Surah Infitaar

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina  Aya 19

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Mbingu zitakapo pasuka.

2. Na nyota zitakapotawanyika.

3. Na bahari zitakapopasuliwa.

4. Na makaburi yatakapofukuliwa.

5. Nafsi itajua iliyoyatanguliza na iliyoyabakisha nyuma.

6. Ewe Mwanadamu ni nini kikudanganyacho na Mola wako Mtukufu.

7. Aliyekuumba na kukutengeneza, kisha akakulinganisha sawa.

8. Katika sura yoyote aliyoitaka amekutengeneza.

9. Sivyo, bali nyinyi mnaikadhibisha siku ya hukumu.

10. Na hakika juu yenu kuna walinzi.

11. Waandishi wenye heshima.

12. Wanayajua mnayoyatenda.

13. Kwa hakika watu wema watakuwa katika neema.

14. Na kwa hakika waovu watakuwa Motoni.

15. Wataingia humo siku ya Malipo.

16. Wala hawatakuwa mbali nao.

17. Na nini kitakujulisha siku ya malipo ni nini?

18. Tena nini kitakujulisha siku ya malipo ni nini?

19. Ni siku ambayo nafsi haitaimiliki nafsi (nyingine) chochote, na amri siku hiyo itakuwa ya Mwenyeezi Mungu.