Sura hii imeteremshwa Makka, Aya 206
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Alif Lam Mym Swad
2. (Hii Our’an ni) Kitabu kilichoteremshwa kwako, basi isiwe dhiki kifuani kwako kwa ajili yake, ili upate kuonya kwacho, na kiwe ni mawaidha kwa walioamini.
3. Fuateni mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu, wala msifuate viongozi (wengine) badala yake, ni kidogo mnayoyakumbuka.
4. Na Vijiji vingapi tuliviangamiza na ilivifikia adhabu yetu usiku au adhuhuri walipokuwa wamelala.
5. Basi hakikuwa kilio chao ilipowafikia adhabu yetu isipokuwa kusema: Bila shaka sisi tulikuwa madhalimu.
6. Na kwa hakika tutawauliza wale waliopelekewa (Mitume) na tutawauliza (pia) waliotumwa (Mitume).
7. Tena kwa hakika tutawasimulia kwa elimu wala hatukuwa mbali.
8. Na siku hiyo kipimo kitakuwa sawa, basi watakaokuwa na uzani mzito hao ndio watakaofaulu.
9. Na watakao kuwa na uzani khafifu, basi hao ndio waliozitia khasara nafsi zao kwa sababu walikuwa wakizifanyia jeuri Aya zetu.
10. Na bila shaka tumekukalisheni katika ardhi na tumekuwekeeni humo vitu vya maisha ni shukrani ndogo tu mnazotoa.
11. Na hakika tulikuumbeni kisha tukakutieni sura kisha tukawaambia Malaika: Msujudieni Adamu. Basi wakasujudu isipokuwa Iblis, hakuwa miongoni mwa waliosujudu.
12. (Mwenyeezi Mungu) akasema: Nini kilichokuzuia kumsujudia nilipokuamrisha? Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.
13. Akasema (Mwenyeezi Mungu) Basi ondoka humo, haikufai kufanya kiburi humo, toka, hakika wewe u miongoni mwa walio duni.
14. Akasema: Nipe muda (nisife) mpaka siku watakapofufuliwa.
15. Akasema: (Mwenyeezi Mungu) Utakuwa miongoni mwa waliopewa muda.
16. Akasema: Kwa sababu umenihukumu mpotovu kwa hakika nitawakalia (waja wako) katika njia yako iliyonyooka.
17. Kisha nitawafikia kwa mbele yao na nyuma yao na kuliyani kwao na kushotoni kwao, wengi katika wao hutawakuta ni wenye kushukuru.
18. Akasema (Mwenyeezi Mungu) Toka humo, hali ya kuwa ni mwenye kudharauliwa na mwenye kufukuzwa, atakaye kufuata miongoni mwao, (nitamtia Motoni) niijaze Jahannam kwa nyinyi nyote.
19. Na ewe Adamu! Kaa wewe na mkeo katika bustani na kuleni mnapopenda, wala msiukaribie mti huu msije kuwa miongoni mwa waliodhulumu.
20. Basi shetani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizofichiwa, na akasema: Mola wenu hakukukatazeni mti huu ila msije kuwa Malaika au kuwa miongoni mwa wakaao milele.
21. Naye akawaapia (kuwaambia) kwa hakika mimi ni mmoja wa watoao shauri njema kwenu.
22. Basi akawateka (wote wawili) kwa udanganyifu, na walipouonja mti ule, tupu zao zikawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya (miti ya huko) Peponi. Na Mola wao akawaita: je, sikukatazeni mti huo na kukwambieni kwamba shetani ni adui yenu dhahiri?
23. Wakasema: Mola wetu! tumedhulumu nafsi zetu, na kama hutusamehe na kuturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye khasara.
24. Akasema: Shukeni, nyinyi kwa nyinyi ni maadu. Na makao yenu yatakuwa katika ardhi, na posho kwa muda.
25. Akasema: Mtaishi humo na mtafia humo na mtatolewa humo.
26. Enyi wanadamu! hakika tumekuteremshieni nguo zifichazo tupu zenu na nguo za mapambo, na nguzo za ucha Mungu ndio bora. Hayo ni katika dalili za Mwenyeezi Mungu ili wapate kukumbuka.
27. Enyi wanadamu! shetani asikutieni katika fitina, kama alivyowatoa wazee wenu katika Pepo, akawavua nguo zao ili kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye pamoja na kabila yake wanakuoneni hali ya kuwa hamuwaoni. Bila shaka sisi tumewajaalia mashetani kuwa marafiki wa wale wasioamini.
28. Na wanapofanya uchafu husema; Tumewakuta nayo baba zetu na Mwenyeezi Mungu ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyeezi Mungu haamrishi mambo mabaya. Je, mnasema juu ya Mwenyeezi Mungu msiyoyajua?
29. Sema: Mola wangu ameamrisha uadilifu, na elekezeni nyuso zenu wakati wa kila swala na muabuduni yeye tu kwa utii khalisi, kama alivyokuumbeni kwanza ndivyo mtakavyorudi.
30. Ameliongoza kundi moja na kundi jingine limethubutikiwa na upotovu kwa sababu wao waliwafanya mashetani kuwa viongozi (wao) badala ya Mwenyeezi Mungu, na wanadhani kuwa wao wameongoka.
