Sura hii imeteremshwa Madina na ina Aya 29
Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu,
1. Kinamtukuza Mwenyeezi Mungu kila kilichomo mbinguni na ardhini, na yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
2. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake, huhuisha na hufisha, na yeye ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
3. Yeye ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho, naye ni wa dhahiri, na wa siri, naye ni Mjuzi wa kila kitu.
4. Yeye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi katika nyakati sita kisha ukakamilika (uumbaji wake) katika Arshi, anajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni na yanayopanda humo, Naye yu pamoja nanyi popote mlipo, na Mwenyeezi Mungu anaona mnayoyatenda.
5. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake, na mambo yote hurudishwa kwa Mwenyeezi Mungu.
6. Huingiza usiku katika mchana na huingiza mchana katika usiku, na yeye anajua yaliyomo vifuani.
7. Mwaminini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, na toeni katika yale aliyokupeni, basi wale walioamini miongoni mwenu na wakatoa, wana malipo makubwa.
8. Na mmekuwaje hamwamini Mwenyeezi Mungu, hali Mtume ana waiteni kumwamini Mola wenu, naye amekwisha chukua ahadi kwenu ikiwa nyinyi ni wenye kuamini.
9. Yeye ndiye anayeteremsha Aya zilizo wazi juu ya mja wake, ili kukutoeni katika giza mwende kwenye nuru, na bila shaka Mwenyeezi Mung.u ni Mpole kwenu, Mwenye kurehemu.
10. Na mmekuwaje hamtoi katika njia ya Mwenyeezi Mungu na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyeezi Mungu? Hawawi sawa miongoni mwenu aliyetoa kabla ya kushinda na kupigana hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale ambao wametoa nyuma na wakapigana. Na Mwenyeezi Mungu amemwahidia wema kila mmoja, na Mwenyeezi Mungu anazo khabari za hayo mnayoyatenda.
11. Ni nani anayempa Mwenyeezi Mungu karadha nzuri ili amzidishie mara mbili? naye atapata malipo mazuri.
12. Siku utakayowaona Waumini wanaume na Waumini wanawake nuru zao zina kwenda mbele yao na kulia kwao (wataambiwa) Furahini leo, ni Bustani zipitazo mito chini yake, kukaa humo milele, huko ndiko kufaulu kukubwa.
13. Siku watakaposema wanafiki wanaume na wanafiki wanawake kuwaambia walioamini: Tungojeni ili tupate mwangaza katika nuru yenu. Wataambiwa: Rudini nyuma yenu na tafuteni nuru. Ndipo ukingo wa ukuta wenye mlango utapigwa kati yao, ndani yake mna rehema na upande wake wa nje kuna adhabu.
14. Watawaita: je, Hatukuwa pamoja nanyi? Watasema: Ndiyo lakini nyinyi mlijitia wenyewe katika ukafiri na mkangojea na mkaona shaka, na matamanio yakakudanganyeni hata amri ya Mwenyeezi Mungu ikafika, na mdanganyifu (Iblis) amekudanganyeni katika (khabari) za Mwenyeezi Mungu.
15. Basi leo haitapokelewa kwenu fidia wala kwa wale waliokufuru makao yenu ni Motoni, ndio rafiki yenu, nayo ni marejeo mabaya.
16. Je, wakati haujafika kwa wale walioamini kwamba nyoyo zao zinyenyekee kwa kumkumbuka Mwenyeezi Mungu na kwa mambo ya haki yaliyoteremka? Wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu zamani na muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikawa ngumu, na wengi wao ni waasi.
17. Jueni ya kuwa Mwenyeezi Mungu huihuisha ardhi baada ya mauti yake. Bila shaka tumekubainishieni Miujiza (mbali mbali) ili mpate kufahamu.
18. Kwa hakika wanaume watoao sadaka na wanawake watoao sadaka na wale wanaompa Mwenyeezi Mungu karadha nzuri watazidishiwa maradufu na wapate malipo mazuri (Akhera).
19. Na wale walioamini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, hao ndio Masiddiki na Mashahidi mbele ya Mola wao, watapata malipo yao na nuru yao; Lakini waliokufuru na kukadhibisha Aya zetu, hao ndio watu wa Motoni.
20. Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo na upuuzi na pambo na kujifakharisha baina yenu, na tamaa ya kuzidiana katika mali na watoto. (Mfano wake ni) kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mazao yake, kisha yanakauka ukayaona yenye rangi ya manjano, kisha yanakuwa yenye kuvunjika vunjika, na katika Akhera ni adhabu kali na (pia) msamaha wa Mwenyeezi Mungu na radhi (yake) na maisha ya dunia siyo ila ni starehe idanganyayo tu.
21. Yaendeeni upesi (mambo ya kukupatieni) msamaha wa Mola wenu na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyowekewa wale waliomwamini Mwenyeezi Mungu na Mitume wake, hiyo ni fadhili ya Mwenyeezi Mungu, humpa amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye fadhili kuu.
22. Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila huwamo kitabuni kabla hatujauumba, kwa hakika hilo ni rahisi kwa Mwenyeezi Mungu.
23. Ili msihuzunike juu ya kitu kilichokupoteeni, wala msifurahi kwa alichokupeni. Na Mwenyeezi Mungu hampendi kila ajivunaye, ajifakharishaye.
24. Ambao wanafanya ubakhili na kuwaamuru watu wafanye ubakhili, na ageukaye, basi Mwenyeezi Mungu yeye ni Mkwasi Mwenye kusifiwa.
25. Kwa hakika tuliwapeleka Mitume wetu kwa dalili wazi wazi na tukakiteremsha Kitabu na mizani pamoja nao, ili watu wasimame kwa uadilifu. Na tumekiumba chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyeezi Mungu ajulishe anayemsaidia yeye na Mitume wake kwa siri. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.[1]
26. Na bila shaka tulimpeleka Nuhu na Ibrahimu na tukauweka katika kizazi chao Unabii na Kitabu, basi wengi wao ni waongofu na wengi wao ni waasi.
27. Kisha tukawafuatisha nyuma yao Mitume wetu (wengine) na tukamfuatisha Isa bin Mariam na tukampa Injili, na tukauweka upole na rehema katika nyoyo za wale waliomfuata. Na uruhubani wameubuni (wenyewe) sisi hatukuwaandikia ila kuitaka radhi ya Mwenyeezi Mungu tu, lakini hawakufuata kama inavyotakiwa kuufuata, basi tukawapa wale walioamini miongoni mwao malipo yao, na wengi wao ni waasi.
28. Enyi mlioamini! mcheni Mwenyeezi Mungu na mwaminini Mtume wake, atakupeni sehemu mbili za rehema zake, na atakufanyieni nuru ya kwenda nayo (Akhera) na atakusameheni, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
29. Ili watu wa Kitabu wajue kwamba: Wao hawana uwezo wowote juu ya fadhili za Mwenyeezi Mungu, na kwa kweli fadhili zimo mikononi mwa Mwenyeezi Mungu, humpa amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye fadhili kuu.