Surah Furqan

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 77

Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Mwenye baraka ni yule aliyeteremsha Qur’an kwa mja wake ili awe muonyaji kwa walimwengu.

2. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakufanya mtoto wala hana mshirika katika ufalme, na ameumba kila kitu, na kakikadiria kipimo.

3. Na badala ya Mwenyeezi Mungu wamefanya miungu ambao hawaumbi chochote hali wao wanaumbwa wala hawajimilikii dhara wala nafuu, wala hawamiliki mauti wala uhai wala ufufuo.

4. Na wamesema wale waliokufuru. Haya si chochote ila ni uzushi aliouzua, na wamemsaidia juu yake watu wengine. Basi wameleta dhulma na uongo.

5. Na wakasema: Ni visa vya (watu) wa zamani alivyoviandikisha, anavyosomewa asubuhi na jioni.

6. Sema: ameyateremsha yule ajuaye siri za mbinguni na ardhini, bila shaka yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

7. Na wakasema: Mtume gani huyu anayekula chakula na anatembea sokoni? Mbona hakuteremshiwa Malaika awe muonyaji pamoja naye?

8. Au aangushiwe khazina au iwe kwake bustani ale katika hiyo? Na madhalimu wakasema: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliyerogwa,

9. Tazama jinsi wanavyokupigia mifano basi wamepotea wala hawataweza (kushika) njia.

10. Mwenye baraka ni yule ambaye akitaka atakufanyia bora kuliko hivyo, Bustani zipitazo mito chini yake na akujaalie majumba ya kifalme. Bali wanakikadhibisha Kiyama, na tumemwandalia mwenye kuikanusha Kiyama Moto mkali.

11. Bali wanakikadhibisha Kiyama, na tumemwandalia mwenye kukikanusha Kiyama Moto mkali.

12. (Moto) utakapowaona katika mahala pa mbali watasikia hasira yake na mngurumo.

13. Na watakapotupwa humo mahala pafinyu hali wamefungwa ndipo hapo watayaita mauti.

14. Msiyaite leo mauti mamoja bali yaiteni mengi.

 15. Sema: Je, haya ni bora au Pepo ya milele ambayo wameahidiwa wacha Mungu? iwe kwao malipo (mazuri) na marejeo.

16. Watapata humo watakayoyataka, wakae humo milele. Hii ni ahadi juu ya Mola wako inayotakiwa kulipwa.

17. Na siku atakayowakusanya hawa na wale wanaowaabudu badala ya Mwenveezi Mungu, basi atasema: Je nyinyi mmewapotez-a waja wangu hawa au wenyewe wamepotea njia?

18. Watasema: Umetakasika na upungufu! haikutupasa kuwafanya viongozi badala yako, lakini wewe uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau mawaidha (yako) na wakawa watu walioangamia.

19. Na bila shaka wamekukadhibisheni kwa yale mliyoyasema, na hamuwezi kuondoa (adhabu) wala kupata msaada. Na atakayedhulumu miongoni mwenu tutamuonjesha adhabu kubwa.

20. Na hatukupeleka kabla yako Mitume ila bila shaka walikuwa wakila chakula na wakitembea masokoni, na tumewajaalia baadhi yenu wawe mtihani kwa wengine, je, mtavumilia? Na Mola wako ndiye aonaye.

21. Na walisema wale wasiotumai kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika, au kumuona Mola wetu? Bila shaka wamejitukuza katika nafsi zao na wameasi uasi mkubwa.

22. Siku watakayowaona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wenye makosa, na watasema: Kuwe na kizuizi kizuiacho.

23. Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo kisha tutayafanya mavumbi yaliyotawanyika.

24. Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makazi mema na mahala penye starehe njema.

25. Na siku itakapopasuka mbingu kwa mawingu, na watateremshwa Malaika kwa wingi.

26. Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.

27. Na siku (hiyo) dhalimu atajiuma mikono yake, akisema: Laiti ningelishika njia pamoja na Mtume.

28. Eee Ole wangu! laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki.

29. Kwa hakika yeye alinipoteza nikaacha mawaidha baada ya kunifikia, na shetani ndiye anayemtupa mwanadamu.

30. Na Mtume atasema: Ee Mola wangu hakika watu wangu wameifanya Qur’an hii kuwa kitu kilichoachwa.

31. Na hivyo ndivyo tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa waovu na Mola wako anatosha kuwa Kiongozi na Msaidizi.

32. Na wakasema wale waliokufuru: Mbona haikuteremshwa kwake Qur’an yote mara moja? Ndivyo hivyo, ili tukuimarishe kwayo moyo wako, na tumeipanga kwa mpango.

33. Wala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea haki na tafsiri iliyo bora.

34. (Ama) wale watakaokusanywa kifudi fudi kwenye Jahannam, hao watakuwa mahala pabaya na ndio wenye kuipotea njia sana.

35. Na bila shaka tulimpa Musa Kitabu na tukamuweka pamoja naye nduguye Harun kuwa waziri.

36. Tukawaambia: Nendeni kwa watu waliokadhibisha Aya zetu, basi tukawaangamiza kabisa.

37. Na watu wa Nuhu, walipowakadhibisha Mitume tukawagharikisha na tukawafanya mazingatio kwa ajili ya wanadamu, na tukawaandalia madhalimu adhabu yenye kuumiza.

