Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 69
Kwa jina la Mwenyeezi Mungii, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Alif Lam Mym.
2. Je watu wanadhani wataachwa waseme tumeamini, nao wasijaribiwe?
3. Na bila shaka tuliwajaribu wale waliokuwa kabla yao, na kwa hakika Mwenyeezi Mungu atawatambulisha wale waongo.
4. Je, wanadhania wale wafanya maovu kwamba watatushinda? Ni mabaya wanayohukumu.
5. Mwenye kutumaini kukutana na Mwenyeezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyeezi Mungu itafika bila shaka, naye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
6. Na anayejitahidi, basi bila shaka anajitahidi kwa ajili ya nafsi yake, kwa hakika Mwenyeezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu.
7. Na walioamini na kufanya vitendo vizuri, kwa hakika tutawaondolea maovu yao, na tutawalipa mema ya yale waliyokuwa wakiyafanya.
8. Na tumemuusia mwanadamu (afanye) wema kwa wazazi wake, na kama wakikushurutisha kunishirikisha na yale usiyo na elimu nayo, basi usiwatii kwangu ni marudio yenu, basi nitawaambia mliyokuwa mkiyatenda.
9. Na walioamini na wakafanya vitendo vizuri bila shaka tutawaingiza katika watu wema.
10. Na katika watu yuko anayesema: Tumemwamini Mwenyeezi Mungu, lakini anapoudhiwa katika (njia ya ) Mwenyeezi Mungu huifanya fitna ya watu kama ni adhabu ya Mwenyeezi Mungu, na kama ukifika msaada kutoka kwa Mola wako lazima watasema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi Je, Mwenyeezi Mungu hajui yaliyomo vifuani mwa walimwengu?
11. Na bila shaka Mwenyeezi Mungu atawatambulisha walioamini, na atawatambulisha wanafiki.
12. Na waliokufuru walisema kuwaambia walioamini: Fuateni njia yetu nasi tutayabeba makosa yenu wala wao hawatabeba chochote katika makosa yao, hakika wao ni waongo.
13. Na hakika wataibeba mizigo yao, na mizigo mingine pamoja na mizigo yao, na kwa hakika wataulizwa siku ya Kiyama juu ya yale waliyokuwa wakiyazua.
14. Na bila shaka tulimpeleka Nuhu kwa watu wake na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka hamsini, basi mafuriko yakawaangamiza hali walikuwa madhalimu.
15. Na tukamuokoa yeye na watu wa (ndani ya ) safina, na tukaifanya (iwe mazingatio kwa walimwengu).
16. Na Ibrahimu alipowaambia watu wake, Mwabuduni Mwenyeezi Mungu na mcheni, hayo ni kheri kwenu ikiwa mnajua.
17. Hakika nyinyi mnayaabudu masanamu kinyume cha Mwenyeezi Mungu, na mnatengeneza uongo, bila shaka wale mnaowaabudu kinyume cha Mwenyeezi Mungu wao hawakushikieni riziki, kwa hiyo tafuteni riziki kwa Mwenyeezi Mungu, na Mwabuduni na Mshukuruni, kwake mtarudishwa.
18. Na kama mkikadhibisha, basi wamekwisha kadhibisha watu wa kabla yenu: Na si juu ya Mitume ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi.
19. Je, hawaoni jinsi Mwenyeezi Mungu aanzishavyo kiumbe kisha anakirudisha? Hakika hayo kwa Mwenyeezi Mungu ni rahisi.
20. Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyoanzisha kuumba kisha Mwenyeezi Mungu ndiye atakaeumba umbo la baadaye. Bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
21. Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye, na kwake yeye mtapelekwa.
22. Na nyinyi hamuwezi kumshinda (Mwenyeezi Munguj ardhini wala mbinguni, wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi kinyume cha Mwenyeezi Mungu.
23. Na wale waliozikataa Aya za Mwenyeezi Mungu na mkutano wake, hao ndio wenye kukata tamaa na rehema yangu, na hao ndio watakaopata adhabu yenye kuumiza.
24. Basi halikuwa jawabu la watu wake ila kusema: Muuweni au mchomeni lakini Mwenyeezi Mungu akamuokoa katika moto. Bila shaka katika hayo mna mazingatio kwa watu wenye kuamini.
