Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 31
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Hakika ulimfikia mtu wakati fulani wa zama ambapo hakuwa kitu kinachotajwa.
2. Kwa hakika tulimuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika, tunamjaribu, hivyo tukamfanya ni mwenye kusikia, mwenye kuona.
3. Hakika sisi tumemuongoza njia awe mwenye kushukuru au awe mwenye kukufuru.
4.Hakika sisi tumewaandalia makafiri minyororo na mapingu na Moto uwakao.
5.Hakika watawa watakunywa katika kikombe kilichochanganyika na kafuri.
6.(Itakuwako) chemchem watakayoinywa waja wa Mwenyeezi Mungu, wataitiririsha mtiririko (mzuri).
7.Wanazitimiza nadhiri na wanaiogopa siku ambayo shari yake itaenea.
8.Na huwalisha chakula masikini na yatima na mfungwa hali ya kuwa wanakipenda.
9.(Husema) Tunakulisheni kwa ajili ya radhi ya Mwenyeezi Mungu tu, hatutaki kwenu malipo wala shukurani.
10.Hakika sisi tunaogopa kutoka kwa Mola wetu siku yenye shida na taabu.
11.Basi Mwenyeezi Mungu atawalinda katika shari ya siku hiyo na kuwakutanisha na neema na furaha.
12.Na atawapa Mabustani na hariri kwa sababu walisubiri.
13.Humo wataegemea viti vya enzi humo hawataona jua (kali) wala baridi (kali).
14. Na vivuli vyake vitafikia karibu yao na matunda yataning’inia chini chini.
15. Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae.
16. Vigae vya fedha, wamevifanya kwa vipimo.
17. Na humo watanyweshwa kikombe kilichochanganyika na tangawizi.
18. Humo mna chemchem inayoitwa salsabil.
19. Na watawazungukia wavulana wasiochakaa, utakapowaona utawafikiri ni lulu zilizotawanywa.
20. Na utakapoyaona humo utaona neema na ufalme mkubwa.
21. Juu yao (watavaa) nguo za hariri laini ya kijani kibichi na za hariri nzito, na watavikwa bangili za fedha na Mola wao atawanywesha kinywaji safi.
22. Hakika haya ni malipo yenu, na juhudi yenu imekubaliwa.
23. Hakika sisi tumekuteremshia Qur’an sehemu sehemu.
24. Basi ngojea hukumu ya Mola wako wala usimtii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufru.
25. Na litaje jina la Mola wako asubuhi na jioni.
26. Na usiku msujudie yeye, na umtukuze usiku (wakati) mrefu.
27. Kwa hakika hawa wanayapenda wayapatayo upesi, na huiacha nyuma yao siku nzito.
28. Sisi tumewaumba na tukaimarisha viungo vyao, na tutakapotaka tutawaleta wengine badala yao walio kama wao.
29. Hakika huu ni ukumbusho basi anayetaka ashike njia kwa Mola wake.
30. Wala hamuwezi kutaka asipotaka Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye elimu, Mwenye hekima.
31. Anamwingiza anayemtaka katika rehema yake, na madhalimu amewawekea dhabu yenye kuumiza.