Sura hii imeteremshwa Madina, Aya 200
Kwajina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
1. Alif, Lam Mym.
2. Mwenyeezi Mungu, hakuna aabudiwaye isipokuwa yeye tu, Mzima wa milele, Mwenye kusimamia mambo ya viumbe.
3. Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na ameteremsha Taurati na Injili.
4. Kabla yake, ziwe uongofu kwa watu, na ameteremsha upambanuzi (kati ya haki na batili) Hakika wale waliozikataa Aya za Mwenyeezi Mungu, wana adhabu kali. Na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kutia adabu.
5. Hakika Mwenyeezi Mungu hakifichiki kwake chochote kilichomo ardhini wala kilichoko mbinguni.
6. Yeye ndiye ambaye huwatia sura katika matumbo namna atakayo, hakuna aabudiwaye isipokuwa yeye tu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
7. Yeye ndiye aliyekuteremshia Kitabu, ndani yake zimo Aya zilizo wazi wazi nazo ndizo msingi wa Kitabu (hiki) na nyingine ni zenye kufichikana. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu, hufuata yaliyofichikana katika hayo kwa ajili ya kutaka upotovu na kutaka kutafsiri (watakavyo). Na hakuna ajuaye tafsiri yake ila Mwenyeezi Mungu na wale waliozama katika elimu tu. Husema: tumeyaamini, yote yanatoka kwa Mola wetu. Na hawakumbuki isipokuwa wenye akili.
8. Mola wetu! usizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza na utupe rehema itokayo kwako, hakika wewe ndiye Mpaji mkuu.
9. Mola wetu! hakika Wewe ndiye Mwenye kuwakusanya watu katika siku isiyokuwa na shaka. Hakika Mwenyeezi havunji miadi.
10. Hakika wale waliokufuru hayatawafaa kitu mali yao wala watoto wao kwa Mwenyeezi Mungu na hao ndio kuni za Moto.
11. Ni kama desturi ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao. Walizikadhibisha Aya zetu, Mwenyeezi Mungu akawashika kwa sababu ya madhambi yao, na Mwenyeezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
12. Waambie wale waliokufuru: Mtashindwa, na mtakusanywa kwenye Jahannam, nacho ni kikao kibaya.
13. Hakika ilikuwa ni mazingatio kwenu katika makundi mawili yaliyokutana, kundi moja lilipigana katika njia ya Mwenyeezi Mungu, na jingine kafiri, likiwaona zaidi kuliko wao mara mbili kwa kuona kwa macho. Na Mwenyeezi Mungu humpa nguvu amtakaye kwa nusra yake, hakika katika hayo mna mazingatio kwa wenye busara.
14. Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na vijana wakiume, na mali mengi ya dhahabu na fedha, na farasi wazuri wazuri, na wanyama na mimea. Hivyo ni vitu vya kustarehea katika uhai wa ulimwenguni, na kwa Mwenyeezi Mungu ndiko kwenye marejeo mazuri.
15. Sema: Je, niwaambieni yaliyo bora kuliko hivyo? Kwa wacha Mungu ziko Bustani kwa Mola wao. zipitazo mito chini yake, watakaa humo milele, na wake waliotakaswa, na radhi ya Mwenyeezi Mungu na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa waja.
16. Ambao husema: Mola wetu! hakika sisi tumeamini, basi tusamehe madhambi yetu, na utuepushe na adhabu ya Moto.
17. Wafanyao subira na wasemao kweli, na watii, na watoao (sadaka) na waombao msamaha (nyakati za) karibu ya alfajiri.
18. Mwenyeezi Mungu, na Malaika, na Wenye elimu, wameshuhudia kuwa hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, ni Mwenye kusimamia uadilifu. Hakuna aabudiwaye isipokuwa yeye tu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
19. Hakika dini mbele ya Mwenyeezi Mungu ni Uislaamu. Na waliopewa Kitabu hawakukhitilafiana ila baada ya kuwajia elimu, kwa sababu ya hasadi baina yao. Na anayezikataa Aya za Mwenyeezi Mungu, basi hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.
20. Kama wakikuhoji, basi sema: Mimi nimemnyenyekea Mwenyeezi Mungu kwa nafsi yangu (pamoja) na walionifuata, na waambie wale waliopewa Kitabu na wasio na elimu: Je, Mmenyenyekea? watakaponyenyekea, basi wameongoka, na wakikataa, basi lililokupasa wewe ni kufikisha tu, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa waja.
21. Hakika wale wanaozikataa Aya za Mwenyeezi Mungu, na kuwaua Manabii pasipo haki, na kuwaua watu wanaoamuru mambo ya uadilifu, basi wape khabari ya adhabu iumizayo.
22. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na Akhera, wala hawana wenye kuwanusuru.
23. Je, huwaoni wale waliopewa fungu katika Kitabu, wanaitwa kwenye Kitabu cha Mwenyeezi Mungu ili awahukumu baina yao kisha kundi moja miongoni mwao hukataa nao wamekwenda upande.
24. Hayo ni kwa sababu walisema: Hautatugusha Moto isipokuwa kwa siku chache, na yakawadanganya katika dini yao yale waliyokuwa wakiyazua.
25. Basi itakuwaje tutakapowakusanya siku ambayo haina shaka ndani yake, na kila nafsi itapewa ilichokichuma, nao hawatadhulumiwa.
26. Sema: Ee Mola! Mwenye kumiliki Ufalme humpa ufalme umtakaye, na humnyang’anya ufalme umtakaye, na humtukuza umtakaye na kumdhalilisha umtakaye. Kheri imo mikononi mwako, hakika wewe ni Muweza wa kila kitu.
