Surah Haaqqa

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina  Aya 52

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Tukio la haki.

2. Ni nini tukio la haki?

3. Na nini kitachokujulisha tukio la haki ni nini?

4. Thamudi na A’di walikadhibisha Kiyama.

5. Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa.

6. Na ama Adi waliangamizwa kwa upepo mkali usiozuilika.

7. Aliowapelekea siku saba na michana minane, moja kwa moja bila kusita, utaona watu wameanguka (wamekufa) kama kwamba ni magogo ya mitende mitupu.

8. Basi je, unamuona mmoja wao aliyebaki?

9. Na Firaun na waliomtangulia na (watu wa) miji iliyopinduliwa walikosa.

10. Na wakamuasi Mtume wa Mola wao ndipo akawakamata kwa mkamato wenye nguvu sana.

11. Maji yalipofurika hakika sisi tulikupandisheni katika jahazi.

12. Ili tuifanye ukumbusho kwenu, na sikio lisikialo lisikie.

13. Na litakapopulizwa baragumu mpulizo mmoja.

14. Na ardhi na milima vitaondolewa na vitavunjwa mvunjiko mmoja.

15. Basi siku hiyo tukio litatokea.

16. Na mbingu itapasuka, nayo siku hiyo itakuwa dhaifu.

17. Na Malaika watakuwa kandoni mwake, na Malaika wa namna nane watachukua Kiti cha Enzi cha Mola wako juu yao.

18. Siku hiyo mtahudhurishwa, haitafichika kwenu siri yoyote.

19. Basi ama yule atakayepewa daftari lake kwa mkono wake wa kulia atasema: Haya someni daftari langu.

20. Hakika nilijua kuwa nitapokea hesabu yangu.

21. Basi yeye atakuwa katika maisha ya raha.

22. Katika Bustani iliyo juu.

23. Vishada vyake vitakuwa karibu.

24. Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa sababu ya vitendo mlivyofanya katika siku zilizopita.

25. Lakini atakayepewa daftari lake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Eh! laiti nisingelipewa daftari langu!

26. Wala nisingelijua ni nini hesabu yangu.

27. Laiti (mauti) yangemaliza.

28. Mali yangu haikunifaa.

29. Ukubwa wangu umenipotea.

30. Mkamateni na mtieni minyororo.

31. Kisha mtupeni Motoni.

32. Tena katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabini mwingizeni.

33. Hakika yeye alikuwa hamwamini Mwenyeezi Mungu, Mtukufu.

34. Wala hahimizi kulisha masikini.

3.5. Basi leo hapa hana rafiki mpenzi.

36. Wala hana chakula ila maji ya usaha.

37. Hali (chakula) hicho isipokuwa wakosefu.

38. Basi naapa kwa mnavyoviona.

39. Na msivyoviona.

40. Kwa hakika hii ni kauli ya Mtume mwenye heshima.

41. Wala hiyo si kauli ya mshairi, ni kidogo tu mnayoyaamini.

42. Wala si kauli ya mchawi, ni kidogo tu mnayoyakumbuka.

43. Ni uteremsho kutoka kwa Mola wa viumbe vyote.

44. Na kama angelizua juu yetu baadhi ya maneno.[1]

45. Lazima tungelimshika kwa mkono wa kulia.

46. Kisha kwa hakika tungelimkata mshipa mkubwa wa moyo.

47. Na hapana mmoja wenu ambaye angeweza kutuzuia naye.

48. Na kwa hakika (hii Qur’an) ni mawaidha kwa wenye kumcha (Mwenyeezi Mungu).

49. Kwa hakika tunajua kuwa miongoni mwenu wamo wanaokadhibisha.

50. Lakini kwa kweli ni sikitiko juu ya wanaokataa.

51. Na hakika hii (Qur’an) ni haki kwa yakini.

52. Basi litukuze jina la Mola wako aliye mkuu.