Surah Bani Israail

Sura hii imeteremshwa Makka, na ina  Aya 111.

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Utukufu ni (wake) ambaye alimpeleka mja wake usiku kutoka Msikiti Mtukufu (wa Makka) mpaka Msikiti wa mbali (wa Falastini) ambao tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake, ili tumuonyeshe baadhi ya dalili zetu. Hakika yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

2. Na tulimpa Musa Kitabu, na tukakifanya muongozo kwa wana wa Israeli (akawaambia) Msimfanye rnlinzi badala yangu.

3. (Na pia akawaambia, enyi) kizazi cha wale tuliowapandisha (katika jahazi) pamoja na Nuhu. Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani nyingi.

4. Na tukawafunulia wana wa Israeli katika Kitabu: Bila shaka mtafanya uharibifu katika nchi mara mbili, na kwa kweli mtaasi uasi mkubwa.

5. Basi ilipofika ahadi ya kwanza ya hizo mbili, tukakuleteeni watu wetu wenye mapigano makali, nao wakaingia majumbani kila upande, na ilikuwa ahadi iliyotimizwa.

6. Kisha tukakurudishieni nguvu juu yao, na tukakusaidieni kwa mali na watoto, na tukakufanyeni kundi kubwa sana.

7. Kama mkifanya wema, rntajifanyia wema nafsi zenu, na kama mkifanya ubaya, basi mtajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho (tutakuleteeni watu wenye nguvu) ili wawafanye vibaya wakubwa wenu na wauingie Msikiti kama walivyouingia mara ya kwanza na wayaangamize kabisa waliyoyashinda.

8. Huenda Mola wenu akakurehemuni, na kama mtarudia (mwendo wenu wa kwanza) sisi pia tutarudia, na tumeifanya Jahannam kuwa gereza kwa ajili ya makafiri.

9. Hakika Qur’an hii inaongoza kwenye yale yaliyonyooka kabisa, na inawapa khabari njema wenye kuamini, wafanyao vitendo vizuri, kwamba, watapata malipo makubwa.

10. Na kwamba wale wasioamini Akhera tumewaandalia adhabu yenye kuumiza.

11. Na mwanadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, na mwanadamu ni mwenye haraka sana.

12. Na tumefanya usiku na mchana, kuwa ishara mbili, kisha tumeifuta ishara ya usiku na tukaifanya ishara ya mchana iangazayo, ili mtafute fadhila

itokayo kwa Mola wenu, na mpate kujua idadi ya miaka na hesabu, na kila kitu tumekieleza wazi wazi.

13. Na kila mwanadamu tumemfungia matendo yake shingoni mwake, na tutamtolea siku ya Kiyama daftari atakayoikuta imekunjuliwa.

14. (Aambiwe) soma daftari yako. Nafsi yako inakutosha leo kukuhesabia.

15. Anayeongoka, basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake tu, na anayepotea, basi anapotea kwa hasara (ya nafsi) yake. Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine, na sisi si wenye kuwaadhibisha mpaka tumpeleke Mtume.

16. Na tunapotaka kuuangamiza mji tunawaamrisha mafisadi wake, lakini wanaendelea na maasi humo, hapo kauli ina hakiki juu yake, na tunauangamiza maangamizo makubwa.

17. Na vizazi vingapi tumeviangamiza baada ya Nuhu! na Mola wako anatosha kwa dhambi za waja wake kuwa Mwenye khabari, Mwenye kuona.

18. Anayetaka (dunia hii) ipitayo upesi, tutamharakisha humo tunayoyataka kwa yule tumtakaye, kisha tumemfanyia Jahannam, ataiingia hali akidharauliwa, (na) kufukuzwa.

19. Na aliyetaka Akhera na akaifanyia juhudi, inayoipasa, naye ni mwenye kuamini, basi hao ndio juhudi yao itakubaliwa.

20. Wote tutawasaidia hawa na hawa katika kipawa cha Mola wako, na kipawa cha Mola wako hakizuiliki (kumfikia mja wake).

21. Tazama jinsi tulivyowafadhilisha baadhi yao kuliko wengine, na bila shaka Akhera ni yenye vyeo vikubwa zaidi, na yenye fadhila kubwa zaidi.

