Surah Ahzab

Sura hii imeteremshwa Madina, na ina Aya 73

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Ewe Nabii! Mche Mwenyeezi Mungu wala usiwatii makafiri na wanafiki bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

2. Na ufuate uliyoletewa Wahyi kutoka kwa Mola wako, kwa hakika Mwenyeezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.

3. Na utegemee kwa Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu atosha kuwa mlinzi.

4. Mwenyeezi Mungu hakumuwekea mwanadamu nyoyo mbili kifuani mwake, wala hakuwafanya wake zenu mliolinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu kuwa mama zenu, wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa watoto wenu khasa, hayo ni maneno yenu ya vinywa vyenu, na Mwenyeezi Mungu husema kweli, naye huongoza njia.

5. Waiteni kwa (ubini wa) ababa zao, maana huo ndio uadilifu mbele ya Mwenyeezi Mungu. Na kama hamuwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika dini na rafiki zenu. Wala si lawama juu venu katika hayo mliyokosa, isipokuwa katika yale ziliyofanya nyoyo zenu kwa kusudi, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

6. Nabii ana haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao, na wakeze ni mama zao, na wenye nasaba wana haki zaidi wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyeezi Mungu kuliko waumini na waliohama. Lakini kama mkifanya wema kwa marafiki zenu (si vibaya) hayo yamekwisha andikwa Kitabuni.

7.  Na tulipoahidiana na Manabii na wewe na Nuhu na Ibrahimu, na Musa na Isa mwana wa Mariam, na tuliahidiana nao ahadi ngumu.

8. Ili awaulize wakweli juu ya ukweli wao, na amewaandalia makafiri adhabu yenye kuumiza.

9. Enyi mlioamini! kumbukeni neema za Mwenyeezi Mungu zilizo juu yenu valipokufikieni majeshi, tuliwapelekea upepo na majeshi msiyo yaona, na Mwenyeezi Mungu anayaona mnayoyafanya.

10. Walipowajia (kukushambulieni) kutokajuu yenu na kutoka chini yenu, na macho yaliponywea na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkaanza kumdhania Mwenyeezi Mungu dhana mbali mbali.

11. Hapo Waumini walijaribiwa na wakateremshwa kwa tetemesho kali.

12. Na waliposema wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, Mwenyeezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu.

13. Na taifa moja miongoni mwao lilisema: enyi wenyeji wa Yathribu! hapa si mahala pa kukaa nyinyi, basi rudini, na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu, lakini hazikuwa tupu, hawakutaka ila kukimbia tu.

14. Na lau kama yangeliingizwa (majeshi) juu yao katika pande zote (za Madina) kisha wakaombwa kufanya vita, wangeifanya, na wasingelikaa humo ila muda kidogo tu.

15. Na kwa hakika walikwishafanya ahadi na Mwenyeezi Mungu zamani, kuwa hawatageuza migongo, na ahadi ya Mwenyeezi Mungu ni yenye kuulizwa.

16. Sema: Kukimbia hakutakufaeni ikiwa mnakimbia mauti au kuuwawa na hata hivyo hamtastareheshwa ila kidogo tu.

17. Sema: Ni nani ambaye aweza kukulindeni na Mwenyeezi Mungu kama Mwenyeezi Mungu) akikutakieni uovu, na akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi kinyume cha Mwenyeezi Mungu.

18. Bila shaka Mwenyeezi Mungu anawajua wale wanaojizuia miongoni mwenu na wawaambiao ndugu zao. Njooni kwetu wala hawaingii vitani ila kidogo tu.

19. Wanachoyo juu yenu, lakini inapofika khofu, utawaona wanakutazama, macho yao yanazungukazunguka kama yule aliyezimia kwa mauti, lakini khofu inapoondoka, wanakuudhini kwa ndimi kali, wakifanya choyo juu ya kheri. Hao hawakuamini, kwa hiyo Mwenyeezi Mungu ameviharibu vitendo vyao, na hayo ni mepesi kwa Mwenyeezi Mungu.

20. Wanafikiri makundi haya hayajaondoka, na kama makundi yangekuja (tena) wangependa laiti wangekaa jangwani pamoja na Mabedui wakiuliza khabari zenu, na kama wangelikuwa pamoja nanyi wasingelipigana ila kidogo tu.

