Sura Dukhan

Sura hii imeteremshwa Makka, ina Aya 59

Kwa jina la Mwenyeezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

1. Haa Mym.

2. Naapa kwa Kitabu kinachobainisha.

3. Kwa hakika tumeiteremsha (Qur’an) katika usiku uliobarikiwa, bila shaka sisi ni waonyaji.

4. Katika (usiku) huu hubainishwa kila jambo la hekima.

5. Ndiyo hukumu inayotoka kwetu, kwa hakika sisi ni waletao (Mitume).

6. Ni rehema itokayo kwa Mola wako, bila shaka yeye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

7. Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake, ikiwa mnayo yakini.

8. Hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, anahuisha na kufisha, Mola wenu na ni Mola wa baba zenu wa mwanzo.

9. Lakini wao (makafiri) wamo katika shaka wakicheza.

10. Basi ingoje siku ambayo mbingu itakapoleta moshi dhahiri.

11. Utakaowafunika watu, hii ni adhabu yenye kuumiza.

12. Mola wetu! tuondolee adhabu, hakika tunaamini.

13. Wataupataje ukumbusho? na amekwisha wafikia Mtume abainishaye.

14. Kisha wakampa mgongo na wakasema: Amefunzwa, Mwenda wazimu.

15. Kwa hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo (lakini) nyinyi mtarudia

(makosa).

16. Siku tutakayo shambulia shambulio kubwa, bila shaka sisi ni wenye kutesa,

17. Na hakika kabla yao tuliwajaribu watu wa Firaun na aliwafikia Mtume aheshimiwaye.

18. (Akasema) Nipeni waja wa Mwenyeezi Mungu kwa hakika mimi ni Mtume mwaminifu kwenu.

19. Na msijitukuze mbele ya Mwenyeezi Mungu mimi kwa hakika nitakuleteeni dalili iliyo wazi.

20. Nami naiikinga kwa Mola wangu na Mola wenu ili msinipige mawe.

21. Na kama hamniamini, basi jitengeni nami.

22. Ndipo akamuomba Mola wake kuwa, hao ni watu waovu.

23. Basi nenda pamoja na waja wangu usiku, hakika nyinyi mtafuatwa.

24. Na iache bahari inapokupwa, hakika wao ni jeshi litakalozamishwa.

25. Mabustani mangapi na chem chem waliziacha!

26. Na mimea na mahala pazuri!

27. Na neema walizokuwa wakijistarehesha.

28. Ndivyo hivyo, na tukazirithisha watu wengine.

29. Mbingu na ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muda.[1]

30. Na bila shaka tuliwaokoa wana wa Israeli katika adhabu yenye kufedhehesha.

31. Ya Firaun, hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka.

32. Na tukawachagua (Mayahudi) kwa ujuzi kuliko walimwengu (wa zama hizo).

33. Na tukawapa katika mambo (yetu) ambayo ndani yake mna neema zilizo dhahiri.

34. Hakika hao wanasema.

35. Hayo siyo ila ni maut.i yetu ya kwanza wala sisi hatutafufuliwa.

36. Basi warudisheni baba zetu ikiwa mnasema kweli.

37. Je, wao ni bora au watu wa Tubbaa, na wale waliokuwa kabla yao? tuliwaangamiza, kwa sababu wao walikuwa waovu.

38. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake kwa mchezo.

39. Hatukuviumba ila kwa haki, lakini wengi wao hawaiui.

40. Hakika siku ya hukumu ni wakati uliowekwa kwa wao wote.

41. Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki chochote, wala hawatasaidiwa.

42. Ila yule Mwenyeezi Mungu atakayemrehemu, hakika yeye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

43. Bila shaka mti wa Zakkum.

44. Ni chakula cha mwenye dhambi.

45. Kama shaba iliyoyeyuka, huchemka matumboni.

46. Kama mchemko wa maji ya Moto.

47. Mkamateni na mburureni mpaka kati kati ya Jahannam.

48. Kisha mwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji ya Moto.

49. Onja! hakika wewe ndiye mwenye nguvu, mheshimiwa!

50. Hakika hii ndiyo mliyokuwa mkibishana.

51. Bila shaka wale wamchao Mwenyeezi Mungu watakuwa katika mahala pa amani.

52. Katika Mabustani na chemchem.

53. Watavaa hariri laini na hariri nzito, wakikabiliana (kwa mazungumzol.

54. Hivyo ndivyo itakavyokuwa, na tutawaoza mahuuru a’yn.

55. Humo watataka kila aina ya matunda na wakae kwa amani.

56. Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza na atawalinda na adhabu ya Jahannam.

57. Kwa fadhili zitokazo kwa Mola wako, huko ndiko, kufaulu kukubwa.

58. Basi tumeifanya nyepesi (hii Qur’an) kwa ulimi wako ili wakumbuke.

59. Kwa hiyo ngoja, hakika wao (pia) wanangoja.