Surah Fatiha

Sura hii imeshuka Makka baada ya Aya tano za suuratul ‘Alaq. Na kwa mara ya pili, imeshuka Madina yalipobadilishwa maelekeo ya Swala. Suuratul Faatiha, ni ya kwanza kupangwa katika Msahafu, lakini katika kushuka ni sura ya pili.

Mwenyeezi Mungu anasema: “Hivi karibuni miongoni mwa watu wajinga watasema: Ni nini kimewageuza kutoka katika kibla chao walichokuwa wakikielekea? Waambie: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyeezi Mungu. Humuongoza amtakae katika njia iliyonyooka.” 2:142.

Mtukufu Mtume s.a.w aliswali akielekea Baytul muqaddas kwa muda wa miaka kumi na mitatu akiwa Makka, kisha alipohamia Madina akaendelea kuswali akielekea Baytul Muqaddas kwa muda wa miezi saba. (wengine wanasema miezi kumi na saba)

Mtume s.a.w alikuwa akimuomba Mwenyeezi Mungu ambadilishie maelekeo ya Swala, akiomba aelekee upande wa Ka’aba katika Swala zake. Siku moja alikuwa akiswali swala ya Adhuhuri katika msikiti wa Bani Salim, rakaa mbili aliziswali ameelekea Baytul Muqaddas kama kawaida yake, kisha Malaika Jibril (a.s) akamshukia, na kumgeuza akamwelekeza upande wa Ka’aba (Makka) kisha akamsomea Aya: “Hakika tumeona uso wako ukielekea mbinguni, basi bila shaka tutakugeuza kwenye kibla ukipendacho, Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtukufu. Na popote mtakapokuwa, zielekezeni nyuso zenu upande huo.” 2:144.

Taz: Alburhan fyitafsiril Qur’an   J.l  Uk. 158

Almizan fyitafsiril Qur’an  J.l  Uk. 334

Majmaul bayan fyitafsiril Qur’an  J.l  Uk. 223

Tafsirus Saafi ‘  J.l  Uk. 195

Tafsirul Qutubi  J.2  Uk. 148-150

Ad-Durrul Mauthur  J.l  Uk. 260

Aalaur Rahman J.l  Uk. 256

Sura hii ina Aya saba pamoja na Bismillahi

1. Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

2. Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, Mola wa viumbe.

3. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

4.Mwenye kumiliki siku ya malipo.

5.Wewe tu tunakuabudu, na kwako tu tunataka msaada.

6.Tuongoze njia iliyo nyooka.

7.Njia ya wale uliowaneemesha, siyo ya (wale) waliokasirikiwa, wala ya (wale) waliopotea.