22. Usifanye mungu mwingine pamoja na Mwenyeezi Mungu usije ukakaa hali ya kudharauliwa (na) kutupwa.

23. Na Mola wako ameamuru kuwa msimwabudu (yeyote) ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee naye yuko kwako, au wote wawili, basi usiwaambie Akh! wala usiwakemee, na useme nao kwa msemo wa heshima.

24. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: Mola  wangu! warehemu (wazazi wangu) kama walivyonilea katika utoto.

25. Mola wenu anajua sana yaliyomo nyoyoni mwenu, kama mkiwa wema, basi hakika yeye ndiye Mwenye kusamehe wenye kurejea.

26. Na umpe jamaa haki yake, na masikini na msafiri wala usitawanye (mali yako) kwa ubadhirifu.

27. Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu za mashetani na shetani ndiye mwenye kumkufuru Mola wake.

28. Na kama unatengana nao kwa kutafuta rehema ya Mola wako unayoitumai, basi sema nao kwa maneno laini.

29. Wala usifanye mkono wako (kama) uliofungwa shingoni mwako, wala usiukunjuwe mkunjuo wa kabisa, usije ukakaa hali ya kulaumiwa (na) kufilisika.

30. Hakika Mola wako humkunjulia riziki amtakaye na hudhikisha. Hakika yeye kwa waja wake ni Mwenye khabari, Aonaye.

31. Wala msiwauwe watoto wenu kwa kuogopa umasikini, sisi ndio tunaowaruzuku wao na nyinyi pia, kwani kuwaua ni kosa kubwa.

32. Wala msikaribie zinaa, hakika huo ni uchafu na ni njia mbaya.

33. Wala msiue nafsi ambayo Mwenyeezi Mungu amekataza, isipokuwa kwa haki. Na mwenye kuuawa kwa kudhulumiwa, basi tumeweka mamlaka kwa mrithi wake, hivyo asipite kiasi katika kuua, hakika yeye atasaidiwa.

34. Wala msikaribie mali ya yatima, isipokuwa kwa njia iliyobora, mpaka afikie baleghe yake, na timizeni ahadi, kwani ahadi itaulizwa.

35. Na timizeni kipimo mpimapo, na pimeni kwa mizani iliyo sawa, Hayo ni (ya) wema na bora mwishoni.

36. Wala usifuate usiyo na elimu nayo, hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa.

37. Wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika wewe huwezi kuipasua ardhi, wala huwezi kufikia urefu wa milima.

38. Hayo yote ubaya wake mbele ya Mola wako ni wenye kuchukiza.

39. Hayo ni katika yale aliyokufunulia Mola wako katika hekima, wala usimweke pamoja Mwenyeezi Mungu, mungu mwingine, usije kutupwa katika Jahannam hali ya kulaumiwa (na) kufukuzwa.

40. Je, Mola wenu amekuchagulieni watoto wanaume na (Mwenyeezi Mungu) akajichukulia watoto wanawake katika Malaika? kwa hakika nyinyi mnasema maneno makubwa.

41. Na tumekwisha eleza kila jambo katika Qur’an hii ili wapate kukumbuka, lakini haiwazidishii ila kuchukia.

42. Sema: Lau wangelikuwa pamoja naye waungu (wengine) kama wasemavyo, hapo bila shaka wangelitafuta njia ya kufikia kwa Mwenyeezi Mungu.

43. Ametakasika Mwenyeezi Mungu na ameepukana na hayo wasemayo kwa uepukano mkubwa.

44. Zinamtukuza mbingu saba na ardhi navilivyomo ndani yake, na hakuna chochote isipokuwa kinamsabihi kwa sifa zake njema, lakini nyinyi hamfahamu kutukuza kwao. Hakika yeye ni Mpole, Mwingi wa kusamehe.

