Surah Buruuj

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina  Aya 22

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Naapa kwa mbingu yenye nyota.

2. Na kwa siku iliyoahidiwa.

3. Na kwa shahidi na kwa anayeshuhudiwa.

4. Wameangamizwa watu wa mahandaki.

5. Moto wenye kuni.

6. Walipokuwa wamekaa hapo.

7. Nao ni mashahidi wa yale waliyoyafanya kwa Waumini.

8. Nao hawakuwachukia ila kwa sababu walimwamini Mwenyeezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa.

9. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kuona kila kitu.

10. Hakika wale wanaowafitini Waumini wanaume na Waumini wanawake, kisha hawakutubu, basi watapata adhabu ya kuungua.

11. Hakika wale Walioamini na kutenda vitendo vizuri watapata Mabustani yanayopita mito chini yake, huko ndiko kufaulu kukubwa.

12. Hakika kutesa kwa Mola wako ni kukali.

13. Hakika yeye ndiye anayeanzisha na kurudisha.

14. Naye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye mapenzi.

15- Mwenye ufalme, Mtukufu.

16. Mwingi wa kutenda alipendalo.

17. Je, imekufikia khabari ya majeshi.

18. (Ya) Firaun na Thamudi?

19. Lakini wale waliokufuru wamo katika kukadhibisha.

20. Na Mwenyeezi Mungu, kwa nyuma yao amewazunguka.

21. Bali hii ni Qur’an Tukufu.

22. Katika ubao uliohifadhiwa.