27. Huutia usiku katika mchana na ukautia mchana katika usiku na ukakitoa kilicho hai katika kilicho maiti, na ukakitoa kilicho maiti katika kilicho hai, na ukamruzuku umtakaye pasi na hesabu.
28. Wenye kuamini wasiwafanye makafiri kuwa viongozi badala ya wenye kuamini, na atakayefanya hivyo, basi hana chochote kwa Mwenyeezi Mungu, ila mtakapojilinda nao kwa kujihifadhi. Na Mwenyeezi Mungu anawatahadharisha na Nafsi yake, na kwa Mwenyeezi Mungu ndio marejeo.
29. Sema: Kama mkificha yaliyomo vifuani mwenu au kuyadhihirisha, Mwenyeezi Mungu anayajua. Na anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini, na Mwenyeezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
30. Siku ambayo kila nafsi itakuta kheri iliyotenda imehudhurishwa, na shari iliyotenda (pia) itapenda lau kungekuwa na nafasi ndefu kati yake na kati ya hiyo (shari). Na Mwenyeezi Mungu anakutahadharisheni naye, na Mwenyeezi Mungu ni Mpole kwa waja.
31. Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyeezi Mungu, basi nifuateni Mwenyeezi Mungu atawapenda na atawasamehe madhambi yenu, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.
32. Sema: Mtiini Mwenyeezi Mungu na Mtume, na kama wakikataa, basi kwa hakika Mwenyeezi Mungu hawapendi makafiri.
33. Hakika Mwenyeezi Mungu amemchagua Adam na Nuhu na watoto wa Ibrahim na watoto wa Imran juu ya walimwengu.
34. Kizazi wao kwa wao, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
35. Wakati aliposema mke wa Imran: Mola wangu! hakika nimeweka nadhiri kwako aliyomo tumboni mwangu kuwa wakfu basi nikubalie, bila shaka wewe ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
36. Basi alipomzaa, akasema: Mola wangu! hakika nimemzaa mwanamke, na Mwenyeezi Mungu anajua sana aliyemzaa, na mwanamume si kama mwanamke. Na mimi nimemwita Mariam, nami namlinda kwa nguvu zake, (yeye) na kizazi chake, (uwalinde) na shetani mwenye kufukuzwa.
37. Basi Mola wake akamkubali kwa mapokezi mazuri, na akamlea kwa ulezi mwema, na akampa Zakaria kumlea. Na Zakaria kila aingiapo kwake (Mariam) chumbani, hukuta vyakula pamoja naye akasema: Ewe Mariam umevipata wapi hivi? akasema: Vyatoka kwa Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hesabu.
38. Pale Pale Zakaria akamuomba Mola wake, akasema: Mola wangu! umpe kutoka kwako kizazi kizuri, hakika wewe ndiye Mwenye kusikia maombi.
39. Mara Malaika wakamwita naye amesimama akiswali chumbani kwamba: Mwenyeezi Mungu anakupa khabari njema za Yahya, atakaye kuwa mwenye kusadikisha neno litokalo kwa Mwenyeezi Mungu, na Bwana na Mtawa, na Nabii miongoni mwa watu wema.
40. Akasema: Mola wangu! nitapataje mtoto na utu uzima umekwisha nifikilia, na mke wangu ni tasa? Akasema: Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu hufanya atakavyo.
41.Akasema: Mola wangu! nifanyie alama: (Mwenyeezi Mungu) Akamwambia: Alama yako ni kutosema na watu siku tatu ila kwa ishara. Na mtaje Mola wako kwa wingi, na uswali jioni na asubuhi.
42. Na (kumbukeni) Malaika waliposema; Ewe Mariam! hakika Mwenyeezi Mungu amekuchagua na amekutakasa, na amekuchagua kuliko wanawake wa ulimwenguni.
43. Ewe Mariam! Mtii Mola wako na usujudu na urukuu pamoja na wenye kurukuu.
44. Hizo ni khabari za ghaibu tunazokufunulia. Hukuwa nao walipokuwa wakitupa kalamu zao (ili kujua) ni nani (katika) wao atakaye mlea Mariam, na hukuwa nao walipokuwa wakishindana.
45. (Kumbukeni) Malaika waliposema: Ewe Mariam! Hakika Mwenyeezi Mungu anakupa khabari njema za neno litokalo kwake, jina lake ni Masihi Isa Mwana wa Mariam, mwenye heshima ulimwenguni na Akhera, na ni miongoni mwa wenye kukurubishwa (mbele ya Mwenyeezi Mungu).
46. Atasema na watu katika uchanga na utu uzima, na atakuwa katika watu wema.
47. Akasema (Mariam): Mola wangu! nitampataje mtoto na hali mtu yeyote hakunigusa? Akasema: Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu huumba anavyotaka, anapohukumu jambo basi huliambia kuwa basi huwa.
48. Na (Mwenyeezi Mungu) atamfundisha kuandika na (kujua) elimu na (kujua) Taurati na Injili.
49. Na (atamfanya) Mtume kwa wana wa Israel, (awaambie) Hakika mimi nimewajieni na dalili itokayo kwa Mola wenu. Mimi nitakufanyieni katika udongo kama namna ya ndege, kisha napulizia ndani yake (awe) ni ndege kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu. Na niwapoze vipofu na wenye mbalanga, niwafufue wafu kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu. Na niwape khabari na mnavyokula na mnavyoviweka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika hayo mna dalili kwenu ikiwa nyinyi ni wenye kuamini.