21. Bila shaka mnao mfano mwema kwa Mtume wa Mwenyeezi Mungu, kwa mwenye kumuogopa Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho, na kumtaja Mwenyeezi Mungu sana.

22.Na Waumini walipoyaona majeshi, walisema: Haya ndiyo aliyotuahidi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli, na haikuwazidishia ila imani na utii.

23. Wapo watu miongoni mwa Waumini waliotimiza ahadi waliyoahidiana na Mwenyeezi Mungu, baadhi yao wamekwishamaliza nadhiri zao, na wako miongoni mwao wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi yao) hata kidogo.

24. Ili Mwenyeezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli wao, na kuwaadhibu wanafiki akipenda, au kuwageukia (kwa rehema) Bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

25. Na wale waliokufuru Mwenyeezi Mungu amewarudisha na ghadhabu yao, hawakupata chochote katika kheri, na Mwenyeezi Mungu amewatoshea Waumini katika mapigano, Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo Mwenye nguvu.

26. Na akawateremsha wale waliowasaidia (maadui) katika watu wa kitabu kutoka katika ngome zao, na akatia khofu katika nyoyo zao, baadhi yao mnawaua na wengine mnawateka.

27. Na akawarithisheni nchi yao na majumba yao na mali zao, na nchi msiyoikanyaga, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.

28. Ewe Nabii! waambie wake zako; Ikiwa mnapenda maisha ya dunia hii na uzuri wake basi njooni, nitakupeni matumizi na kukuacheni muacho mzuri.

29. Na kama mnamtaka Mwenyeezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera, basi Mwenyeezi Mungu amewaandalia wafanyao mema miongoni mwenu malipo makubwa.

30. Enyi wakc wa Nabii! atakayefanva maovu dhahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili, na hayo ni rahisi kwa Mwenyeezi Mungu.

31. Na miongoni mwenu atakayemtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake na kutenda mema tutampa malipo yake mara mbili, na kumwandalia riziki yenye heshima.

32. Enyi wake wa Nabii! nyinyi si kama yeyote katika wanawake kama mkimcha (Mwenyeezi Mungu) basi msiwe laini katika usemi ili asitamani mtu mwenye ugonjwa moyoni mwake, na semeni maneno mazuri.

33. Na kaeni majumbani mwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani, na simamisheni swala, na toeni zaka, na mtiini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyeezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba (ya Mtume), na (anataka) kukutakaseni sana sana.[1]

34. Na kumbukeni yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za Mwenyeezi Mungu na (maneno ya) hekima, kwa hakika Mwenyeezi Mungu ni Mpole, Mwenye khabari.

35. Bila shaka wanaume wenye kufuata vizuri nguzo za Uislaamu, na wanawake wanaozifuata vizuri nguzo za Uislaamu na wanaume wanaoamini vizuri nguzo za Imani, na wanawake wanaoamini vizuri nguzo za Imani, na wanaume wanaotii na wanawake wanaotii, na wanaume wasemao kweli, na wanawake wasemao kweli, na wanaume wanaosubiri, na wanawake wanaosubiri, na wanaume wanao nyenyekea, na wanawake wanao nyenyekea, na wanaume wanaotoa sadaka, na wanawake wanaotoa sanaka, na wanaume wanaofunga saumu, na wanawake wanaofunga saumu, na wanaume wanaolinda tupu zao, na wanawake wanaolinda (tupu zao) na wanaume wanaomtaja Mwenyeezi Mungu kwa wingi na wanawake wanaomtaja Mwenyeezi Mungu (kwawingi) Mwenyeezi Mungu amewaandalia msamaha na malipo makubwa.

36. Haiwi kwa mwanaume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyeezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na khiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotovu ulio wazi.

37. Na ulipomwambia yule ambaye Mwenyeezi Mungu amemneemesha na wewe (pia) umemneemesha: Shikamana na mkeo na umche Mwenyeezi Mungu, na ukaficha katika nafsi yako aliyotaka Mwenyeezi Mungu kuyatoa, na ukawachelea watu, hali Mwenyeezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi ya kumchelea. Basi Zaid alipokwisha haja naye tulikuoza wewe ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga wanapomaliza haja nao, na amri ya Mwenyeezi Mungu ni yenye kutekelezwa.