31. Enyi wanadamu! (Waislamu) chukueni, pambo lenu kila mahala wakati wa ibada na kuleni (vizuri) na kunyweni (vizuri) wala msipite kiasi, hakika yeye hawapendi wapitao kiasi.
32. Sema: Ni nani aliyeharamisha mapambo ya Mwenyeezi Mungu ambayo amewatolea waja wake na vitu vizuri vya riziki? sema: Vitu hivyo ni kwa waumini katika maisha ya dunia (na) khasa siku ya Kiyama. Hivyo ndivyo tunavyo zibainisha Aya kwa watu wanaojua.
33. Waambie’. Mola wangu ameharamisha mambo machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika, na dhambi na uasi pasipo haki, na kumshirikisha Mwenyeezi Mungu na ambacho hakukiteremshia dalili, na kusema juu ya Mwenyeezi Mungu msiyo yajua.
34. Na kila umati una muda, basi utakapowafikia muda wao hawatakawia hata saa moja wala hawatatangulia.
35. Enyi wanadamu! iwapo watakufikieni Mitume miongoni mwenu, wanakuelezeni Aya zangu, basi watakaomcha (Mungu) na kufanya wema. haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
36. Na wale wanaokadhibisha Aya zetu na kuzifanyia kiburi, hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.
37. Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uongo Mwenyeezi Mungu au anayezikadhibisha Aya zake? Hao itawafikia sehemu yao aliyowaandikia (Mwenyeezi Mungu) mpaka watakapo wafikia wajumbe wetu kuwafisha, watasema: Wako wapi mliokuwa mkiwaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu? Watasema: Wametupotea, na watajishuhudia wenyewe kwamba hakika wao walikuwa makafiri.
38. Atasema: Ingieni Motoni pamoja na umma zilizopita kabla yenu za Majini na watu, kila utakapoingia umati utawalaani wenzao, mpaka watakapokusanyika wote humo, wa nyuma wao watasema kwa ajili ya wa kwanza wao: Mola wetu! hawa ndio walio tupoteza, basi wape adhabu ya Moto mara dufu, atasema: Kwa nyinyi nyote ni (adhabu) mara dufu, lakini nyinyi hamjui.
39. Na wa kwanza wao watawaambia wa nyuma wao. Basi nyinyi pia hamkuwa na ubora kuliko sisi, kwa hiyo onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyachuma.
40. Hakika wale waliokadhibisha Aya zetu na kuzifanyia kiburi, hawatafunguliwa milango ya mbingu wala hawataingia Peponi mpaka apite ngamia katika tundu ya sindano, na hivi ndivyo tunavyowalipa waovu.
41. Watakuwa na kitanda cha Jahannam, na juu yao nguo za kujifunika (za Moto wa Jahannam) na hivi ndivyo tunavyo walipa madhalimu.
42. Na wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, hatumkalifishi mtu yeyote ila kwa kiasi cha uweza wake hao ndio watu wa Peponi, wao humo watakaa milele.
43. Na tutaiondoa chuki yote vifuani mwao, chini yao itapita mito, na watasema: Kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu. Ambaye aliyetuongoza kufikia haya wala hatukuwa wenye kuongoka kama Mwenyeezi Mungu hakutuongoza. Bila shaka Mitume wa Mola wetu walileta haki. Na watanadiwa ya kwamba hii ndiyo Pepo mliyorithishwa kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafanya.
44. Na watu wa Peponi watawaita watu wa Motoni (waseme) sisi tumekuta aliyotuahidi Mola wetu kuwa ni kweli. Je, nyinyi pia mmekuta aliyowaahidini Mola wenu kuwa ni kweli? Watasema (watu wa Motoni) ndiyo. Mara mtangazaji atatangaza baina yao (aseme): Laana ya Mwenyeezi Mungu iko juu ya madhalimu.
45. Ambao wanazuilia njia ya Mwenyeezi Mungu na wanataka kuipotosha, nao hawaiamini Akhera.
46. Na kati ya hao wawili (watu wa Peponi na watu wa Motoni kutakuwa na) pazia, na juu ya mahala palipoinuka patakuwa watu watakaowafahamu wote kwa alama zao, na watawaita watu wa Peponi (waseme): Amani iwe juu yenu. Hawajaingia humo, (Peponi) nao wanatumai.
47. Na macho yao yanapogeuzwa kwenye watu wa Motoni, husema: Mola wetu, usituweke pamoja na watu madhalimu.
48. Na watu wa mahala palipoinuka watawaita watu wanaowafahamu kwa alama zao, watasema: Haukukusaidieni wingi wenu wala mlivyokuwa mkijivunia.
49. Je, hawa ndio wale mliokuwa mkiwaapia kwamba Mwenyeezi Mungu hatawafikishia rehema? Ingieni Peponi, hakuna khofu juu yenu, wala hamtahuzunika.
50. Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi (kuwaambia) Mtumwagie maji au katika vile alivyokupeni Mwenyeezi Mungu. Watasema: Hakika Mwenyeezi Mungu ameviharimisha vyote viwili kwa makafiri.
51. Ambao waliifanya dini yao kuwa u puuzi na mchezo, na maisha ya dunia yakawadanganya. Basi leo sisi tunawasahau kama walivyosahau mkutano wa siku yao hii na kwa sababu walikuwa wakizikana Aya zetu.