50. Na ninasadikisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati na ili niwahalalishieni baadhi ya yale mliyoharamishiwa. Na nimewajieni na dalili kutoka kwa Mola wenu, basi Mcheni Mwenyeezi Mungu na nitiini.
51. Hakika Mwenyeezi Mungu ndiye Mola wangu na ni Mola wenu, basi muabuduni, hii ndiyo njia iliyonyooka.
52. Isa alipotambua ukafiri wao, alisema: Nani atakuwa msaidizi wangu kwa (njia ya) Mwenyeezi Mungu? wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa (njia) ya Mwenyeezi Mungu. Tumemwamini Mwenyeezi Mungu, nawe shuhudia kwamba sisi ni wenye kunyenyekea kwake.
53. Mola wetu! tumeyaamini uliyoyateremsha, na tumemfuata Mtume, basi tuandike pamoja na wenye kushuhudia.
54. Wakafanya vitimbi: Na Mwenyeezi Mungu akafanya vitimbi. Na Mwenyeezi Mungu ni Mbora wa wenye kufanya vitimbi.
55. (Kumbukeni) Aliposema Mwenyeezi Mungu: Ewe Isa! Mimi nitakufisha na nikuinue kwangu. Na nikuepushe na wale waliokufuru, na niwafanye wale waliokufuata (wawe) juu ya wale waliokufuru mpaka siku ya Kiyama kisha marejeo yenu ni kwangu, nitahukumu baina yenu katika yale mliyokuwa mkikhitilafiana.
56. Ama wale waliokufuru, basi nitawaadhibu adhabu kali duniani na Akhera, wala hawana wenye kuwanusuru.
57. Na wale walioamini na kufanya vitendo vizuri basi atawalipa thawabu zao, na Mwenyeezi Mungu hawapendi wenye kudhulumu.
58. Hicho (Kitabu) tunakusomea ni katika dalili na Qur’an yenye hekima.
59. Hakika mfano wa Isa mbele ya Mwenyeezi Mungu ni kama mfano wa Adam, alimuumba kwa udongo, kisha akamwambia kuwa, basi akawa.
60. Ndiyo haki itokayo kwa Mola wako, basi usiwe miongoni mwa wenye kutia shaka.
61. Na atakayebishana nawe katika hili baada ya ujuzi uliokujia, basi waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu na tuiweke laana ya Mwenyeezi Mungu iwashukie wenye kusema uongo.
62. Hakika hii ndiyo khabari ya kweli, wala hakuna aabudiwaye ila Mwenyeezi Mungu tu, na hakika Mwenyeezi Mungu ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
63. Na kama wakikataa, basi hakika Mwenyeezi Mungu anawajua waharibifu.
64. Sema: Enyi watu wa Kitabu! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu, tusimwabudu ila Mwenyeezi Mungu tu, wala tusimshirikishe na chochote, wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa ni waungu badala ya Mwenyeezi Mungu. Basi wakikataa, waambieni: Shuhudieni kwamba sisi ni wenye kunyenyekea (kwa Mwenyeezi Mungu).
65. Enyi watu wa Kitabu! mbona mnabishana juu ya Ibrahim na hali havikuteremshwa Taurati na Injili ila baada yake, basi hamfahamu?
66. Nyinyi ndio waliobishana katika yale mliyoyajua, tena kwanini mnabishana katika yale msiyoyajua? Na Mwenyeezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
67. Ibrahim hakuwa Myahudi wala Mkristo, lakini alikuwa ni mwenye kushikamana na dini ya sawasawa, mwenye kunyenyekea, wala hakuwa katika washirikina.
68. Hakika watu wanaomkurubia zaidi Ibrahim ni wale waliomfuata, Nabii huyu, na wale walioamini. Na Mwenyeezi Mungu ndiye Mlinzi wa Waumini.
69. Kundi moja miongoni mwa watu wa Kitabu wanapenda kukupotezeni, wala hawapotezi ila nafsi zao na wala wao hawatambui.
70. Enyi watu wa Kitabu, kwanini mnazikataa Aya za Mwenyeezi Mungu hali mnashuhudia?
71. Enyi watu wa Kitabu! kwa nini mnachanganya haki na batili, na mnaificha haki na hali mnajua?
72. Na kundi moja katika watu wa Kitabu lilisema: Aminini yaliyoteremshwa juu ya wale walioamini mwanzo wa mchana, na mkatae mwisho wake, huenda watarejea.
73. Wala msimwamini ila yule anayefuata dini yenu. Sema Hakika uongofu ni uongofu wa Mwenyeezi Mungu. Kuwa apewe mtu mfano wa yale mliyopewa, au wakuhojini mbele ya Mola wetu! Sema: Hakika fadhili ziko mkononi mwa Mwenyeezi Mungu humpa amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye ujuzi.
74. Humchagua kwa rehema zake amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ndiye Mwenye fadhili kubwa.
75. Na katika watu wa Kitabu yuko ambaye ukimpa amana ya mali mengi hukurejeshea, na katika wao yuko ambaye ukiweka kwake amana ya dinari moja hakurejeshei isipokuwa uendelee kumsimamia. Hayo ni kwamba wao husema: Hatuna madhambi kwa (kula mali ya) wajinga na wanasema uongo juu ya Mwenyeezi Mungu hali wanajua.
76. Kwanini? (wanayo madhambi). Anayetekeleza ahadi yake na kujilinda na madhambi, basi hakika Mwenyeezi Mungu anawapenda wanaojilinda.