45. Na unaposoma Qur’an tunatia pazia lenye kusitiri baina yako na baina ya wale wasioamini Akhera.

46. Na tumetia vifuniko nyoyoni mwao wasije wakaifahamu, na katika masikio yao mna uzito. Na unapomtaja Mola wako katika Qur’an peke yake, basi wao hugeuza migongo yao kwa chuki.

47. Tunajua sana sababu wanayo sikilizia, wanapokusikiliza, na wanaponong’ona, madhalimu wanaposema: Nyinyi hamumfuati isipokuwa mtu aliyerogwa.

48. Tazama jinsi wanavyokupigia mifano, basi wamepotea, hivyo hawawezi kupata njia.

49. Na wakasema: Je, tutakapokuwa mifupa na mapande yaliyosagika, je, tutafufuliwa kuwa viurnbe wapya?

50. Sema: Kuweni mawe au chuma.

51. Au kiumbe chochote katika vile vinavyoonekana vigumu katika nyoyo zenu (hata hivyo mtafufuliwa). Hapo watasema; Nani atakayeturudisha tena? Yule yule aliye kuumbeni mara ya kwanza! Ndipo watakutikisia vichwa vyao na watasema: Yatakuwa lini hayo? sema: Huenda yakawa karibu.

52. Siku atakapokuiteni, na nyinyi mtaitika kwa kumsifu na mtafahamu kuwa hamkukaa (duniani) ila kidogo tu.

53. Na waambie waja wangu waseme yaliyo bora, maana shetani huchochea ugomvi kati yao. Hakika shetani kwa mwanadamu ni adui dhahiri.

54. Mola wenu anakujueni sana, akipenda atakurehemuni, au akipenda atakuadhibuni. Na hatukukutuma kuwa mlinzi juu yao.

55. Na Mola wako anawajua sana wote waliomo katika mbingu na ardhi. Na kwa hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine, na Daudi tulimpa Zaburi.

56. Sema: Waiteni wale mnaodai (kuwa ni waungu) badala yake, kisha hawataweza kukuondoleeni dhara wala kubadilisha.

57. Hao wanaowaomba, (wenyewe) wanatafuta ukaribiano na Mola wao, (hata) aliye karibu sana miongoni mwao, na wanatumai rehema zake, na wanaogopa adhabu yake, Hakika adhabu ya Mola wako ni ya kuogopwa.

58. Na hakutakuwa mji wowote ila sisi tutauhilikisha kabla ya siku ya Kiyama au kuuadhibu adhabu kali, hayo yameandikwa katika Kitabu.

59. Na hakuna kinachotuzuia kuileta Miujiza (waitakayo) ila ni kuwa, watu wa zamani waliikadhibisha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa dalili dhahiri, lakini wakamkanusha, na hatupeleki Miujiza ila kwa ajili ya kuhadharisha.

60. Na (kumbuka) tulipokuambia: Hakika Mola wako amewazunguka watu. Na hatukuifanya ndoto ile tuliyokuonyesha ila kwa kuwajaribu watu, na pia mti uliolaaniwa katika Qur’an. Na tunawahadharisha lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa.

61. Na (kumbuka) tulipowaambia Malaika: Mtiini Adamu, basi wakamtii isipokuwa Iblis. Akasema: je, nimtii yule uliyemuumba kwa udongo?

62. Akasema: Unaonaje, huyu ndiye umempa heshima zaidi kuliko mimi? kama ukinipa muda mpaka siku ya Kiyama, bila shaka nitakiangamiza kizazi chake ila wachache tu.

63. (Mwenyeezi Mungu) akasema: Ondoka! Na atakayekufuata miongoni mwao, basi hakika Jahannam ndiyo malipo yenu, malipo kamili.

64. Na wavute uwezao miongoni mwao kwa sauti yako, na uwakusanyie wapandao farasi wako, na waendao kwa miguu, na shirikiana nao katika mali na watoto na uwaahidi. Lakini shetani hawaahidi ila udanganyifu.

65. Hakika wewe huna mamlaka juu ya waja wangu. Na Mola wako anatosha kuwa ni wa kutegemewa.

66. Mola wenu ni yule anayekuendesheeni majahazi katika bahari ili mtafute fadhila zake, bila shaka yeye ni Mwenye kurehemu kwenu.