52. Na bila shaka tumewaletea Kitabu tulichokibainisha kwa elimu, ni muongozo na rehema kwa watu wanaoamini.
53. Hawatazamii ila matokeo yake, siku yatakapotokea matokeo yake, watasema wale walio isahau zamani: Kwe1i Mitume wa Mola wetu walileta haki. Je, tunao waombezi ili watuombee? au tutarudishwa ili tufanye yasiyokuwa yale tuliyokuwa tukiyafanya? Bila shaka wamezitia khasarani nafsi zao, na umewapotea ule uongo waliokuwa wakiutunga.
54. Hakika Mola wenu ni Mwenyeezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika nyakati sita, kisha ukakamilika (uumbaji wake) katika Arshi. Huufunika usiku kwa mchana uufuatiao upesi, na jua na mwezi na nvota vimetiishwa kwa amri yake. Fahamuni kuumba na amri zote ni zake. Ametukuka Mwenyeezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
55. Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika yeye hawapendi warukao mipaka.
56. Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa, na muombeni kwa kuogopa na kwa kutumai, hakika rehema ya Mwenyeezi Mungu iko karibu na wanaofanya mema.
57. Na yeye ndiye apelekaye pepo kuwa khabari njema kabla ya kufika rehema yake (mvua) Hata zinapobeba wingu zito tunalisukuma kwenye mji ulokufa, kisha tunateremsha maji kwa (wingu) hilo na kwa hayo tunaotesha kila aina ya matunda, hivyo ndivyo tutakavyo wafufua wafu ili mpate kukumbuka.
58. Na nchi nzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake, na iliyo mbaya haioti ila kwa taabu tu, hivyo ndivyo tunavyoeleza Aya kwa watu wanaoshukuru.
59. Hakika tulimpeleka Nuhu kwa watu wake, akawaambia: Enyi watu wangu! mwabuduni Mwenyeezi Mungu nyinyi hamna Mungu ila yeye, hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya siku iliyo kuu.
60. Wakuu wa watu wake wakasema: Sisi tunakuona umo katika upotovu ulio dhahiri.
61. Akasema: Enyi kaumu yangu! mimi simo katika upotovu lakini mimi ni Mtume nitokae kwa Mola wa walimwengu.
62. Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu na nina kunasihini na ninayajua kutoka kwa Mwenyeezi Mungu msiyoyajua.
63. Je, mnastaajabu kukufikieni mawaiddha kutoka kwa Mola wenu kwa njia ya mtu aliye ni mmoja wenu, ili akuonyeni na ili muogope na mpate kurehemewa.
64. Walimkadhibisha, basi tukamuokoa yeye na waliokuwa pamoia naye katika jahazi, na tukawazamisha wale waliozikadhibisha Aya zetu, hakika hao walikuwa watu vipofu.
65. Na kwa Adi (tulimpeleka) ndugu yao Hudi, akawaambia: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Mwenyeezi Mungu, nyinyi hamna Mungu ila yeye tu, basi hamuogopi?
66. Wakasema wakuu waliokufuru katika kaumu yake: Sisi tunakuona umo katika upumbavu na kwa hakika tunakuona u miongoni mwa waongo.
67. Akasema: Enyi kaumu yangu! mimi sina upumbavu, lakini mimi ni Mtume kutoka kwa Mola wa walimwengu.
68. Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu, na mimi kwenu ni mwenye kukunasihini, muaminifu.
69. Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu kwa njia ya mtu aliye mmoja wenu ili akuonyeni? Na kumbukeni alipowafanyeni makhalifa baada ya watu wa Nuhu na amewazidishieni nguvu katika umbo, basi mzikumbuke, neema za Mwenyeezi Mungu ili mpate kufaulu-
70. Wakasema; je, umetujia ili tumwabudu Mwenyeezi Mungu peke yake na tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee unayotuahidi ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.
71. Akasema: Bila shaka adhabu na ghadhabu zimekwisha kukuangukieni kutoka kwa Mola wenu. Je, mnanijadili katika majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo Mwenyeezi Mungu hakuyateremshia dalili? basi ngojeni, mimi ni pamoja nanyi katika wangojao.
72. Basi tukamuokoa yeye na waliokuwa pamoja naye kwa rehema zetu, na tukakata mizizi ya wale walio zikadhibisha Aya zetu, na hawakuwa wenye kuamini.
73. Na kwaThamudi (tulimpeleka) ndugu yao Saleh, akawaambia: Enyi watu wangu! muabuduni Mwenyeezi Mungu, nyinyi hamna Mungu ilaYeye: Hakika umekwisha kukufikieni Muujiza ulio dhahiri kutoka kwa Mola wenu. Huyu ni ngamia jike wa Mwenyeezi Mungu aliye na Ishara kwenu (ya Utume wangu) basi muacheni ale katika ardhi ya Mwenyeezi Mungu, wala msimtie dhara, isije ikakushikeni adhabu iumizayo.
74. Na kumbukeni alipowafanyeni makhalifa baada ya Adi na kukuwekeni (vizuri) katika ardhi, mkajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake na mkachonga majumba katika majabali. Basi zikumbukeni neema za Mwenyeezi Mungu, wala msiasi ardhini kwa kufanya uharibifu.
75. Wakasema wakuu wa kaumu yake waliotakabari, kuwaambia wale walio dhaifu wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnajua kwamba Saleh ametumwa na Mola wake? wakasema: Hakika tunayaamini yale aliyotumwa nayo.
