Sura hii imeteremshwa Makka, na ina Aya 19
Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba.
2. Amemuumba Mwanadamu katika pande la damu.
3. Soma, na Mola wako ni Mtukufu mno.
4. Ambaye amefunza (kuandika) kwa kalamu.
5. Amemfunza mwanadamu asilolijua.
6. Sivyo, hakika mwanadamu anaasi sana.
7. Kwa kujiona ametosha.
8. Bila shaka marejeo ni kwa Mola wako.
9. Je, umemuona ambaye humkataza.
10. Mja (wa Mungu) anaposwali?
11. Je, unaonaje kama yuko katika muongozo.
12. Au anaamuru ucha Mungu?
13. Je, unaonaje kama anakadhibisha na kurudi nyuma?
14. Je, hujui kuwa Mwenyeezi Mungu anaona?
15. Sivyo, kama haachi, tutamkokota kwa nywele za utosini.
16. Utosi muongo, wenye makosa.
17. Basi na amwite mshauri wake.
18. Nasi tutawaita askari wa adhabu.
19. Akome, usimtii bali sujudu na uwe karibu (na Mwenyeezi Mungu).