25. Na alisema: Hakika nyinyi mmeshika masanamu badala ya Mwenyeezi Mungu kwa kupendana baina yenu katika maisha ya dunia, lakini siku ya Kiyama mtakataana wenyewe kwa wenyewe, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi, na makazi yenu yatakuwa Motoni na hamtapata wasaidizi.
26. Basi Luti akamwamini. Na (Ibrahimu) akasema: Hakika mimi nahamia kwa Mola wangu, bila shaka yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
27. Na tulimpa Isihaka na Yaakub, na tukauweka katika kizazi chake Unabii na Kitabu, na tukampa malipo yake katika dunia, naye katika Akhera kwa hakika atakuwa miongoni mwa watu wema.
28. Na Luti alipowaambia watu wake: Bila shaka nyinyi mnafanya uovu (ambao) hakuna aliyekutangulieni kwa (uovu) huo katika walimwengu.
29. Je, mnawaendea wanaume, na mnaikata njia, na mnafanya maovu katika mikusanyiko yenu? Basi halikuwa jawabu la watu wake ila kusema Tuletee adhabu ya Mwenyeezi Mungu ikiwa wewe ni miongoni mwa wasema kweli.
30.Akasema: Mola wangu! Nisaidie juu ya watu mafisadi.
31. Na wajumbe wetu walipomjia Ibrahimu na khabari njema, wakasema:
Bila shaka tutawaangamiza wenyeji wa mji huu, hakika wenyeji wake wamekuwa madhalimu.
32. Akasema: Hakika humo yumo Luti, Wakasema: Sisi tunajua sana aliyomo humo, kwa hakika tutamuokoa yeye na watu wake ila mkewe aliye miongoni mwa watakaokaa nyuma.
33. Na wajumbe wetu walipomfikia Luti, aliwahuzunikia, na moyo wake ulipata dhiki kwa ajili yao, wakasema: Usiogope wala usihuzunike, bila shaka sisi tutakuokoa wewe na watu wako ila mke wako aliye miongoni mwa watakaokaa nyuma.
34. Kwa hakika sisi tutateremsha juu ya wenyeji wa mji huu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu walikuwa wakiasi.
35. Na bila shaka tumeacha katika (mji) huo dalili za wazi kwa watu wanaofahamu.
36. Na kwa Madyan (tulimtuma) ndugu yao, Shua’ybu, naye akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyeezi Mungu na itarajieni siku ya Akhera wala msitembee katika ardhi mkifisadi.
37. Lakini wakamkadhibisha, basi likawashika tetemeko la nchi na wakawa ndani ya nyumba zao wenye kuanguka kifudifudi.
38. Na pia kina Adi na Thamudi (Tuliwaangamiza) Na hakika maskani zao zimekubainikieni, na shetani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia njia na hali walikuwa wenye kuona.
39. Na (vile vile) Qaruni na Firaun na Hamana, na hakika aliwafikia Musa kwa Miujiza (iliyokuwa) wazi wazi, lakini walijivuna katika ardhi, wala hawakuweza kushinda.
40. Basi kila mmoja tulimtesa kwa sababu ya dhambi zake, miongoni mwao yuko tuliyempelekea kimbunga cha changarawe, na miongoni mwao yuko tuliyemdidimiza ardhini, na miongoni mwao yuko tuliyemzamisha. Na hakuwa Mwenyeezi Mungu Mwenye kuwadhulumu lakini walikuwa wakijidhulumu (wenyewe).
41. Mfano wa wale waliofanya waungu asiyekuwa Mwenyeezi Mungu, kama mfano wa buibui ajitandiaye nyumba, na bila shaka nyumba iliyo mbovu kuliko zote ni nyumba ya buibui, laiti wangelijua.
42. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu anajua yale wanayoyaabudu badala yake, naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
43. Na hiyo ndiyo mifano tunayoeleza kwa watu, na hawaifahamu ila wanaye kujua.
44. Mwenyeezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki. Kwa hakika katika hayo mna mazingatio kwa wenye kuamini.