76. Wakasema wale waliotakabari: Sisi tunayakataa yale mnayoyaamini.
77. Na wakamuua yule ngamia na wakaasi amri ya Mola wao na wakasema:
Rv/eSaleh! tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume.
78. Na tetemeko (la ardhi) likawanyakua na wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekwisha kufa.
79. Basi (Saleh) akawaacha na akasema: Enyi kaumu yangu! bila shaka nimekufikishieni ujumbe wa Mola wangu na nimekunasihini, lakini nyinyi hamuwapendi wenye nasaha.
80. Na (tulimpeleka ) Luti alipowaambia kaumu yake: Je, mnafanya uchafu ambao hajakutangulieni yeyote kwa (ufasiki) huo katika walimwengu?
81. Hakika nyinyi mnafika kwa wanaume kwa kuwaingilia badala ya wanawake, ama nyinyi ni watu wafujaji.
82. Na hayakuwa majibu ya kaumu yake isipokuwa kusema: Wafukuzeni katika mji wenu, kwa sababu wao ni watu wanao jitakasa.
83. Basi tukamuokoa yeye (Luti) na watu wake isipokuwa mke wake, alikuwa miongoni mwa waliokuwa nyuma.
84. Na tukawapigishia mvua (ya adhabu) basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa waovu.
85. Na kwa watu wa Madyana (tulimpeleka) ndugu yao Shua’yb akawaambia:
Enyi kaumu yangu! muabuduni Mwenyeezi Mungu, hamna Mungu ilaYeye. Zimekwisha kukufikieni hoja dhahiri kutoka kwa Mola wenu, basi kamilisheni kipimo (cha kibaba) na mizani (pia) wala msiwapunguzie watu vitu vyao wala insifanye uharibifu katika ardhi baada ya kuwa imekwisha tengenea, hivyo ni bora kwenu ikiwa nyinyi mmeamini.
86. Wala msikae katika kila njia kuogopesha (watu) na kuwazuilia na dini ya Mwenyeezi Mungu wale wenye kuamini, na kutaka kuipotosha. Na kumbukeni mlipokuwa wachache, na akakufanyeni kuwa wengi, na tazameni jinsi ulivyokuwa mwisho wa waharibifu.
87. Na ikiwa liko taifa miongoni mwenu lililoamini yale niliyotumwa nayo, na taifa (jingine) halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyeezi Mungu ahukumu kati yetu, naye ndiye Mbora wa wenye kuhukumu.
88. Wakuu waliotakabari katika kaumu yake wakasema: Ewe Shuay’b lazima tutakutoa wewe na wale walioamini pamoja nawe katika mji wetu, au huna budi kurudi katika mila yenu, akasema, Je, ingawa tunaichukia?
89. Bila shaka tumemzulia Mwenyeezi Mungu uongo ikiwa tutarudi katika mila yenu, baada ya Mwenyeezi Mungu kutuokoa nayo, wala hatuwezi kuirudia isipokuwa akitaka (jambo) Mwenyeezi Mungu Mola wetu (huwa), Mola wetu amekienea kila kitu kwa elimu, kwa Mwenyeezi Mungu tunategemea. Mola wetu! jukumu baina yetu na baina ya wenzetu kwa haki nawe ndiye Mbora wa wanaohukumu.
90. Na wakuu walio kufuru katika kaumu yake wakasema ikiwa nyinyi mtamfuata Shua’yb hapo bila shaka mtakuwa wenye khasara.
91. Basi tetemeko (la ardhi) likawanyakua na wakaamkia majumbani rnwao wamejifudikiza, wamekwisha kufa.
92. Wale waliomkadhibisha Shua’yb wakawa kama kwamba hawakuwamo, wale walomkadhibisha Shuayb) ndio waliokuwa wenye khasara.
93. Basi akawaachilia mbali na akasema; Enyi kaumu yangu! bila shaka nimekufikishieni ujumbe wa Mola wangu na nimekupeni nasaha, basi vipi nihuzunike juu ya makafiri?
94. Na hatukumleta Nabii yeyote katika mji wowote (akakadhibishwa) isipokuwa tuliwatesa wakazi wake kwa taabu na mashaka ili wapate kunyenyekea.
95. Kisha tukabadilisha mahala pa ubaya kwa wema, hata wakazidi, na wakasema; Taabu na raha ziliwafikia baba zetu, basi tukawaangamiza kwa ghafla, hali ya kuwa hawatambui.
96. Na kama watu wa miji wange amini na kumcha (Mwenyeezi Mungu) lazima tungeliwafungulia baraka za mbingu na ardhi, lakini walikadhibisha, tukawaangamiza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
97. Je, watu wa miji wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafikia usiku hali wakiwa wamelala?
98. Au watu wa miji wameaminisha kuwa adhabu yetu haitawafikia mchana hali wanacheza?
99. Je, wamesalimika kuadhibiwa na Mwenyeezi Mungu? Hawaaminishi adhabu ya Mwenyeezi Mungu ila watu (ambao watakuwa) wenye khasara.
100. Je, haiwaongozi wale ambao wanairithi ardhi baada ya wakazi wake kwamba tukitaka tutawatia (msiba) kwa dhambi zao na tutapiga muhuri juu ya nyoyo zao kwa hiyo hawatasikia?