38. Si kosa kwa Nabii katika yale ambayo Mwenyeezi Mungu amemlazimisha, ndiyo kawaida ya Mwenyeezi Mungu kwa wale waliopita zamani, na amri ya Mwenyeezi Mungu ni kipimo kilichokadiriwa.

39. Wale wanaofikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu na kumuogopa yeye wala hawamuogopi yeyote isipokuwa Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu ndiye atoshaye kuhesabu.

40. Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu bali, ni Mtume wa Mungu na Mwisho wa Mitume na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.[2]

41. Enyi mlioamini! mkumbukeni Mwenyeezi Mungu kwa wingi.

42. Na mtukuzeni asubuhi najioni.

43. Yeye ndiye anayekurehemuni, na Malaika wake, ili kukutoeni katika giza kukupelekeni kwenye nuru, naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini.

44. Maamkiano yao siku ya kukutana naye yatakuwa: Amani, Na amewaandalia malipo yenye heshima.

 45. Ewe Nabii kwa hakika sisi tumekutuma (ili uwe) shahidi na mtoaji wa khabari nzuri na muonyaji.

46. Na muitaji (wa watu) kwa Mwenyeezi Mungu kwa idhini yake, na (uwe) taa itoayo nuru.

47. Na wape khabari njema Waumini kuwa, wanafadhili kubwa itokayo kwa Mwenyeezi Mungu.

48. Na usiwatii makafiri na wanafiki, wala usijali udhia wao, na tegemea kwa Mwenyeezi Mungu na Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi.

49. Enyi mlioamini! Mtakapowaoa wanawake wenye kuamini kisha mkawapa talaka kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayohesabu, na wapeni cha kuliwaza na muwaache muacho mzuri.

 50. Ewe Nabii! tumekuhalalishia wake zako ambao uliwapa mahari yao, na (wanawake) uliowamiliki mkono wako katika wale aliokupa Mwenyeezi Mungu, na mabinti wa ami yako na mabinti wa mjomba wako, na mabinti wa dada ya mama yako, waliohama pamoja nawe, na mwanamke muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii, na kama Nabii akitaka kumuoa, ni halali kwako tu, si kwa waumini wengine. Bila shaka tumekwisha jua tuliyowafaridhia katika wake zao, na iliyowamiliki mikono yao ili isiwe dhiki kwako, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

51. Umwakhirishe umtakaye miongoni mwao na kumkaribisha umtakaye na kama ukimtaka yule uliyemtenga, basi si vibaya kwako, hivyo itakuwa karibu zaidi yaburudike macho yao wala wasihuzunike, na wawe radhi juu ya kile unachowapa wao wote. Na Mwenyeezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi, Mpole.

52. Baada ya hawa si halali kwako (kuoa) wanawake (wengine) wala si (halali) kuwabadilisha kwa wake wengine ingawa uzuri wao ukikupendeza, isipokuwa yule uliommiliki mkono wako na Mwenveezi Mungu ni Mchungaji wa kila kitu.

53. Enyi mlioamini! msiingie nyumba za Nabii ila kama mkipewa ruhusa kwenda kula, pasipo (kwenda kukaa) kungojea kiive. Lakini mnapoitwa basi ingieni, na mnapokwisha kula, tawanyikeni, wala msishughulike kuzungumza, maana Jambo hili humuudhi Mtume, naye anakuoneeni haya, lakini Mwenyeezi Mungu haoni haya kusema haki. Nanyi mnapowauliza (wakeze) waulizeni nyuma ya pazia, hayo ni safi kabisa kwa nyoyo zenu na kwa nyoyo zao, wala haiwapasi (nyinyi) kumuudhi Mtume wa Mwenyeezi Mungu wala msiwaoe wake zake baada yake kabisa, hakika hilo ni (kosa) kubwa mbele ya Mwenyeezi Mungu.[3]

54. Mkidhihirisha chochote au kukificha, basi hakika Mwenyeezi Mungu anajua kila kitu.

55. Si dhambi juu yao (wake za Mtume) katika (kuonana na) Baba zao, wala watoto wao, wala Kaka zao, wala watoto wa Dada zao, wala wanawake wao, wala wale iliyo wamiliki mikono yao. Na muogopeni Mwenyeezi Mungu, bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Shahidi juu ya kila kitu.