77. Hakika wale wanaouza ahadi ya Mwenyeezi Mungu na viapo vyao kwa thamani ndogo, hao hawana fungu Akhera, wala hatasema nao Mwenyeezi Mungu, wala hatawatazama siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao watapata adhabu iumizayo.
78. Na hakika katika wao kuna kundi linalozipotoa ndimi zao kwa (kusoma) Kitabu ili mpate kuyadhania (maneno yao) kwamba ni ya Kitabu, na kumbe si ya Kitabu. Na wanasema: Hayayanatoka kwa Mwenyeezi Mungu na hali hayakutoka kwa Mwenyeezi Mungu, na wanaserna uongo juu ya Mwenyeezi Mungu hali wanajua.
79. Haiwezekani kwa mtu yeyote kupewa na Mwenyeezi Mungu Kitabu na Hekima na Utume, kisha awaambie watu: Kuweni wenye kuniabudu mimi badala ya Mwenyeezi Mungu, lakini (huwaambia) kuweni Wanachuoni wacha Mungu kwa sababu mlikuwa mkifundisha kitabu, na kwa sababu mlikuwa mkisoma.
80. Wala hatawaamuruni kuwafanya Malaika na Manabii kuwa ni wenye kuabudiwa je, atawaamrishaje ukafiri baada ya nyinyi kuwa Waislamu?
81. Na kumbukeni Mwenyeezi Mungu aliposhika ahadi kwa Manabii: Nitakapokupeni Kitabu na Hekima, kisha awafikieni Mtume mwenye kuwafikiana na mlicho nacho, mumwamini na mumnusuru. Akawaambia: Je, mmekubali na kushika agizo langu juu ya hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema: Basi shuhudieni, na mimi ni pamoja nanyi katika mashahidi.
82. Basi atakayekataa baada ya hayo, basi hao ndio wavunjao amri.
83. Je, wanataka dini isiyokuwa ya Mwenyeezi Mungu, na hali wamenyenyekea kwake, walio katika mbingu na nchi kwa hiari na kwa nguvu, na Kwake watarejeshwa.
84. Sema: Tumemwamini Mwenyeezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa, na yaliyoteremshwa juu ya Ibrahim na Ismaili na Is’haka na Yaakub na Makabila, na alichopewa Musa na Isa na Manabii kutoka kwa Mola wao. Hatubagui baina yao hata mmoja, na sisi ni wenye kumnyenyekea Yeye.
85. Na anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislam, basi haitakubaliwa Kwake, na yeye katika Akhera ni miongoni mwa wenye khasara.
86. Mwenyeezi Mungu atawaongozaje watu waliokufuru baada ya kuamini kwao, na wakashuhudia kwamba Mtume ni wa haki, na zikawajia dalili zilizo wazi. Na Mwenyeezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
87. Hao malipo yao ni kushukiwa na laana ya Mwenyeezi Mungu na Malaika na watu wote.
88. Ni wenye kudumu humo, hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa nafasi.
89. Isipokuwa waliotubu baada ya hayo na wakasahihisha, basi hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
90. Hakika wale waliokufuru baada ya kuamini kwao, kisha wakazidi kukufuru, haitakubaliwa toba yao, na hao ndio waliopotea.
91. Hakika wale waliokufuru na wakafa hali makafiri, basi haitakubaliwa kwa mmoja wao ijapokuwa kutoa fidia ya dhahabu kwa kujaza ardhi yote. Hao ndio watakaopata adhabu iumizayo, wala hawatakuwa na wasaidizi.
92. Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda, na chochote mnachokitoa, basi Mwenyeezi Mungu hakika anakijua.
93. Vyakula vyote vilikuwa ni halali kwa wana wa Israeli ila kile alichojiharamishia Israeli mwenyewe kabla ya kuteremshwa Taurati. Waambie: Leteni Taurati muisome, ikiwa mnasema kweli.
94.Basi wenye kumzulia Mwenyezi Mungu uongo baada ya hayo, basi hao ndio wenye kudhulumu.
95.Sema: Amesema kweli Mwenyezi Mungu, basi ifuateni mila ya Ibrahim, mtu wa dini ya sawa sawa, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
96.Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu ( kwa ajili ya ibada) ni ile iliyoko Makka yenye kubarikiwa na muongozo kwa viumbe.
97.Humo mna dalili zilizo wazi katika hizo ni mahala aliposimama Ibrahiim. Na mwenye kuingia humo huwa katika amani. Na ni haki ya mwenyezi Mungu juu ya watu kuhiji Nyumba hiyokwa mwenye kuiweza njia ya kwenda. Na anaekataa, basi Mwenyezi Mungu si muhitaji kwa walimwengu
98.Sema: Enyi watu wa kitabu! Kwanini mnazikataa Aya za Mwenyezi Mungu, na hali Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya yale mnayoyatenda?
99.Sema: Enyi watu wa kitabu! Kwanini kumzuilia njia ya Mwenyezi Mungu yule alie amini mkitafuta kupotoa na hali mna shuhudia? Na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda.
100.Enyi mlioamini! Mkiwatii baadhi ya wale waliopewa kitabu, watakurudisheni kuwa makafiri baada ya imani yenu.
101.Na mtakataaje hali nyinyi mnasomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume wake yuko kati yenu? Na mwnye kushikamana na Mwenyezi Mungu, basi amekwisha ongozwa kwenye njia iliyo nyooka.
102.Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mugnu ipasavyo kumcha, wala msife ila nyinyi mu Waislaam.