101. Hiyo ni miji tunakusimulia baadhi ya khabari zake, na bila shaka Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo wazi, lakini hawakuwa wenye kuamini waliyoyakadhibisha zamani. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyozipiga muhuri nyoyo za makafiri.
102. Na kwa wengi wao hatukuona (kutekeleza) ahadi yoyote, bali kwa hakika wengi wao tuliwakuta wapotovu.
103. Kisha baada ya (Mitume hao) tukampeleka Musa na hoja zetu kwa Firaun na watu wake. Lakini wakazikataa basi tazama jinsi ulivvokuwa mwisho wa waharibifu.
104. Na akasema Musa: Ewe Firaun! kwa hakika mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu.
105. Yanipasa nisiseme juu ya Mwenyeezi Mungu isipokuwa haki. Kwa hakika nimekufikieni kwa dalili zilizo wazi zitokazo kwa Mola wenu, basi wapeleke wana wa Israeli pamoja nami.
106. (Firaun) akasema: Kama umekuja na hoja basi ilete ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.
107. Ndipo akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka dhahiri.
108. Na akatoa mkono wake, mara ukawa mweupe kwa watazamao.
109. Wakasema wakuu wa kaumu ya Firaun hakika huyu ni mchawi mjuzi.
110. Anataka kukutoeni katika ardhi yenu, basi mnatoa shauri gani?
111. Wakasema: Muwache kidogo yeye na ndugu yake, na watume wakusanyao katika miji.
112. Wakuletee wachawi wote wajuzi.
113. Na wakaja wachawi kwa Firaun, wakasema: Hakika tutapata malipo ikiwa tutashinda.
114. Akasema: Naam Nanyi bila shaka mtakuwa miongoni mwa wanaokaribishwa.
115. Wakasema: Ewe Musa! ama utatupa wewe au tutakuwa sisi watupao (kwanza).
116. Akasema: Tupeni Basi walipotupa wakayaroga macho ya watu, wakawaogopesha na wakaleta uchawi mkubwa.
117. Na tukampelekea Wahyi Musa kuwa: Tupa fimbo yako. Mara ikavimeza walivyovizua.
118. Basi ukweli ukasimama na yakaharibika waliyokuwa wakiyatenda.
119. Kwa hiyo walishindwa hapo, na wakawa wenye kudhalilika.
120. Na wachawi wakaangushwa wakisujudu.
121. Wakasema: Tumemuamini Mola wa walimwengu.
l 22. Mola wa Musa na Haruni.
123. Akasema Firaun: Oh! mmemwamini kabla sijawaruhusuni? hakika hii ndiyo hila mliyofanya mjini ili muwatoe humo wenyeji wake, lakini hivi karibuni mtajua.
124. Lazima nitaikata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitakusulubuni nyote.
125. Wakasema: Hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu.
126. Nawe hutufanyii kisasi ila kwa sababu tumeziamini hoja za Mola wetu zilipotufikia. Mola wetu! tumiminie uvumilivu na utufishe hali ya kuwa Waislaamu.
127. Na wakasema wakuu wa kaumu ya Firaun, Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi na kukuacha wewe na waungu wako? Akasema: Tutawaua wavulana wao na tutawaacha hai wanawake wao, na bila shaka sisi ni wenye nguvu juu yao.
128. Musa akawaambia kaumu yake: Ombeni msaada kwa Mwenyeezi Mungu na vumilieni. Hakika ardhi ni ya Mwenyeezi Mungu atamrithisha amtakaye katika waja wake, na mwisho (mwema) ni kwa wamchao.
129. Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia na baada ya wewe kutujia. (Musa) akasema: Huenda Mola wenu atamwangamiza adui yenu na kukufanyeni watawala katika nchi na aone jinsi mtakavyofanya.
130. Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firaun kwa miaka (ya njaa) na upungufu wa matunda ili wapate kukumbuka.
131. Ulipowafikia wema, wakasema: Huu ni kwa ajili yetu. Na ukiwafikia ubaya humnasibishia ukorofi huo Musa na walio pamoja naye. Sikilizeni hakika ukorofi wao ni kwa Mwenyeezi Mungu lakini wengi wao hawajui.
132. Na wakasema: Dalili yoyote utakayotuletea ili uturoge kwayo hatutakuamini.
133. Ndipo tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa dalili mbali mbali lakini wakatakabari na walikuwa watu wabaya.
134. Na ilipowaangukia adhabu, wakasema: Ewe Musa! tuombee kwa Mola wako yale aliyokuahidi, kama ukituondolea adhabu, bila shaka tutakuamini na kwa hakika tutawapeleka wana wa Israeli pamoja nawe.
135. Lakini tulipowaondolea adhabu, mpaka muda fulani wao waufikie mara wakavunja ahadi.
136. Uasi tukalipiza kisasi kwao na tukawazamisha baharini kwa sababu walizikadhibisha Aya zetu na wakaghafilika nazo.
137. Na tukawarithisha watu waliokuwa wanaonekana dhaifu mashariki ya ardhi na magharibi yake ambayo tuliitia baraka (nyingi) na likatimia neno jema la Mola wako kwa wana wa Israeli kwa sababu walivumilia, na tukayaangamiza yale aliyokuwa ameyatengeneza Firaun na watu wake, na (pia) yale waliyokuwa wakiyajenga.
138. Na tukawavusha wana wa Israeli bahari , na wakafikia watu waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao. Wakasema Ewe Musa! tufanyie waungu, kama (wao) walivyo na miungu. (Musa) akasema: Hakika nyinyi ni watu mfanyao ujinga.