67. Na inapokufikieni taabu katika bahari, hupotea wale mnaowaita isipokuwa yeye tu. Lakini anapokufikisheni salama nchi kavu, mnakataa, na mwanadamu ni mwingi wa kukanusha.

68. Je, mmesalimika kuwa hatakudidimizeni upande wa nchi kavu au hatakuleteeni tufani la kokoto kisha msipate mlinzi?

69. Au mmesalimika kuwa hatakurudisheni humo (baharini) mara nyingine na kukupelekeeni upepo mkali, na akuzamisheni kwa sababu mmekufuru, kisha hamtapata msaidizi juu yetu kwa (adhabu) hii.

70. Na hakika tumewatukuza wanadamu na tumewabeba nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku katika vitu vizuri, na tumewatukuza kuliko wengi wa wale tuliowaumba, kwa utukufu mkubwa.

71. Siku tutakapowaita kila watu pamoja na viongozi wao, basi atakayepewa daftari yake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma daftari yao, wala hawatadhulumiwa hata kidogo.

72. Na aliye kipofu katika (dunia) hii, basi atakuwa kipofu katika Akhera, na (atakuwa) aliyepoteza zaidi njia.

73. Na hakika walikaribia kukushawishi uache tuliyokufunulia ili upate kutuzulia mengineyo, na hapo bila shaka wangelikufanya rafiki.

74. Na kama tusingelikuimarisha ungelikuwa karibu kuwaelekea kidogo.

75. Hapo bila shaka tungelikuonjesha adhabu kubwa ya maisha na adhabu kubwa ya mauti, kisha usingepata msaidizi juu yetu.

76. Na kwa hakika walikaribia kukufukuza katika nchi ili wakutoe humo, na hapo wasingelikataa baada yako ila (muda) kidogo tu.

77. Ndiyo desturi ya wale tuliowatuma kabla yako katika Mitume wetu, wala hutapata mabadiliko katika desturi yetu.

78. Simamisha swala jua linapopinduka mpaka giza la usiku, na (kusoma) Qur’an alfajiri. Hakika (kusoma) Qur’an alfajiri kunakubaliwa (sana).

79. Na katika usiku amka kwa (kusoma) hiyo Qur’an ni (ibada) zaidi kwako huenda Mola wako akakuinua cheo kinachosifika.

80. Na sema: Mola wangu! niingize mwingizo mwema, na nitoe kutoka kwema, na unipe nguvu kutoka kwako zinazo saidia.

81. Na sema: Ukweli umefika na uongo umetoweka, hakika uwongo ndio wenye kutoweka.

82. Na tunateremsha Qur’an ambayo ni ponyo na rehema kwa wenye kuamini, wala hayawazidishii madhalimu ila hasara tu.

83. Na tunapomneemesha mwanadamu, hupuuza (kumkumbuka Mwenyeezi Mungu) na kujitenga upande, na inapomgusa shari hukata tamaa.

84. Sema: Kila mmoja hufanya kwa njia yake, na Mola wenu anamjua sana aliyeongoka zaidi katika njia.

85. Na wanakuuliza juu ya roho, sema; Roho imetokana na amri ya Mola wangu, nyinyi hamkupewa katika elimu (ya roho) ila kidogo.

86. Na kama tungelipenda bila shaka tungeliondoa yale tuliyokufunulia, kisha usingelipata kwa (jambo) hili mlinzi juu yetu.

87. Ila kwa rehema itokayo kwa Mola wako hakika fadhila yake iliyo juu yako ni kubwa.

88. Sema: Hata wakijikusanya watu (wote) na majinni (wote) ili kuleta mfano wa hii Qur’an hawataweza kuleta mfano wake hata kama watasaidiana wao kwa wao.

89. Na bila shaka tumewaeleza watu kwa namna nyingi katika Qur’ani hii kila mfano, lakini watu wengi zaidi wanakataa (kila kitu) isipokuwa kufru.