38. Na kina Adi na Thamudi na watu wa khandaki na vizazi vingi vilivyokuwa kati yao.

39. Na wote tuliwapigia mifano na wote tuliwaangamiza kabisa.

40. Na kwa hakika, wao walifika kwenye mji ulionyeshewa mvua mbaya, basi je, hawakuwa wakiuona? Bali walikuwa hawatumaini kufufuliwa.

41. Na wanapokuona hawakufanyii ila kejeli tu, je, huyu ndiye Mwenyeezi Mungu aliyemtuma kuwa Mtume.

42. Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza kwa miungu yetu kama tusingelikazana juu yao. Na karibu watajua, watakapoiona adhabu ni nani aliyepotea njia?

43. Je, umemuona yule aliyefanya matamanio yake kuwa Mungu wake? Basi je, utakuwa mlinzi wake?

44. Au je, unafikiri kuwa wengi wao wanasikia au wanafahamu? Hao siyo ila ni kama wanyama, bali wao wameipotea njia zaidi.

45. Je, hukuona Mola wako jinsi alivyokitandaza kivuli? Na angelitaka bila shaka angekifanya kitulie, kisha tumelifanya jua liwe dalili juu yake.

46. Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo.

47. Naye ndiye aliyekufanyieni usiku kuwa kivazi na usingizi kuwa mapumziko, akaufanya mchana kuwa matawanyiko.

48. Naye ndiye azitumaye pepo kuwa khabari njema kabla ya (kufika) rehema yake, na tunayateremsha kutoka mawinguni maji safi.

49. Ili kwa hayo tuihuishe nchi iliyokufa na tuwanyweshe baadhi ya tuliowaumba katika wanyama na watu wengi.

50. Na kwa hakika tunaigawa (hii mvua) baina yao mara kwa mara ili wakumbuke, lakini watu wengi wanakataa ila kukufuru tu.

51. Na kama tungetaka tungewapelekea katika kila mji muonyaji.

52. Basi usiwatii makafiri na ushindane nao kwa (Qur’an) mashindano makubwa.

53. Naye ndiye aliyeziunganisha bahari mbili, hii ni tamu itulizayo kiu, na hii ni yenye chumvi kali, na akaweka kinga kati yake na kizuizi kizuiacho.

54. Naye ndiye Muumba mwanadamu kwa maji, kisha akamfanyia nasabu na ujamaa wa ndoa. Na Mola wako ni Mwenye uwezo.

55. Na wanayaabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu yasiyowafaa wala yasiyowadhuru, na kafiri ni mwenye kwenda kinyume na Mola wake.

56. Nasi hatukukupeleka ila uwe mtoaji wa khabari njema na muonyaji.

57. Sema: Sikuombeni malipo juu yake, isipokuwa mwenye kutaka ashike njia iendayo kwa Mola wake.

58. Na umtegemee Mzima wa milele ambaye hatakufa, na umtukuze kwa sifa zake njema. Naye anatosha kwa dhambi za waja wake kuwa ni Mwenye khabari.

59. Ambaye aliziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika nyakati sita, kisha ukakamilika (uumbaji wake) katika Arshi. Mwenyeezi Mungu Mwingi wa rehema, kwa hiyo uliza khabari zake kwa ajuaye.

60. Na wanapoambiwa: Msujudieni Rahmani, husema: Ni nani Rahmani? Je, tumsujudie unayetuamuru? Na inawazidishia chuki.

61. Mwenye baraka ni yule aliyezijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo jua na mwezi wenye kung’aa.

62. Naye ndiye aliyefanya usiku na mchana vifuatane, kwa yule anayetaka kukumbuka au anayetaka kushukuru.

63. Na waja wa Rahmani ni wale wanaotembea ardhini na unyenyekevu na wajinga wakisema nao, husema: Amani.

64. Na wale wanaokesha usiku kwa ajili ya Mola wao kwa kusujudu na kusimama.

65. Na wale wanaosema: Mola wetu! tuondolee adhabu ya Jahannam, bila shaka adhabu yake ni yenye kuendelea.

66. Hakika (Jahannam) hiyo ni kituo kibaya na mahala (pabaya) pa kukaa.

67. Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo, wala hawafanyi ubakhili na wanakuwa waadilifu baina ya hayo.

68. Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Mwenveezi Mungu wala hawaui nafsi aliyoiharamisha Mwenyeezi Mungu isipokuwa kwa haki, wala hawazini, na atakayefanya hayo atapata dhambi.

69. Atazidishiwa adhabu siku ya Kiyama na atakaa humo kwa kufedheheka.

70. Ila yule aliyetubia na kuamini na kufanya vitendo vizuri, basi hao ndio Mwenyeezi Mungu atawabadilishia maovu yao kuwa mema, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

71. Na aliyetubia na kufanya wema, basi kwa hakika yeye anatubu kwa Mwenyeezi Mungu toba ya kweli.

72. Na wale ambao hawashuhudii uongo na wanapopita penye upuuzi, hupita kwa heshima.

73. Na wale ambao wanapokumbushwa Aya za Mola wao hawajifanyi viziwi nazo na vipofu.

74. Na wale wanaosema: Mola wetu! utupe katika wake zetu na watoto wetu yaburudishayo macho, na utujaalie kuwa viongozi kwa wamchao (Mwenyeezi Mungu).

75. Hao ndio watakaolipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu.

76. Wakae humo milele, kituo kizuri na mahala pazuri pa kukaa.

77. Sema: Mola wangu asingekujalini kama si kule kuomba kwenu, na hali nyinyi mmekwisha kadhibisha, kwa hiyo hivi karibuni (adhabu) itakuwa yenye kushika.