139. Hakika wanayoyashika hawa yataangamia na ni bure waliyokuwa wakiyafanya.
140. Akasema: Je, nikutafutieni mungu badala ya Mwenyeezi Mungu hali yeye amekufadhilisheni juu ya walimwengu?
141. Na (kumbukeni) tulipokuokoeni kwa watu wa Firaun waliokupeni adhabu mbaya, wakiwaua wavulana wenu na kuwacha hai wanawake wenu, na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa uliotoka kwa Mola wenu.
142. Na tulimwahidi Musa siku thelathini na tukazitimiza kwa kumi, ndipo ikatimia miadi ya Mola wake ya siku arobaini. Na Musa akamwambia ndugu yake Haruni: Shika mahala pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya waharibifu.
143. Na Musa alipofika kwenye miadi yetu na Mola wake akazungumza naye, (Musa) akasema; Molawangu! nionyeshe ili nikuone. Akasema. Huwezi kuniona, lakini tazama jabali, kama litakaa mahala pake ndipo utaniona. Basi Molawake alipoonyesha (Nuru yake) kwenye jabali akalifanya kuvunjika vunjika, na Musa akaanguka hali ya kuzimia, na alipozindukana akasema: Wewe ndiye Mtukufu, natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa wanaoamini.
144. Akasema: Ewe Musa! hakika nimekuchagua juu ya watu kwa ujumbe wangu na maneno yangu. Basi pokea niliyokupa na uwe miongoni mwa wanaoshukuru.
145. Na tukamwandikia katika mbao mawaidha ya kila namna, na maelezo ya kila jambo. Basi yashike kwa imara na uwaamrishe watu wako washike yaliyo bora katika hayo, nitakuonyesheni makao ya wavunjao amri.
146. Nitawaepusha na Aya zangu wale wanaotakabari katika nchi pasipo haki, na kila hoja wanayoiona hawaiamini, na kama wakiiona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia, lakini wakiiona njia ya upotovu wanaishika kuwa ndiyo njia hayo ni kwa sababu ya kuzikadhibisha Aya zetu na wameghafilika nazo.
147. Na wale walio zikadhibisha Aya zetu na mkutano wa mwisho, vitendo vyao vimeharibika, hawatalipwa ila yale yale waliyokuwa wakiyatenda.
148. Na baada yake watu wa Musa wakafanya katika mapambo yao kiwiliwili cha ndama kilichokuwa na sauti. Je, hawakuona kuwa yeye hasemi nao wala hawaongozi njia? walimfanya (mungu) na wakawa wenye kudhulumu.
149. Na walipojuta na wakaona kuwa wamekwishapotea, wakasema: Kama asingeturehemu Mola wetu na kutusamehe, bila shaka tungelikuwa miongoni mwa wapatao khasara.
150. Na Musa aliporudi kwa watu wake, hali ya kukasirika (na) masikitiko, akasema: Ni maovu mliyonifanyia nyuma yangu. Je, mmeiharakia amri ya Mola wenu? na akazitupa zile mbao na akakamata kichwa cha nduguye kukivutia kwake akasema: Ewe mwana wa mama yangu! hakika watu (hawa) wamenidharau, na hata walikaribia kuniua, basi usiwafurahishe maadui juu yangu, wala usiniweke pamoja na watu madhalimu.
151. Akasema (Musa) Mola wangu! nisamehe mimi na ndugu yangu, na utuingize katika rehema yako, wewe ndiye Mwenye kurehemu zaidi kuliko wenye kurehemu.
152. Hakika wale waliomfanya ndama (kuwa mungu) zitawafikia ghadhabu zinazotoka kwa Mola wao na udhalili kama maisha ya dunia na hivyo ndivyo tunavyowalipa wazushi.
L53. Na wale waliofanya mabaya, kisha wakatubu baada yake na kuamini hakika Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
154. Na ilipotulia ghadhabu ya Musa akazichukua zile mbao na katika maandiko yake ulikuwamo uongofu na rehema kwa wale wanaomuogopa Mola wao.
155. Na Musa akawachagua watu sabini katika kaumu yake kwa miadi yetu, na lilipowashika tetemeko (la nchi) akasema: Mola wangu! kama ungetaka ungeliwaangamiza wao na mimi zamani. Je, unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyofanya wapumbavu katika sisi? hayakuwa haya ila ni majaribio yako, kwayo humpoteza umtakaye na humuongoza umtakaye, wewe ndiye Kiongozi wetu, basi tusamehe na uturehemu, na wewe ndiye Mbora wa kusamehe.
156. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika Akhera, sisi tunarejea kwako. Akasema. Adhabu yangu nitamfikishia nimtakaye, na rehema yangu imeenea kila kitu, basi nitaiandika kwa ajili ya wale wanaomcha (Mwenyeezi Mungu) na kutoa zaka na wanaoziamini Aya zetu.
157. Ambao wanamfuata Mtume, Nabii aliyoko Makka, ambaye wanamuona ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, ambaye anawaamrisha mema na anawakataza yaliyo mabaya na kuwahalalishia vizuri na kuwaharamishia maovu, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomwamini yeye na kumtukuza na kumsaidia na wakaifuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye, hao ndio wenye kufaulu.