56. Hakika Mwenyeezi Mungu na Malaika wake humsalia Mtume, enyi mlioamini! msalieni (Mtume) na muombeeni amani.

Aya 56

 SWALAWAAT ITAKIKANAYO

Iliposhuka Aya hii, maswahaba walimuuliza Mtume: Tutakuswalia vipi? Mtume akawaambia, semeni: “Allahumma Swalli alaa Muhammad wa alaa Aali Muhammad”…

Taz: Tafsirul Basaair: J.32 Uk. 653-672 

         Majmaul Bayani: J. 4 Uk. 369

        Almizan fyitafsiril Qur’an:  j.16 uk366

       Alburhan fyitafsiril Qur’an:  j.3 uk.335

       Tafsirus Saafi:  j.4 uk.201

        Al-TafsirulKaashif:  j.6 uk.237 

Mtume s.a.w anasema: Msiniswalie swala iliyo katika, maswahaba wakauliza: Ni swala gani iliyokatika? Mtume s.a.w akajibu: Mnasema, Allahumma swalli a’laa Muhammad, mnanyamaza, lakini semeni: Allaahumma swalli a’laa Muhammad wa A’laa Aali Muhammad.”

Taz: Yanaabiul Mawadda:  J.l  Uk. 6

As’swawaaiqul muhriqa: Uk. 146

Angalia: kusema, “Swallallahu a’layhi wasallama” ni batili, unatakiwa kusema: “Swallallahu alayhi wa Aalihi.”

57. Kwa hakika wale wanaomuudhi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, Mwenyeezi Mungu amewalaani katika dunia na Akhera, na amewaandalia adhabu yenye kufedhehesha.

58. Na wale wanaowaudhi wanaume waummini na wanawake waumini pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilizo dhahiri.

59. Ewe Nabii! waambie wake zako, na mabinti zako, na wake wa waumini: Wateremshe juu yao shungi zao. Hivyo inaelekea zaidi wajulikane na wasiudhiwe, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.

60. Kama wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao na watangazao uovu mjini hawataacha (visa vyao) kwa hakika tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda kidogo.

61. Wamelaaniwa popote waonekanapo wakamatwe na wauawe kabisa.

62. Ni kawaida ya Mwenyeezi Mungu iliyokuwa kwa wale waliopita zamani, wala hutapata mabadiliko katika kawaida ya Mwenyeezi Mungu.

63. Watu wanakuuliza khabari za Kiyama, sema: Elimu yake iko kwa Mwenyeezi Mungu tu. Na nini kitakujulisha. pengine Kiyama kiko karibu.

64. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu amewalaani makafiri na amewaandalia Moto uwakao.

65. Watakaa humo Milele, hawatapata mlinzi wala msaidizi.

66. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa Motoni, waseme: Laiti tungemtii Mwenyeezi Mungu na tungemtii Mtume.

67. Na watasema: Mola wetu! hakika tumewafuata mabwana wetu na wakubwa wetu, basi wao wametupoteza njia.

68. Mola wetu! wape hawa adhabu mara dufu na uwalaani laana kubwa.

69. Enyi mlioamini! msiwe kamawale waliomtaabisha Musa, lakini Mwenyeezi Mungu alimtakasa na yale waliyoyasema, naye alikuwa mwenye heshima mbele ya Mwenyeezi Mungu.

70. Enyi mlioamini! muogopeni Mwenyeezi Mungu na semeni maneno ya sawa.

71. Atakutengenezeeni vizuri vitendo vyenu na atakusameheni madhambi yenu, na anayemtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake bila shaka amefaulu kufaulu kukubwa.

72. Kwa hakika sisi tulizitolea amana mbingu na ardhi na milima lakini vikakataa kuichukua na vikaiogopa, lakini mwanadamu akaichukua. Bila shaka yeye ni dhalimu mkubwa mjinga sana.

73. Ili Mwenyeezi Mungu awaadhibu wanaume wanafiki na wanawake wanafiki, na wanaume washirikina na wanawake washirikina, na Mwenyeezi Mungu awasamehe Waumini wanaume na Waumini wanawake, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.