103. Na shikamaneni na kamba ya Mwenyeezi Mungu nyote wala msifarakane. Na kumbukeni neema ya Mwenyeezi Mungu iliyo juu yenu, mlipokuwa maadui na akaziunganisha nyoyo zenu, hivyo kwa neema yake mkawa ndugu na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto naye akawaokoeni nalo. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anavyokubainishieni dalili zake ili mpate kuongoka.
104. Na wawepo katika nyinyi kundi lenye kulingania kheri, na kuamrisha mema na kukataza maovu, na hao ndio watakao faulu.
105. Wala msiwe kama wale waliofarakana wakakhitilafiana baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi, na hao ndio wenye adhabu kubwa.
106. Siku ambayo nyuso zitakuwa nyeupe, na nyuso (nyingine) zitakuwa nyeusi, Ama ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi (wataambiwa): Mmekufuru baada ya kuamini kwenu? Basi onjeni adhabu kwa sababu mlikuwa mkikataa.
107. Ama ambao nyuso zitakuwa nyeupe, watakuwa katika rehema ya Mwenyeezi Mungu, wao humo ni wenye kukaa milele.
108. Hizo ni Aya za Mwenyeezi Mungu tunakusomea wewe kwa haki, na Mwenyeezi Mungu hataki dhulma kwa walimwengu.
109. Na vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ni vya Mwenyeezi Mungu na kwa Mwenyeezi Mungu hurejezwa mambo yote.
110. Nyinyi ni kundi bora mliotolewa kwa ajili ya watu, mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamwamini Mwenyeezi Mungu. Na kama watu wa Kitabu wangeamini ingelikuwa bora kwao, katika wao kuna ambao wameamini na wengi wao ni wenye kutoka kwenye twaa.
111. Hawatakudhuruni isipokuwa ni kuwaudhi (kwa maneno) tu, na watakapopigana nanyi watawakimbieni kisha hawatasaidiwa.
112. Wamepigwa na udhalili popote walipo ila kwa (kushika) Sharia ya Mwenyeezi Mungu na kanuni za watu, na wamerudi na hasira ya Mwenyeezi Mungu na umasikini umepigwa juu yao. Hayo ni kwa sababu ya wao kutoamini dalili za Mwenyeezi Mungu, na kuwaua Manabii pasipo na haki. Hayo ni kwa sababu waliasi na walikuwa wakiruka mipaka.
113. Hawakuwa wote sawasawa, katika watu wa Kitabu kuna watu wanaosimama wakasoma Aya za Mwenyeezi Mungu nyakati za usiku na huku wakinyenyekea.
114. Wanamwamini Mwenyeezi Mungu na siku ya Mwisho na wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanaharakia mambo mema, na hao ni miongoni mwa watu wema.
115. Na kheri yoyote watakayoifanya hawatakosezwa (malipo yake) na Mwenyeezi Mungu anawajua wamchao.
116. Hakika wale waliokufuru hayatawafaa kitu mali yao wala watoto wao kwa Mwenyeezi Mungu, na hao ndio watu wa Motoni, wao humo ni wenye kukaa milele.
117. Mfano wa vile wanavyotoa katika maisha haya ya dunia ni kama upepo (ambao) ndani yake mna baridi kali uliofikilia mmea wa watu waliodhulumu nafsi zao na ukaliangamiza. Na Mwenyeezi Mungu hakuwadhulumu, lakini wao wenyewe wanajidhulumu.
118. Enyi mlioamini! msiwafanye wasiri (wenu) watu wasiokuwa nyinyi, hawataacha kukufanyieni ubaya. Wanayapenda yale yanayokudhuruni, bila shaka bughdha imedhihirika katika midomo yao, na yanayoficha vifua vyao ni makubwa zaidi. Hakika tumekubainishieni dalili ikiwa nyinyi mnafahamu.
119.Nyinyi ndiyo ambao mnawapenda wala wao hawawapendi na mnaamini kitabu chote. Na wanapokutana nanyi husema: Tumeamini, na wakiwa peke yao, wanakuumieni vidole kwa hasira. Waambieni: Kufeni na hasira yenu, hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani.
120. Kama likiwafikia jema, (wao)huwaudhi na likiwafikia baya, hulifurahia. Na mkisubiri na kumcha ( Mwenyezi Mungu) hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayoyatenda.
121. Na ( kumbuka) ulipotoka asubuhi ukaacha ahali zako kuwaweka waumini mahala pakupigana , na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia, mjuzi.
122. ( kumbuka) makundi mawili katika nyinyi yalipotaka kufanya woga na hali Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyanusuru, na kwa Mwenyezi Mungu wategemee wenye kuamini.
123.Na bila shaka Mwenyezi Mungu alikusaidieni katika ( vita vya) Badri hali nyinyi ni madhalili. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru.
124.Ulipowaambia wenye kuamini: Je, haiwatoshi Mola wenu kuwasaidieni kwa Malaika elfu tatu wenye kuteremshwa?
125. Kwanini, ( inawatosha) kama mkisubiri na kumcha Mungu na watakufikieni katika wakati wao huu, atawasaidia Mola wenu kwa Malaika elfu tano wenye kushambulia kwa nguvu.
126. Na Mwenyezi Mungu hakufanya ila ni bishara kwenu, na zipate tumaini nyoyo zenu. Na msaada hautoki ( popote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
127. Ili apate kuliangamiza kundi katika wale waliokufuru au awadhalilishe, warejee hali wameshindwa.
128. (Wewe) huna neno katika shauri (hili) awakubalie toba yao au awaadhibu, maana hakika wao ni madhalimu.