158. Waambie: (Muhammad); Enyi watu! hakika mimi ni Mtume wa Mwenyeezi Mungu kwenu nyote, ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi, hapana aabudiwaye ila Yeye tu, Ahuishaye na Afishaye. Basi mwaminini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake Nabii aliyoko Makka, ambaye anamwamini Mwenyeezi Mungu na maneno yake, na mfuateni ili mpate kuongoka.
159. Na katika kaumu ya Musa, wako watu wanaoongoza kwa haki, na kwa haki hiyo wanafanya uadilifu.
160. Na tuliwagawanya makabila kumi na mbili, mataifa mbali mbali. Na Tukampa Wahyi Musa, walipomuomba maji watu wake kuwa: Pigajiwe kwa fimbo yako. Mara zikabubujika chem chem kumi na mbili, na kila watu wakajua mahala pao pa kunywea. Na tukawafunika kivuli kwa mawingu na tukawateremshia Manna na Salwa kuleni katika vitu vizuri tulivyokupeni, wala hawakutudhulumu sisi, bali walikuwa wamejidhulumu wenyewe.
161. Na (kumbukeni) walipoambiwa: Kaeni katika mji huu na humo kuleni popote mpendapo, na semeni; Tufutie dhambi zetu, na ingieni mlangoni kwa unyenyekevu, tutakusameheni makosa yenu tutawazidishia (mema) watendao mema.
162. Lakini wale waliodhulumu miongoni mwao alibadilisha kauli isiyokuwa ile waliyoambiwa. Basi tukawapelekea adhabu kutoka mbinguni kwa sababu walikuwa wakidhulumu.
163. Na waulizeni habari za mji ambao ulikuwa kando ya bahari, walipokuwa wakivunja (sheria ya) Jumamosi, samaki wao walipowajia juu juu siku ya Jumamosi yao, na siku isiyokuwa Jumamosi hawakuwa wakiwajia. Hivyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakiasi.
164. Na baadhi ya watu kati yao waliposema: Kwanini mnawaonya watu ambao Mwenyeezi Mungu atawaangamiza au atawaadhibu kwa adhabu kali wakasema: Tupate kuwa na udhuru mbele ya Mola wenu, na huenda wakamcha (Mwenyeezi Mungu).
165. Basi walipoyasahau waliyokuwa wakikumbushwa, tuliwaokoa wale waliokuwa wakikataza maovu, na tukawatesa wale waliodhulumu kwa adhabu mbaya kwa sababu walikuwa wakiasi.
166. Na walipokataa kuyaacha waliyokatazwa tukawaambia: Kuweni manyani madhalili.
167. Na (kumbukeni) alipotangaza Mola wako lazima atawapelekea mpaka siku ya Kiyama ambao watawaadhibu kwa adhabu mbaya. Hakika Mola wako ni Mwepesi wa kuadhibu, na bila shaka yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
168. Na tukawafarikisha (Mayahudi) katika ulimwengu makundi makundi, wako katika wao watu wema, na wengine katika wao ni kinyume cha hao. Na tukawajaribu kwa mema na mabaya ili wapate kurejea.
169. Basi kikafuatia nyuma yao kizazi kibaya waliorithi Kitabu, wanachukua vitu vya dunia hii ya karibu, na wanasema: Tutasamehewa na kama vitu vingine vya namna hii vikiwafikia watavichukua. Je, hawakufanywa ahadi katika kitabu kuwa hawatasema juu ya Mwenyeezi Mungu ila haki? nao wamekwisha soma yaliyomo humo, na nyumba ya Akhera ni bora kwa wale wanaomcha (Mwenyeezi Mungu). Je hamfahamu?
170. Na wale wanaokishika Kitabu na wanasimamisha swala, (tutawalipa mema) hakika sisi hatupotezi malipo ya wafanyao mema.
171. Na (kumbukeni) tulipoung’oa mlima (tukauning’iniza) juu yao kama kwamba ni kivuli, na wakadhani kwamba utawaangukia. (Tukawaambia):
Shikeni kwa nguvu tuliyokupeni na yakumbukeni yaliyomo ili mpate kumcha (Mwenyeezi Mungu).
172. Na (kumbuka) Mola wako alipowaleta katika wanadamu kutoka miongoni mwao kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi zao: Je mmi siye Mola wenu? wakasema: Ndiye, tunashuhudia (kuwa wewe ndiye mola wetu) msije mkasema siku ya Kiyama, hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo.
173. Au mkasema: Baba zetu ndio walioshirikisha zamani, nasi tulikuwa kizazi nyuma yao, je utatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wapotovu?
174. Na hivyo ndivyo tunavyozipambanua Aya (zetu) na huenda wao watarejea.
175. Na wasomee khabari za yule tuliyempa Aya zetu, kisha akajivua nazo, na shetani akamfuata na akawa miongoni mwa waliopotea.
176. Na kama tungelitaka tungelimwinua kwazo, lakini yeye akagandamana kwenye ardhi na kuyafuata matamanio yake. Basi hali yake ni kama hali ya mbwa, ukimpigia kelele anahema au ukimwacha (pia) anahema. Hivyo ndivyo hali ya watu waliozikadhibisha Aya zetu, basi simulia hadithi huenda watafikiri.
