakia muongozo?

11. Na hakika katika sisi wamo wema na wengine katika sisi ni kinyume cha hayo, tulikuwa njia mbalimbali.

12. Nasi tulijua kuwa hatuwezi kumshinda Mwenyeezi Mungu katika nchi wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia.

13. Nasi tulipousikia muongozo, tukauamini, basi anayemwamini Mola wake hataogopa khasara wala ubaya.

14. Nasi wamo miognoni mwetu waliosilimu na wamo miongoni mwetu waovu lakini aliyesilimu basi hao ndio waliotafuta uongofu.

15. Ama wale waovu, basi wamekuwa kuni za Jahannam.[1]

16. Na kama wangelishika kwa imara njia (iliyonyooka) tungeliwanywesha maji kwa wingi.

17. Ili tuwajaribu kwa hayo, na anayepuuza kumkumbuka Mola wake atamsukuma kwenye adhabu ngumu.

18. Na kwa hakika Misikiti yote ni ya Mwenyeezi Mungu basi msimuombe mwingine pamoja na Mwenyeezi Mungu.

19. Na kwa hakika mja wa Mwenyeezi Mungu aliposimama kumuomba (Mola wake) walikuwa karibu kumuangukia.

20. Sema: Ninamuomba Mola wangu tu wala simshirikishi na yeyote.

21. Sema kwa hakika mimi similiki kwa ajili ya dhara juu yenu wala kheri.

22. Sema bila shaka hapana yeyote awezaye kunilinda na Mwenyeezi Mungu, wala sitapata makao ya salama ila kwake yeye tu.

23. Ila kwa kufikisha (ujumbe) utokao kwa Mwenyeezi Mungu na amri zake, na atakayemuasi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, basi bila shaka atapata Moto wa Jahannam watakaa humo milele.

24. Hata watakapoyaona wanayoahidiwa ndipo watakapojua ni nani mwenye msaidizi dhaifu na mwenye idadi ndogo.

25. Sema: Sijui kama yako karibu mliyoahidiwa na Mola wangu atayawekea muda mrefu.

26. Ni mjuzi wa siri wala hamdhihirishii yeyote siri yake.

27. Isipokuwa Mtume aliye mridhia, basi hakika yeye humuwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.

28. Ili ajue (Mtume) kuwa: Wamekwisha fikisha ujumbe wa Mola wao, na anayajua (Mwenyeezi Mungu) yote waliyo nayo, na amedhibiti idadi ya kila kitu.