Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 24
Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Vinamtukuza Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyorno ardhini na yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
2. Yeye ndiye aliyewatoa waliokufuru miongoni mwa watu wa Kitabu katika nyumba zao wakati wa uhamisho wa kwanza, hamkudhani kuwa watatoka, nao walidhani kuwa ngome zao zitawalinda na Mwenyeezi Mungu, lakini Mwenyeezi Mungu akawafikia kwa mahala wasipopatazamia, na akatia woga katika nyoyo zao, wakazivunja nyumba zao kwa mikono yao na kwa mikono ya waumini, basi angalieni, enyi wenye macho.
3. Na lau kama Mwenyeezi Mungu asingeliwaandikia uhamisho angeliwaadhibu duniani, na katika Akhera watapata adhabu ya Moto.
4. Hayo ni kwa sababu walimhalifu Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na atakayemhalifu Mwenyeezi Mungu basi kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
5. Mtende wowote mlioukata au mliouacha umesimama katika mizizi yake, basi ni kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu, na kuwafedhehesha wavunjao Sharia.
6. Na mali aliyoleta Mwenyeezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwao hamkuyaendea kwa farasi wala kwa ngamia, lakini Mwenyeezi Mungu huwapa mamlaka Mitume wake juu ya yeyote amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
7. Mali aliyoleta Mwenyeezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwa watu wa vijijini, ni kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu na Mtume na jamaa (zake) na mayatima na masikini na msafiri, ili isiwe inayorudia baina ya matajiri wenu tu. Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni basi jiepusheni, na mcheni Mwenyeezi Mungu, kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
8. (na mali hayo) ni kwa mafukara walio hama ambao walifukuzwa katika nyumba zao na mali zao wakitafuta fadhili za Mwenyeezi Mungu na radhi (yake) na wakamsaidia Mwenyeezi Mungu na Mtume wake hao ndio wakweli.
9. Na (pia wapewe) wale waliofanya maskani (yao madina) na kushika imani kabla ya hao, wanawapenda waliohamia kwao, wala hawapati dhiki nyoyoni mwao kwa hayo waliyopewa, na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo. Na aepushwaye na ubakhili wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.
10. Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu! tusamehe sisi na ndugu zetu waliotutangulia katika imani wala usiweke mfundo katika nyoyo zetu kwa walioamini, Mola wetu! hakika wewe ni Mpole sana, Mwenye kurehemu.
11. Je, huwaoni wale wanaofanya unafiki wanawaambia ndugu zao waliokufuru miongoni mwa watu wa Kitabu: Kama mkifukuzwa bila shaka nasi pia tutaondoka pamoja nanyi, wala hatutamtii yeyote kabisa juu yenu, na kama mkipigwa vita lazima tutakusaidieni, na Mwenyeezi Mungu anashuhudia kuwa wao kwa hakika ni waongo.
12. Kama wakifukuzwa hawatatoka pamoja nao, na kama wakipigwa hawatawasaidia, na kama wakiwasaidia lazima watakimbia, kisha hawatasaidiwa.
13. Hakika nyinyi mnaogopwa zaidi katika nyoyo zao kuliko (wanavyo muogopa) Mwenyeezi Mungu, hayo ni kwa sababu wao ni watu wasiofahamu.
14. Hawatapigana nanyi kwa umoja (wao) isipokuwa katika vijiji vilivyohifadhiwa, au nyuma ya kuta, mapigano yao baina yao ni makali, utawadhani kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio na akili.
15. (Hali yao ni) kama ya wale waliowatangulia hivi karibuni, walionja ubaya wa mambo yao, nao watapata adhabu yenye kuumiza.
16. Ni kama shetani anapomwambia mtu: Kufuru: Lakini anapokufuru, husema: Mimi si pamoja nawe, hakika namuogopa Mwenyeezi Mungu, Mola wa walimwengu.
17. Basi mwisho wa wote wawili ukawa kwamba waingie Motoni kukaa milele humo, na hayo ndiyo malipo ya madhalimu.
18. Enyi mlioamini! mcheni Mwenyeezi Mungu na mtu aangalie aliyoyatanguliza kwa ajili ya kesho, na mcheni Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.
19. Wala msiwe kama wale waliomsahau Mwenyeezi Mungu, kwa hiyo akawasahaulisha nafsi zao, hao ndio wavunjao Sharia.
20. Hawawi sawa watu wa Motoni na watu wa Peponi, watu wa Peponi ndio wenye kufuzu.
21. Lau kama tungeliiteremsha hii Qur’an juu ya mlima ungeliuona ukinyenyekea (na) kupasuka kwa sababu ya khofu ya Mwenyeezi Mungu na hiyo ni mifano tunawapigia watu ili wafikiri.
22. Yeye ndiye Mwenyeezi Mungu ambaye hapana aabudiwaye isipokuwa Yeye tu, ajuaye yasiyoonekana na yanayoonekana, yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
23. Yeye ndiye Mwenyeezi Mungu ambaye hapana aabudiwaye isipokuwa Yeye tu, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani. Mwangaliaji. Mwenye nguvu, Jabbaari, Mkubwa, Mwenyeezi Mungu yu mbali na hao wanaomshirikisha.
24. Yeye ndiye Mwenyeezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mfanyaji wa sura, Mwenye majina mazuri, kinamtukuza kilichomo mbinguni na ardhini. naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.