177. Uovu ulioje wa mfano wa wanaozikadhibisha Aya zetu na wakajidhulumu nafsi zao?
178. Mwenyeezi Mungu atakaye muongoza basi yeye ndiye mwenye kuongoka na atakayempoteza basi hao ndio wenye khasara.
179. Na bila shaka tumewaumbia Moto wa Jahannam wengi katika majinni na wanadamu. Nyoyo wanazo lakini hawafahamu kwazo, na macho wanayo lakini hawaoni kwayo, na masikio wanayo lakini hawasikii kwayo, hao ni kama wanyama, basi wao ni wapotovu zaidi, hao ndio walioghafilika.
180. Na Mwenyeezi Mungu ana majina mazuri, basi muombeni kwayo, na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.
181. Na katika wale tuliowaumba, wako watu wanaoongoza kwa haki, na wanafanya uadilifu kwa haki hiyo.
182. Na wale waliokadhibisha Aya zetu, tutawavuta kidogo kidogo kwa mahala wasipopajua.
183. Nami nitawapa muda, hakika hila yangu ni madhubuti.
184. Je, hawaafiki? Mwenzao hana wazimu, hakuwa yeye ila ni muonyaji dhahiri.
185. Je, hawaoni ufalme wa mbingu na ardhi na vitu alivyoviumba Mwenyeezi Mungu? na inaweza kuwa ajali yao iko karibu, basi baada ya haya hadithi gani watakayoiamini?
186. Ambaye Mwenyeezi Mungu amempoteza basi hana muongozi, na anawaacha katika uasi wao wakitangatanga.
187. Wanakuuliza juu ya Kiyama kutokea kwake kutakuwa lini? Waambie:
Elimu yake iko kwa Mola wangu tu. Hakuna wa kuidhihirisha kwa wakati wake ila yeye tu. Ni nzito katika mbingu na ardhi, haitakufikieni ila kwa ghafla. Wanakuuliza kama kwamba wewe una pupa nayo, sema: Elimu yake iko kwa Mwenyeezi Mungu tu, lakini watu wengi hawajui.
188. Sema: Sina mamlaka ya kujipa nafuu wala ya kujiondolea madhara ila apendavyo Mwenyeezi Mungu, na lau kama ningelijua ghaibu bila shaka ningejizidishia mema mengi, wala isingenigusa dhara, mimi si chochote ila ni muonyaji na mtoaji wa khabari njema kwa watu wanaoamini.
189. Yeye ndiye aliyekuumbeni katika nafsi moja na katika (nafsi) hiyo ameumba mwenzake ili apate utulivu kwake. Na anapomwingilia hushika mimba nyepesi na kutembea nayo, (hata) anapokuwa mja mzito (wa mimba pevu, mume na mke) wakamuomba Mwenyeezi Mungu, Mola wao: Kama ukitupa (mtoto) mwema, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.
190. Basi anapowapa (mtoto) mwema, wanamuwekea washirika katika kile alichowapa, ametukuka Mwenyeezi Mungu na yale wanayomshirikisha.
191. Je, wanawashirikisha wale ambao hawaumbi kitu hali wao wameumbwa ?
192. Wala hawawezi kuwanusuru, wala hawawezi kujinusuru wenyewe.
193. Na kama mkiwaita kwenye muongozo hawatawafuateni, ni mamoja kwenu ikiwa mtawaita au mtanyamaza kimya.
194. Hakika wale mnaowaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu ni waja kama nyinyi, basi waiteni nao wawaitikieni ikiwa nyinyi mnasema kweli.
195. Je, wanayo miguu ya kuendea? au je, wanayo mikono ya kushikia? au je, wanayo macho ya kuonea? au je, wanayo masikio ya kusikilia? Sema:
Waiteni washirika wenu kisha nifanyieni vitimbi wala msinipe nafasi.
196. Bila shaka Kiongozi wangu ni Mwenyeezi Mungu aliyeteremsha Kitabu, naye ndiye awalindaye wafanyao mema.
197. Na wale mnaowaabudu badala yake hawana uwezo wa kukunusuruni wala wa kujinusuru wenyewe.
198. Na kama mkiwaita katika uongofu hawasikii, na unawaona wanakutazama lakini hawaoni.
199. Shikamana na kusamehe na amrisha mema na wapuuze wajinga.
200. Na kama wasiwasi wa shetani ukikusumbua, basi jikinge kwa Mwenyeezi Mungu kwa sababu yeye ndiye asikiaye, Ajuaye.
201. Hakika wale wanaomcha (Mwenyeezi Mungu) zinapowagusa pepesi za shetani mara hukumbuka tahamaki wamekwisha ona njia.
202. Na ndugu zao wanawavutia kwenye upotovu kisha wao hawaachi.
203. Na usipowaletea Aya husema: Kwa nini hukuichagua? Sema: Hakika nayafuata niliyoletewa Wahyi kutoka kwa Mola wangu. Hizi ni dalili zitokazo kwa Mola wenu na ni muongozo na rehema kwa watu wanaoamini.
204. Na Our’an isomwapo, basi isikilizeni na nyamazeni ili mpate kurehemewa.
205. Na mkumbuke Mola wako moyoni mwako kwa unyenyekevu na khofu na bila ya kupiga kelele katika usemi, asubuhi na jioni, wala usiwe miongoni mwa walio ghafilika.
206. Hakika wale walio karibu na Mola wako hawajivuni wakaacha kumwabudu, na wanamtakasa na wanamsujudia.