45. Soma uliyofunuliwa katika Kitabu na usimamishe swala. Bila shaka swala huzuia mambo machafu na maovu, na kwa hakika kumbuko la Mwenyeezi Mungu ni (jambo) kubwa kabisa, na Mwenyeezi Mungu anajua mnayoyatenda.
46. Wala msibishane na watu wa Kitabu ila kwa yale yaliyo bora, isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tunaamini yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja nasi ni wenye kunyenyekea kwake.
47. Na hivyo ndivyo tumekiteremsha Kitabu, basi wale tuliowapa Kitabu wanakiamini, na miongoni mwao hawa yuko anayekiamini, na hawazikatai Aya zetu isipokuwa makafiri.
48. Na hukuwa mwenye kusoma Kitabu chochote kabla ya hiki, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kulia ingekuwa hivyo wangelifanya shaka wapotovu.
49. Bali hizi ni Aya wazi wazi (zinazokubaliwa) katika vifua vya wale waliopewa elimu, na hawazikatai Aya zetu Isipokuwa madhalimu.
50. Na wakasema: Mbona hakuteremshiwa Miujiza kutoka kwa Mola wake? Bila shaka katika hayo mna rehema na mawaidha kwa watu wanaoamini.
51. Je, hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu wanachosomewa? Bila shaka katika hayo mna rehema na mawaidha kwa watu wanaoamini.
52. Sema: Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa shahidi kati yangu na kati yenu: anajua yaliyomo katika mbingu na ardhini, na wale wanaokubali batili na kumkataa Mwenyeezi Mungu, hao ndio wenye kupata hasara.
53. Na wanakuhimiza (waletewe) adhabu, na kama pasingeliwekwa wakati maalumu adhabu ingeliwafikia, na lazima itawafikia kwa ghafla nao hawatambui.
54. Wanakuhimiza adhabu ifike upesi. Na kwa hakika Jahannam imewazunguka makafiri.
55. Siku itakapowafunika adhabu kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na atasema: Onjeni mliyokuwa mkitenda.
56. Enyi waja wangu mlioamini, kwa hakika ardhi yangu ina wasaa, basi niabuduni Mimi tu.
57. Kila nafsi itaonja mauti, kisha mtarudishwa kwetu.
58. Na ambao wameamini na kufanya vitendo vizuri, bila shaka tutawakalisha katika maghorofa ya Peponi mpitamo mito chini yake, wakae humo milele. Ni neema ilioje kwa malipo ya wenye kutenda!
59. Ambao walisubiri na kwa Mola wao wanategemea.
60. Na wanyama wangapi hawabebi riziki zao? Mwenyeezi Mungu huwaruzuku wao na nyinyi pia, naye ndiye Mwenye kusikia, Mjuzi.
61. Na kama ukiwauliza ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akavitiisha jua na mwezi? Bila shaka watasema Mwenyeezi Mungu. Wapi basi wanakogeuzwa?
62. Mwenyeezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humdhikishia. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
63. Na ukiwauliza: Ni nani ateremshae maji mawinguni na kuihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila shaka watasema: Mwenyeezi Mungu, sema kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mungu, lakini wengi wao hawafahamu.
64. Na hayakuwa maisha haya ya dunia ila upuuzi na mchezo, na nyumba ya Akhera ndiyo maisha khasa, laiti wangelijua.
65. Na wanapopanda katika jahazi, wanamuomba Mwenyeezi Mungu, wakimtakasishia utii, lakini anapowafikisha salama barani, mara wanamshirikisha.
66. Wapate kuyakanya tuliyowapa na wapate kustarehe, lakini karibuni watajua.
67. Je, hawaoni kuwa, tumeifanya nchi takatifu kuwa na amani hali hunyang’anywa watu wa pembezoni mwake, je, wataamini batili na kuzikataa neema za Mwenyeezi Mungu?
68. Na nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzushia uongo Mwenyeezi Mungu, au anayekadhibisha haki inapomjia? Je, si katika Jahannam yatakuwa makazi ya makafiri?
69. Na wale wanaojitahidi kwa ajili yetu, lazima tutawaongoza kwenye njia zetu. Na bila shaka Mwenyeezi Mungu yu pamoja na wafanyao mema.