129. Ni vya Mwenyeezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini humsamehe amtakaye na humwadhibu amtakaye, na Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
130. Enyi mlioamini! msile riba mkizidisha zidisha, na mcheni Mwenyeezi Mungu ili mpate kufaulu.
131. Na ogopeni Moto ambao umeandaliwa makafiri.
132. Na mtiini Mwenyeezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa.
133. Na harakieni kuomba msamaha kwa Mola wenu na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na nchi iliyoandaliwa kwa wenye kumcha Mwenyeezi Mungu.
134. Ambao hutoa (mali yao) katika raha na katika shida na wenye kujizuia na ghadhabu na wenye kuwasamehe watu, na Mwenyeezi Mungu hupenda wafanyao wema.
135. Na wale ambao wanapofanya uchafu au wakidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyeezi Mungu wakaomba msamaha wa madhambi yao, na ni nani anayesamehe madhambi isipokuwa Mwenyeezi Mungu, na hawaendelei na (maovu) waliyoyafanya hali wanajua.
136. Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao, na Bustani zinazopita mito chini yake. Ni wenye kukaa milele humo, na wema ulioje ujira wa watendao.
137. Bila shaka mifano mingi imepita kabla yenu, basi nendeni katika ardhi muone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.
138. Haya ndiyo maelezo yaliyo wazi kwa watu na muongozo na mawaidha kwa wenye kumcha.
139. Na msilegee wala msihuzunike maana nyinyi ndio wenye kutukuka ikiwa ni wenye kuamini.
140. Kama mmepata jeraha, basi hao watu wamekwisha patajeraha kama hilo, na siku za namna hii tunawaletea watu kwa zamu, na ili Mwenyeezi Mungu apate wajua wale walio amini katika nyinyi, na ili awafanye mashahidi katika nyinyi na Mwenyeezi Mungu hawapendi wenye kudhulumu.
141. Na ili Mwenyeezi Mungu awatakase walioamini, na awaangamize makafiri.
142. Je, mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyeezi Mungu hajawajua wale waliofanya jihadi katika nyinyi na kuwajua wenye kusubiri.
143. Na kwa hakika mlikuwa mkiyatamani mauti kabla ya kuyakuta, basi mmekwisha yaona nanyi mnatazama.
144. Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume aliyepitiwa na Mitume kabla yake. Basi je, akifa au akiuliwa mtarudi nyuma kwa visigino vyenu? na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru kitu Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu atawalipa wanaoshukuru.
145. Na nafsi haiwezi kufa ila kwa amri ya Mwenyeezi Mungu, kwa muda uliowekwa. Na anayetaka malipo ya dunia tutampa humo, na anayetaka malipo ya Akhera tutampa huko na tutawalipa wanaoshukuru.
146. Na Manabii wangapi (ambao) Wanachuoni wacha Mungu walipigana pamoja nao, na hawakulegea kwa yale yaliyowapata katika njia ya Mwenyeezi Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakudhalilika, na Mwenyeezi Mungu huwapenda wenye kusubiri.
147. Wala halikuwa neno lao ila ni kusema: Molawetu! tusamehe madhambi yetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu na uimarishe miguu yetu na utusaidie juu ya watu makafiri.
148. Mwenyeezi Mungu akawapa malipo ya dunia na malipo mema ya Akhera, na Mwenyeezi Mungu anawapenda wenye kufanya mema.
149. Enyi mlioamini! ikiwa mtawatii waliokufuru watakurejesheeni kwa visigino vyenu (hivyo) mtageuka kuwa wenye hasara.
150. Lakini Mwenyeezi Mungu ndiye Mlinzi wenu naye ndiye bora wa wasaidizi.
151. Tutatia khofu katika nyoyo za wale waliokufuru kwa sababu ya kumshirikisha Mwenyeezi Mungu (na kitu) ambacho hakukiteremshia dalili, na makazi yao ni Moto, nayo ni makazi mabaya ya wenye kudhulumu.
l52. Na bila shaka Mwenyeezi Mungu amewatimizia miadi yake mlipowaua kwa idhini yake mpaka mlipolegea na mkagombana katika amri, na mkakhalifu baada ya kuwaonyesha mkipendacho. Wako miongoni mwenu wanaopenda dunia na wako miongoni mwenu wanaopenda Akhera. Kisha akawaepusha nao ili awajaribu, na hakika amekwisha wasamehe, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye wema juu ya wenye kuamini.
153. (Kumbukeni) mlipokuwa mkikimbia mbio wala hamkumtazama yeyote na hali Mtume akiwaiteni nyuma yenu. Kisha akakupeni (Mwenyeezi Mungu) dhiki juu ya dhiki ili msipate kusikitika kwa yale yaliyo kupoteeni wala kwa yale yaliyokupateni. Na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa yale mnayoyatenda.
154. Kisha akawateremshia baada ya huzuni amani ya usingizi ukawafunika kundi moja katika nyinyi, na kundi jingine limeshughulishwa na nafsi zao, wakimdhania Mwenyeezi Mungu lisilokuwa haki, dhana ya kikafiri. Husema: Tuna kitu katika jambo hili? Waambie: Hakika mambo yote ni ya Mwenyeezi Mungu. Hulificha katika nafsi zao ambalo hawakudhihirishii. Husema: Tungekuwa na chochote katika jambo hili tusingeuawa hapa. Waambie: Kama mngekuwa majumbani mwenu bila shaka wangetoka wale walioandikiwa kuuawa kwenda mahala pa maangamivu yao. Na ili Mwenyeezi Mungu ajaribu yaliyomo vifuani mwenu, na kusafisha yaliyomo nyoyoni mwenu. Na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo vifuani.
