Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 25
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Mbingu itakapopasuka.
2. Na ikamtii Mola wake na ikafanya ndivyo.
3. Na ardhi itakaponyooshwa.
4. Na ikatupa vilivyomo na ikawa tupu.
5. Na ikamtii Mola wake na ikafanya ndivyo.
6. Ewe Mtu! hakika wewe ni mwenye kufanya juhudi kwa Mola wako, juhudi ambayo utaikuta.
7. Basi atakayepewa daftari lake katika mkono wake wa kulia.
8. Basi atahesabiwa hesabu nyepesi.
9. Na atarudi kwa watu wake mwenye furaha.
10. Ama atakayepewa daftari lake nyuma ya mgongo wake.
11. Basi atayaita mauti.
12. Na ataingia Motoni.
13. Maana yeye alikuwa anakaa katika watu wake kwa furaha.
14. Hakika yeye alidhani kuwa hatarejea.
15. Naam, hakika Mola wake alikuwa akimuona.
16. Basi ninaapa kwa wekundu wa jua linapokuchwa.
17. Na kwa usiku na unavyovikusanya.
18. Na kwa mwezi unapokomaa.
19. Mtakutana na hali baada ya hali.
20. Basi wana nini hawaamini?
21. Na wanaposomewa Qur’an hawanyenyekei.
22. Lakini wale waliokufuru wanakadhibisha.
23. Na Mwenyeezi Mungu, anajua zaidi wanayoyakusanya.
24. Basi wape khabari ya adhabu yenye kuumiza.
25. Isipokuwa wale walioamini wakatenda vitendo vizuri, watapata malipo mema yasiyokoma.