90. Na wakasema: Hatuwezi kukuamini mpaka utububujishie chemchem katika ardhi.

91. Au uwe na bustani ya mitende na mizabibu, kisha ukabubujishe mito katikati yake kwa mmiminiko (mkubwa).

92. Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyodai, au utuletee Mwenyeezi Mungu na Malaika uso kwa uso.

93. Au uwe na nyumba ya dhahabu au upande mbinguni, na hatutaamini kupanda kwako mpaka ututeremshie Kitabu tukisome. Sema; Mola wangu ni Mtakatifu! Mimi ni nani isipokuwa ni mwanadamu na ni Mtume tu.

94. Na hakuna lililowazuilia watu kuamini ulipowafikia uongofu isipokuwa walisema: Je, Mwenyeezi Mungu humtuma binadamu kuwa mjumbe (wake?).

95. Sema: kama katika ardhi wangelikuwa Malaika watembeao kwa utulivu, bila shaka tungeliwateremshia kutoka mbinguni Malaika kuwa Mtume (wao).

96. Sema: Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa Shahidi baina yangu na baina yenu, hakika yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.

97. Na ambaye Mwenyeezi Mungu anamuongoza, basi yeye ndiye aliyeongoka. na anayempoteza, basi wewe hutawapatia viongozi wasio kuwa yeye. Na tutawakusanya siku ya Kiyama hali ya kuwa wanakokotwa juu ya nyuso zao, na hali ya kuwa vipofu na mabubu na viziwi. Makazi yao ni Jahannam (na) kila izimikapo kidogo tutawazidishia muwako.

98. Hayo ni malipo yao kwa sababu walizikataa hoja zetu na wakasema: :-tutakapokuwa mifupa na mapande yaliyosagika tutafufuliwa kuwa viumbe wapya?

99. Je, hawakuona kwamba Mwenyeezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi ni Mwenye uwezo wa kuumba mfano wa wao? Na amewawekea muda usio na shaka, lakini madhalimu wamekataa (kila kitu) isipokuwa kukufuru.

100. Sema: Kama mngelizimiliki khazina za rehema ya Mola wangu, hapo lazima nyinyi mngelizizuia kwa kuogopa kuzitumia, na mwanadamu ni mchoyo sana.

101. Na kwa hakika tulimpa Musa hoja tisa zilizo wazi, basi waulize wana wa Israeli, alipowafikia na Firaun akamwambia; Hakika mimi nakuona ewe Musa umerogwa.

102. Akasema: Bila shaka umekwisha jua hakuna aliyeteremsha (hoja) hizi isipokuwa Mola wa mbingu na ardhi, kuwa dalili, na hakika mimi nakuona ewe Firaun, umekwisha angamia.

103. Basi (Firaun) akataka kuwafukuza katika nchi, kwa hiyo tukamzamisha yeye na waliokuwa pamoja naye wote.

104. Na tukawaambia baada yake wana wa Israeli; kaeni katika nchi, na itakapofika ahadi ya mwisho, tutakuleteni pamoja.

105. Na kwa haki tumeiteremsha (Qur’an) na kwa haki imeteremka. Na hatukukuleta ila uwe mtoaji wa khabari njema na muonyaji.

106. Na Qur’an tumeigawanya ili uwasomee watu kwa kituo, na tumeiteremsha kidogo kidogo.

107. Sema: Muiamini au msiiamini. Hakika wale waliopewa elimu kabla yake wanaposomewa (Qur’an) huanguka kifudifudi kwa kusujudu.

108. Na wanasema Mola wetu ni Mtakatifu, hakika ahadi ya Mola wetu ndio itimizwayo.

109. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidishia unyenyekevu.

110. Sema: Muombeni Mwenyeezi Mungu au muombeni Rahmani kwa jina lolote mnalomwita, kwani ana Majina mazuri. Wala usiiseme swala yako kwa sauti kubwa, wala usiiseme kwa sauti ndogo, bali shika njia baina ya hizo.

111. Na sema; Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu ambaye hakujifanyia mtoto wala hana mshirika katika ufalme, wala hana rafiki kwa sababu ya udhaifu, na mtukuze kwa matukuzo makubwa.