Surah Fajr

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina  Aya 30

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Naapa kwa alfajiri.

2. Na kwa masiku kumi.

3. Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja.

4. Na kwa usiku unapopita.

5. Hakika katika hayo mna kiapo kwa wenye akili.

6. Je hukuona jinsi Mola wako alivyowafanya Adi.

7. Wa Iram, wenye majumba marefu marefu.

8. Ambao mfano wao haukuumbwa katika miji.

9. Na Thamudi waliochonga majabali (huko) bondeni.

10. Na Firaun mwenye majeshi.

11. Ambao walifanya maovu katika miji.

12. Kisha walizidisha humo ufisadi.

13. Kwa hiyo Mola wako akawateremshia namna ya adhabu.

14. Hakika Mola wako ni Mwenye kuvizia.

15. Ama Mwanadamu Mola wake anapomjaribu na akamtukuza na kumneemesha, basi husema: Mola wangu amenitukuza.

16. Na ama anapomjaribu na kumpunguzia riziki yake, husema: Mola wangu amenidhalilisha.

17. Sivyo bali nyinyi hamuheshimu yatima.

18. Wala nyinyi hamhimizi juu ya kulisha masikini.

19. Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa.

20. Na mnapenda mali kwa pendo la kupita kiasi.

21. Sivyo itakapovunjika ardhi vipande vipande.

22. Na akaja Mola wako, na Malaika safusafu.

23. Na siku hiyo italetwa Jahannam siku hiyo mwanadamu atakumbuka, lakini kutamfaa nini kukumbuka?

24. Atasema: Laiti ningelitanguliza (wema) kwa ajili ya uhai wangu!

25. Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake.

26. Wala hatafunga yeyote jinsi ya kufunga kwake.

27. Ewe nafsi yenye kutua!

28. Rudi kwa Mola wako hali ya kuridhia (na) mwenye kuridhiwa.

29. Basi ingia katika waja wangu (wema).

30. Na ingia katika Pepo yangu.