155. Hakika wale waliokimbia miongoni mwenu siku yalipo kutana makundi mawili, ni shetani ndiye aliyewatelezesha kwa sababu ya baadhi ya waliyoyachuma. Na Mwenyeezi Mungu amekwisha wasamehe, bila shaka Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mpole.
156. Enyi mlioamini! msiwe kama wale waliokufuru na wakasema juu ya ndugu zao, waliposafiri katika nchi au walipokuwa vitani. Wangekuwa kwetu wasinge likufa wala wasingeuliwa. Ili Mwenyeezi Mungu ayafanye hayo kuwa majuto katika nyoyo zao. Na Mwenyeezi Mungu anahuisha na kufisha, na Mwenyeezi Mungu anaona mnayoyatenda.
157. Na kama mkiuliwa katika njia ya Mwenyeezi Mungu au mkifa, basi msamaha na rehema kutoka kwa Mwenyeezi Mungu ni bora kuliko vile wanavyokusanya.
158. Na kama mkifa au mkiuliwa, ni kwa Mwenyeezi Mungu ndiko mtakakokusanywa.
159. Basi kwa sababu ya rehema ya Mwenyeezi Mungu umekuwa laini kwao na kama ungekuwa mkali mshupavu wa moyo, wangekukimbia. Basi wasamehe na uwaombee msamaha na ushauriane nao katika mambo, na unapoazimia basi mtegemee Mwenyeezi Mungu, hakika Mwenyeezi Mungu anawapenda wenye kumtegemea.
160. Akikusaidieni Mwenyeezi Mungu, hapanayeyote mwenye kuwashinda na kama akiwaacheni ni nani atakayekusaidieni baada yake? Na kwa Mwenyeezi Mungu peke yake wategemee wenye kuamini.
161. Wala haiwi kwa Nabii yeyote kufanya khiyana na atakayefanya khiyana atayaleta siku ya Kiyama aliyoyakhini, kisha kila mtu atalipwa aliyoyachuma, na wao hawatadhulumiwa.
162. Je aliyefuata radhi ya Mwenyeezi Mungu ni kama yule aliyestahiki ghadhabu ya Mwenyeezi Mungu, na makazi yake ni Jahannam? napo ni mahala pabaya pa kurejea.
163. Wao ni wenye vyeo mbele ya Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye kuyaona wanayoyatenda.
164. Bila shaka, Mwenyeezi Mungu amewaneemesha Waumini aliowapelekea Mtume miongoni mwao, akiwasomea Aya zake na akiwatakasa na akiwafunza Kitabu na hekima na ingawa zamani walikuwa katika upotovu ulio wazi.
165. Je, ulipowafikia msiba (mmoja) hali nyinyi mmekwisha watia mara mbili ya huo husema: Umetoka wapi huu? Waambie: Huo umetoka kwenu wenyewe. Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
166. Na hayo yaliyowafikia nyinyi siku yaliyokutana makundi mawili ni kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu, na ili awajue wenye kuamini,
167. Na ili awajue ambao wamefanya unafiki. Na wakiambiwa: Njooni mpigane katika njia ya Mwenyeezi Mungu au mjitetee. Husema: Tungelijua kupigana tungewafuateni. Wao siku ile walikuwa karibu zaidi na kufuru kuliko imani. Husema kwa midomo yao yasiyokuwamo nyoyoni mwao, na Mwenyeezi Mungu anajua sana wanayoyaficha.
168. Wale waliosema juu ya ndugu zao, na hali wamekaa (hawakwenda vitani) Kama wangetutii wasingeuliwa. Waambie: Jiondoleeni mauti ikiwa mnasema kweli.
169. Wala usidhani wale walio uliwa katika njia ya Mwenyeezi Mungu kuwa ni wafu, bali ni hai wanaruzukiwa kwa Mola wao.
170. Ni wenye furaha kwa ihisani ya Mwenyeezi Mungu aliyowapa, na wanawafurahikia walio nyuma yao ambao hawajawafuata, kwamba hapana khofu juu yao wala wao hawatahuzunika.
171. Wanafurahikia neema ya Mwenyeezi Mungu na ihisani yake, na kwamba Mwenyeezi Mungu hazipotezi thawabu za wenye kuamini.
172. Wale walio mwitikia Mwenyeezi Mungu na Mtume baada ya kuwapata majeraha kwa wale waliofanya wema miongoni mwao na kumcha Mungu wana malipo makubwa.
173. Wale ambao watu waliwaambia: Hakika watu wamekwisha wakusanyikieni, basi waogopeni (hilo) likawazidisha imani na wakasema: Mwenye kututosha ni Mwenyeezi Mungu, na ni Mbora wa kutegemewa.
174. Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyeezi Mungu, hawakuguswa na ubaya na wakafuata radhi ya Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.
175. Hakika huyo ni shetani huwatia khofu marafiki zake, basi msiwaogope, niogopeni Mimi ikiwa nyinyi ni wenye kuamini.
176. Wala wasikuhuzunishe ambao hufanya haraka kukataa, hakika wao hawatamdhuru kitu Mwenyeezi Mungu. Anataka Mwenyeezi Mungu asiwawekee fungu lolote huko Akhera, na wana adhabu kubwa.
177. Hakika wale walionunua kufru kwa imani hawataweza kumdhuru Mwenyeezi Mungu chochote, na wana adhabu yenye kuumiza.
178. Wala wasidhani wale waliokufuru kwamba muda tunaowapa ni bora kwao, hakika tunawapa muda ili wazidi maovu, na wana adhabu yenye kudhalilika.
179. Hakuwa Mwenyeezi Mungu kuwaacha Waumini katika hali mliyo nayo mpaka apambanue wabaya na wazuri, wala hakuwa Mwenyeezi Mungu kuwajulisheni mambo ya ghaibu, lakini Mwenyeezi Mungu huchagua katika Mitume yake amtakaye. Basi mwaminini Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, na kama mtaamini na mkamcha (Mwenyeezi Mungu) basi mna malipo makubwa.
180. Wala wasidhani wale wanaofanya ubakhili katika fadhila zake kuwa ni bora kwao, bali ni vibaya kwao, watafungwa kongwa za yale waliyofanyia ubakhili siku ya Kiyama. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu ni Mjuzi wa mnayoyafanya.
181. Kwa hakika Mwenyeezi Mungu amesikia kauli ya wale waliosema:
Mwenyeezi Mungu ni masikini na sisi ni matajiri. Tutayaandika waliyoyasema, na kuua kwao Manabii bila ya haki, na tutawaambia: Onjeni adhabu ya kuungua.
182. Hilo ni kwa sababu ya yaliyotangulizwa na mikono yenu na kwamba Mwenyeezi Mungu si dhalimu kwa waja.
183. Wale waliosema: Hakika Mwenyeezi Mungu ametuahidi kwamba tusimwamini Mtume yeyote mpaka atutolee sadaka itakayoliwa na Moto. Waambie: Bila shaka wamekuja kwenu Mitume kabla yangu na dalili zilizo wazi na kwa yale mliyoyasema: Basi kwanini mliwaua ikiwa nyinyi ni wenye kusema kweli.
184. Na kama wakikukadhibisha basi wamekwisha kadhibishwa Mitume kabla yako, waliokuja na dalili zilizo wazi na Vitabu vyenye waadhi na Kitabu chenye nuru.
185. Kila nafsi itaonja mauti na bila shaka mtapewa malipo yenu siku ya Kiyama, na mwenye kuepushwa na Moto akatiwa Peponi, basi amefaulu, na haukuwa uhai wa ulimwengu ila ni raha ya udanganyifu.
186. Hapana shaka mtapata misukosuko katika mali zenu na nafsi zenu, na bila shaka mtasikia udhia mwingi kutoka kwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu na wale walio shiriki. Na ikiwa mtasubiri na mkamcha Mungu, basi hakika hayo ni katika mambo ya kuazimia.
187. Na (kumbukeni) Mwenyeezi Mungu alipofunga ahadi nawale waliopewa Kitabu: Lazima mtakibainisha kwa watu wala hamtakificha. Wakaitupilia mbali (ahadi hiyo) nyuma ya migongo yao, na wakaiuza kwa thamani ndogo, basi ni mabaya mno wanayoyanunua.
188. Usidhani wale wanaofurahia mambo waliyoyafanya, na wanapenda kusifiwa kwa yale wasiyoyafanya, basi usidhani wao watasalimika na adhabu, na wana adhabu yenye kuumiza.
189. Na ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
190. Hakika katika kuumba mbingu na ardhi na kutofautiana kwa usiku na mchana ni dalili kwa wenye akili.
191. Ambao humkumbuka Mwenyeezi Mungu wakiwa wima na wakikaa na wakilala na wanafikiri katika umbo la mbingu na nchi (wakasema) Mola wetu! hukuviumba hivi bure, utukufu ni wako, basi tuepushe na adhabu ya Moto.
192. Mola wetu! hakika wewe utakayemtia Motoni utakuwa umemdhalilisha, na wenye kudhulumu hawatakuwa na wenye kuwanusuru.
193. Mola wetu! hakika tumemsikia mwitaji anayeita kwenye imani kwamba:
Mwaminini Mola wenu, nasi tukaamini. Mola wetu! tusamehe madhambi yetu na utufutie maovu yetu na utufishe pamoja na watu wema.
194. Mola wetu! na umpe uliyotuahidi kwa Mitume wako wala usitufedheheshe siku ya Kiyama, hakika wewe huvunji miadi.
195. Akawakubalia Mola wao kwamba; Mimi sitapoteza malipo ya menye kufanya miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, ni nyinyi kwa nyinyi. Basi wale waliohama na wakafukuzwa katika majumba yao na wakaudhiwa katika njia ya Mwenyeezi Mungu na wakapigana na kuuawa, hakika nitawafutia makosa yao, na hakika nitawaingiza katika Mabustani yanayopita mito chini yake, malipo kutoka kwa Mwenyeezi Mungu, na Mwenyeezi Mungu kwake kuna malipo mema.
196. Usikudanganye mwendo wa wale waliokufuru katika miji.
197. (Hiyo) ni starehe chache, kisha makao yao ni Jahannam na ni mahala pabaya mno pa kupumzikia.
198. Lakini wale waliomcha Mola wao watapata Mabustani yanayopita mito chini yake watakaa milele humo, makaribisho toka kwa Mola wao, na yaliyoko kwa Mwenyeezi Mungu ni bora kwa watu wema.
199. Na hakika katika watu wa Kitabu wako wanaomwamini Mwenyeezi Mungu na yaliyoteremshwa kwenu na yaliyoteremshwa kwao ‘kwa kunyenyekea kwa Mwenyeezi Mungu. Hawauzi Aya ya Mwenyeezi Mungu kwa thamani ndogo hao wana malipo yao mbele ya Mola wao, hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.
200. Enyi mlioamini! subirini na muwashinde (makafiri) katika kusubiri, na kuweni imara, na mcheni Mwenyeezi Mungu ili mpate kufaulu.